27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 7, 2024

Contact us: [email protected]

UCHIMBAJI MADINI KINYWE EPANKO WAFIKIA HATUA MUHIMU  

 

Na Hassan Bumbuli, Dar es Salaam


TANZANIA inajiandaa kuwa moja ya mataifa yanayozalisha kwa wingi madini ya Kinywe maarufu kama Graphite ambapo kama miradi yote itakamilika itakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 384,000 kwa mwaka.

Uwezo huo ambao unakadiriwa katika miradi mitatu mikubwa ya Nachu wenye uwezo wa kuzalisha tani 240,000, mradi wa Namangale wenye uwezo wa kutoa tani 100,000 pamoja na ule wa Epanko wenye uwezo wa kuzalisha tani 44,000.

Miradi hiyo mtatu mikubwa ikikamilika yote na kuanza kufanya kazi, itaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa madini hayo Duniani ikitanguliwa na China ambayo inazalisha zaidi ya tani 700,000 kwa mwaka huku nchi zingine kama India ikishika nafasi ya tatu kwa kuzalisha tani 170,000 na Brazil nafasi ya nne kwa tani 80,000.

Kati ya miradi yote mitatu ya madini ya Graphite, Mradi wa Epanko ulioko katika kijiji cha Epanko, mji wa  Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro ndiyo mradi ambao unaonekana kuiva na kukaribia kuanza kuzaa matunda muda sio mrefu kwani wahusika wote wako tayari na kusubiri kauli ya Mthamini Mkuu. Ni hali  kama ya kupakua  na kula.

Mradi huo kwa sasa sasa umeingia katika hatua nzuri baada ya Kampuni inayowekeza katika mradi huo ya TanzGraphite kuanza kukamilisha mahitaji muhimu ya mradi huo ikiwamo mpango  utekelezaji (action Plan).

Kinachosubiriwa  ni kupitishwa   rasimu ya fidia na        Mthamini Mkuu  ili fidia zianza kutolewa kwa wale walioridhia mpango husika  na kuwekeana  saini mambo muhimu ya mradi.

Mradi huo ambao ni moja ya miradi mikubwa ya uchimbaji madini hayo hapa nchini na Afrika kwa ujumla  umepitia katika  hatua kadhaa ambapo baada ya kukamilika kwa hatua ya utafiti kampuni hiyo kwa idhini ya serikali walianza mchakato shirikishi wa kufanya tathmini na uthaminishaji wa mali, pamoja na kuandaa mpango wa kuwahamisha wananchi watakaopisha mradi huo.

Hatua mbalimbali zimefanyika hadi hivi sasa ili kuhakikisha mradi huo  wenye manufaa makubwa hapa nchini kwa upande wa Wananchi, Wilaya ya Ulanga na Mkoa wa Morogoro kwa ujumla unakamilika na kuanza uchimbaji.

Kikosi kazi kilichoundwa kusimamia masuala kadhaa ikiwemo suala la uhamishaji wa wananchi kimekuwa kikiendelea kukamilisha kazi zake kwa awamu na awamu ya sasa kimekamilisha awamu ya kwanza ya mpango wa kuhamisha wananchi  watakaopisha mradi huo.

“Awali tulianza na zoezi la utambuzi wa kaya,  ikafuata hatua ya uthaminishaji  ambayo ilifanywa vyema na serikali chini ya Mthamini Mkuu hatua hii ilikuwa muhimu sana kwani ndiyo ambayo itawezesha zoezi la ulipaji wa fidia, kujenga makazi mapya na ya huduma za kijamii na kisha zoezi la kuandaa mpango wa kuwahamisha watu kupisha uchimbaji wa mgodi,” anasema Nasor Said Msemaji wa Kampuni ya TanzGraphite .

Amesema mambo yote kuhusiana na mradi huo yanakwenda vizuri sana, na hadi sasa mpango wa kuwahamisha wananchi umewasilishwa serikalini na kwa wadau wakiwemo wananchi ambapo sasa zoezi shirikishi linaendelea kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi wote  watakaopisha mradi huo  katika kijiji cha Epanko.

Meneja maendeleo ya Jamii wa TanzGraphite, Benard Mihayo,  amesema pamoja na kwamba mpango wa kuwahamisha wananchi umekamilika lakini bado kampuni hiyo kwa kushirikiana na serikali ya kijiji na vitongoji inaendelea kutoa elimu juu ya masuala muhimu kuhusu mradi huo.

“Tunafahamu mradi huu ulivyo mkubwa na tunafahamu juu ya sintofahamu nyingi zinazojitokeza, lakini niseme tu kwamba kampuni imejipanga kuwafanyia wananchi mambo makubwa na  ya kiutu.

Mbali na kulipwa fidia za kupisha mradi, kampuni itawajengea nyumba wananchi katika eneo la Kitonga ambalo limeshafanyiwa tathimini, itawapa maeneo ya kulima lakini kwa kuwa tunafahamu kwamba maeneo ya kulima yatakuwa mapya basi kampuni itawahudumia wananchi kwa kuwapa chakula kwa kipindi cha miaka miwili,” anasema.

Amesema pamoja na hivyo Kampuni ya TanzGraphite itajenga miundombinu  ya huduma muhimu kwa ajili ya kijiji kipya ikiwemo Shule, Zahanati pamoja na uchimbaji wa visima vya maji salama yenye uhakika kwa maeneo yote muhimu yaliyoainishwa kwa ajili ya huduma ya maji salama kwa wananchi.

“Hii haijawahi kutokea katika suala zima la ulipaji wa fidia kwa wananchi hapa nchini, tunafanya haya kwa kuamini kwamba ni stahiki kwa wananchi, lakini pamoja na hayo mradi wenyewe wa madini utakuwa na manufaa makubwa sana kwa wananchi, asilimia kubwa ya vijana wa hapa kijijini watapata ajira kwenye maeneo mbalimbali ya mradi wa madini,” anasema Mihayo.

Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Jacob Kasema, ameipongeza TanzGraphite na kikosi kazi kwa kukamilisha awamu ya kwanza ya mpango wa kuhamisha wananchi, na kukitaka kikosi kazi kuendelea na zoezi linalofuata huku wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi.

“Mradi umefika pazuri, kwa upande wa Serikali tunaona hakuna shida, ninawapongeza Kampuni na kikosi kazi kwa hapa walipofikia ambapo sasa matumaini yanaonekana. Tuna tatizo la wananchi wachache ambao wamekuwa na shida katika suala la uthaminishaji, hawa tuliwapa siku 60 ili wajitokeze na kisha tukawaongeza siku 30 sasa kama bado hawatajitokeza kufanyiwa uthamini maana yake Serikali itachukua hatua zinazostahili,” anasema Mkuu huyo wa Wilaya.

Mpango huo wa uhamishaji makazi umechukua miezi 12 ukihusisha masuala mbalimbali muhimu ikiwamo kuainisha na kubaini watu watakaoathiriwa na mradi, kukagua ardhi, mali zilizopo kwenye ardhi, kuandaa tathimini ya awali, kutathimini eneo watakalohamishiwa wananchi kwa kuangalia miundombinu ikiwamo barabara, viwanja vya michezo na mambo mengine muhimu kwa maisha  endelevu.

Baada ya kukamilika kwa kazi hizo, Kikosi kazi kiliandaa taarifa ambayo imewasilishwa Serikalini, na katika ngazi zote na Wizara zote zinazohusika ikiwamo Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga kwa ajili ya utekelezaji.

Mradi wa madini ya Graphite wa Epanko ni moja ya miradi mikubwa ya uchimbaji wa madini hayo duniani, na unatarajia kuwa na manufaa makubwa kuanzia kwa wananchi wa Epanko na Tanzania kwa ujumla hasa kwa kuwa kutaifanya Tanzania kuwa mzalishaji namba mbili wa madini hayo duniani  baada ya China akifuatiwa  na India na baada ya miaka mitano itakuwa nchi pekee katika Afrika kwani Zimbabwe na Madagascar zitakuwa zimemaliza hazina zake.

Madini ya Graphite (Kinywe) ndiyo yanayotumika katika kutengeneza vitu mbalimbali ikiwamo betri za simu, kompyuta mpakato  ‘laptop’ na penseli, na vitu vingine vyenye asili ya ukaa. Umuhimu  wa madini hayo umeongezeka  maradufu baada ya uamuzi kufanywa na nchi za dunia ya kwanza  kuwa karibuni wataachana na matumizi ya magari yanayotumia petroli ambayo huchafua hewa kwa ukaa na hivyo kutumia magari ya umeme badala yake ambapo betri zitatengenezwa kutoka katika madini hayo ambayo Tanzania inayo kwa wingi kutoka sehemu zinazofahamika tano ikiwamo mikoa ya Morogoro , Lindi , Mtwara, Manyara na Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles