Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wachimbaji wa madini wametakiwa kuzingatia uchimbaji salama katika maeneo ya migodi yao ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji madini kwa tija na migodi iendelee kubaki salama.
Hayo yamebainishwa leo Jumatano Desemba 29, 2021 na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko alipokutana na kuzungumza na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la machimbo la Nyamalimbe Makarashani lililopo wilaya ya Geita mkoani humo.
Dk. Biteko amewaagiza wakaguzi wa migodi katika machimbo hayo kuhakikisha wanaweka utaratibu wa daftari kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu kwa kusainisha majina ya wachimbaji wanaoingia na kutoka kwenye maduara.
“Tuna watoto bado tunazaa wanahitaji madarasa, kuna akina mama wanajifunzua tunahitahitaji huduma bora za afya, maji safi, miundombinu bora na vitu vingine vingi ambavyo tunatamani vifanyike kupitia madini yetu.
“Lakini ukweli ni kwamba bado madini yetu yalikuwa hayatunufaishi kwani ukiangalia hali ya watu na sifa ya madini inayohubiriwa ni vitu viwili tofauti kwani tunao utajiri lakini unawanufaisha watu wengine na ndiyo maana Rais wetu Samia Suluhu Hassan anataka kuona utajiri huo ukibaki miongoni mwa Watanzania wenyewe,” amesema Dk. Biteko na kutoa wito kwa wachimbaji hao kusimamia kila gramu inayopatikana iende sokoni.
Aidha, katika hatua nyingine Dk. Biteko amesema Serikali inataka watu wenye leseni ya kununua madini huku akihimiza kuanzishwa kwa soko la madini katika eneo la Nyamalimbe badala ya kwenda Katoro.