29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

UCHUMI WA VIWANDA WAHITAJI MAENEO TENGEFU

Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

KATIKA kuhakikisha Tanzania inafika uchumi wa kati, Serikali iliamua kutumia utaratibu wa kutenga maeneo tengefu ya viwanda (special economic zones) ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zitakazowezesha uendeshaji wa viwanda hivyo.

Pamoja na kutengwa kwa maeneo hayo, bado yanakabiliwa na changamoto za hapa na pale kama vile ukosefu wa miundombinu ya barabara za kuelekea katika maeneo husika na miundombinu ya maji, hali ambayo inaweza kuwa kikwazo kwa wawekezaji.

Kutokana na hali hii, Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania inaiomba Serikali kuweka mazingira wezeshi katika maeneo tengefu ya viwanda, ikiwa ni pamoja na vivutio maalumu vya kodi na visivyo vya kodi ili kuongeza kasi ya uzalishaji wa viwanda kwenye maeneo hayo.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkamu Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte, alisema mfumo huo umetumika kwa mafanikio makubwa nchi za Asia hasusan China, India, Vietnam, Malaysia, Singapore na nchi nyingine nyingi.

Anasema baadhi ya nchi za bara la Afrika kama vile Kenya, Ethiopia, Uganda, Ghana na Rwanda ziliiga mfumo huo na kujipatia mafanikio makubwa, huku nyingine nyingi zikiwa mbioni kuiga mfumo huo.

Anasema utafiti waliofanya unaonesha kwamba changamoto nyingi za wawekezaji wa viwanda zinawakumba wale ambao wako nje ya maeneo yaliyotengwa na ambayo yako chini ya EPZ.

“Maoni ya sekta binafsi kwamba njia pekee ya kuharakisha uchumi wa viwanda katika nchi yetu, ni kutumia mfumo wa kuwa na maeneo tengefu ya viwanda na ambayo yamejengewa miundombinu yote.

“Ili mwekezaji yeyote wa nje au wa ndani anayetaka kuwekeza kwenye kiwanda chake, anaonyeshwa sehemu ya jengo, analipia tu kodi ya pango, anasimika mashine zake na anaanza uzalishaji” alisema Shamte.

Shamte anaishukuru Serikali kwa juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na uhusiano baina yake na sekta binafsi.

Shamte anasema katika mkutano wao mkuu wa mwaka huu, umebebwa na dhima ya kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji katika viwanda kupitia ubia kati ya umma na sekta binafsi katika kuendeleza maeneo tengefu ya viwanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye, anaamini kuwa kuimairishwa kwa maeneo tengefu kutarahisisha uzalishaji kutokana na upatikanaji wa huduma muhimu kama vile umeme, maji na miundombinu mingine.

Profesa Damian Gabagambi ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokine (SUA) na Mtaalamu wa masuala ya Uchumi, anasema mpango wa kutenga maeneo tengefu ni miongoni mwa jitihada za Serikali kuelekea uchumi wa kati.

Utekelezaji wa malengo hayo uligawanywa katika sehemu mbili, ikiwa ni yale ya muda wa kati unaolenga kufikia uchumi wa kati hadi 2020 kwa kutumia mpango unaofahamika kama ‘Economic Processing Zones’ (EPZ).

Profesa Gabagambi anaufananisha mpango huu na kujenga kiota kisha ukawavutia ndege kuingia katika kiota hicho, ambapo mfumo huu huwalenga wawekezaji wtakaokuwa na uwezo wa kuuza nje ya nchi asilimia 80 ya bidhaa wanazozalisha.

Katika mpango huu, Serikali hutoa motisha na vivutio mbalimbali kwa wawekezaji hao ikiwa ni pamoja na kupunguziwa kiwango cha kodi, gharama za umeme maji na huduma nyingine.

Mpango mwingine unaolenga kufikia uchumi wa kati kwa kutumia sekta ya viwanda ni ule unaolenga mwaka 2030, ambao hutekelezwa kwa mtindo wa kuwa na maeneo tengefu ya viwanda ambayo hupewa huduma zote muhimu kama vile maji, miundombinu ya barabara au reli na umeme ili kuwavutia wawekezaji wengi na kurahisisha uzalishaji.

Tofauti na EPZ, mpango huu mwekezaji huuza bidhaa zake popote bila ya kupangiwa na Serikali wapi wauze bidhaa zinazozalishwa.

“Kinachotakiwa ni kuya-‘promote’ hayo maeneo na huduma zinazopatikana yaweze kufahamika sehemu nyingi duniani sambamba na kushawishi wawekezaji kuja kuona fursa zinazopatikana katika maeneo hayo.

Si lazima kupeleka umeme moja kwa moja katika maeneo ya uzalishaji lakini umeme wa Gridi ni vizuri ukasogezwa karibu na maeneo hayo ili wawekezaji wasisubiri kwa muda mrefu wanapohitaji huduma hiyo,” anasema Profesa Gabagambi.

Anaamini kuwa kinachopaswa kufanyika ni kuhakikisha kunakuwa na mwendelezo wa yale yaliyoanzishwa na si kila anapokuja mkurugenzi mpya anaanza na lake, bali uwe ni utaratibu wa muda mrefu anapokuja mwekezaji anaelekezwa wapi anaweza kuwekeza.

Anasema mitindo hii yote miwili imesaidia kuleta mageuzi ya viwanda katika mataifa mbalimbali barani Ulaya na Asia ikiwamo India.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles