24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Uchunguzi wa kina unahitajika ajali ya Tarime

WIKI hii taifa limepoteza watu 15 kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha mabasi madogo ya kusafirisha abiria wilayani Tarime mkoani Mara.

Ajali hiyo, ilihusisha magari aina ya Toyota Hiace zinazosafirisha abiria katika ya mji wa Musoma na Tarime ambazo ziligongana uso kwa uso kisha moto mkubwa ukawaka.

Moto huo ulisababisha watu 15 kupoteza uhai kwa kuungua vibaya na kuteketea kabisa, kitendo ambacho kimefanya hata mili yao ishindwe kutambuliwa na ndugu zao.

Ni ajali mbaya ambayo kwa kweli tunaweza kusema imeacha maumivu makubwa si kwa familia tu, bali kwa taifa na kuibua maswali mengi.

Lakini katika ajali hii, watu wanne walinusurika japo wapo waliovunjika miguu na mikono, huku wakiungua vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.

Hivi sasa wamelezwa Hospitali ya Rufaa Bugando mkoani Mwanza wakiendelea na matatibu.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amesema Serikali imeamua kuzika miili hiyo sehemu katika eneo ambalo kulitokea ajali.

Alisema uamuzi huo, umechukuliwa na Serikali kutokana miili hiyo kushindwa kutambuliwa na ndugu zao, baada ya kuharibika vibaya, lakini  miili hiyo itachukuliwa sampuli za vipimo vya vinasaba (DNA) ili ndugu watakapojitokeza waweze kuitambua.

Tunakubaliana na Malima kutokana na ukweli kwamba miili hiyo, haiwezi kutambuliwa mara moja, lakini kuna mambo kadhaa ambayo sasa umefika wakati Serikali lazima iyafanye.

Mosi, Serikali kupitia mamlaka zake za usafirishaji ianze kuweka utaratibu wa kila daladala kuandika majina ya abiria wao wanapanda kuanzia kwenye vituo vikubwa na kuyakabidhi polisi.

Kwa mfano gari imeanza safari stendi kuu ya mabasi Musoma mjini, inashindikana nini kuandika majina ya abiria wote waliomo ndani na yakakabidhiwa kwa askari wa usalama barabarani ambao wako kwenye vituo hivi.

Kwa kufanya hivi tunaamini kutasaidia pindi inatokea ajali mbaya kama hii, majina ya abiria yakatambulika mara moja hata kama ndugu zao watashindwa kuitambua kutokana na kuungua vibaya.

Haiwezekani Watanzania wakaendelea kupoteza maisha kiasi hiki, halafu mamlaka zilizopewa dhamana zipo hazikuni vichwa sawa sawa namna ya kupata ufumbuzi wa matukio haya.

Wote tunatambua wazi  ajali haipangwi, lakini kama tukaweka utaratibu wa kuandika majina ya wasafiri wetu itsaidia.

Mbona katika vituo hivyo mabasi makubwa ya abiria yote huacha nakala ya majina kwa askari kabla ya kuvuka geti kuu la kutokea?

Pamoja na yote hayo, tumesikitishwa na kitendo cha polisi wilayani Tarime mpaka sasa kushindwa kueleza umma kwa kina chanzo cha ajali hii.

Maana kila mtu anajiuliza na kukosa majibu ilikuwaje hadi abiria hawa wakashindwa kuaokolewa ndani ya magari haya.

Sisi MTANZANIA, kwanza tunazipa pole familia zote ambazo zimepatwa na msiba huu mzito ambao umepoteza wapendwa wao, tunajua wapo wazazi walioacha watoto, wapo watoto walioacha wazazi wao na wengine kupata vilema vya kuduma, tunasisitiza kuwa uchunguzi wa kina wa ajali hii unahitajika ili Watanzania ajali hii imetokeaje.

Tunaishauri Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano kukaa chini na kuangalia namna ya kuanza kuzibana hizi daladala na namna ya kuacha majina ya wasafiri kwenye stendi kuu.

Japo tunaamini zikiwa safarini huendelea kupanda abiria wengine ambao kimsingi hawawezi kufikia idadi ile ambayo wanatoka nayo kituoni.

Tunamalizia kwa kuwapa pole wafiwa wote na Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi-amina.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles