TRIPOLI, LIBYA
MAKUNDI yanayopingana nchini hapa yamekutana kwa mara ya kwanza kwa muda wa zaidi ya miezi mitano mjini Sicily hapo jana huku Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte akiwasilisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika uchaguzi mwaka 2019.
Hata hivyo haijawa wazi iwapo kukutana kwao kutaleta mabadiliko ya kweli katika mgogoro wa kisiasa unaoikumba Libya.
Kulingana na mjumbe ambaye hakutaka jina lake litajwe, mazungumzo hayo yalisababisha Jenerali Khalifa Hiftar ambaye ni kamanda wa jeshi aliloliunda mwenyewe la LNA linalolidhibiti eneo la Mashariki mwa Libya, kukubali Fayez Siraj anayeongoza Serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliyoko Mjini Tripoli, anaweza kuendelea kushikilia nafasi yake hadi pale uchaguzi utakapofanyika.
Waziri Mkuu wa Italia, Conte alisema bado ni muhimu uchaguzi ufanyike kwa kuweka mbele usalama na kuheshimu mahakama na katiba.
Kwa upande wake, Ghassan Salame mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya, ameonya ama mchakato wa kisiasa usonge mbele au mapigano mapya huenda yakatokea wakati wowote.
Taarifa ya pamoja ilitaja umuhimu wa kufanyika uchaguzi kati ya mwezi Machi na Juni mwakani na kuzihimiza pande zote zinazohasimiana zisitishe vurugu.
Mazungumzo ya pande hizo mbili zinazohasimiana nchini Libya yalihudhuriwa pia na Rais wa Tunisia, Bejd Caid Essebsi, Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev, Waziri Mkuu wa Algeria, Ahmed Ouyahia, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya, Salame na Rais wa Misri, Abdel-Fattah al-Sissi pia walihudhuria.
Claudia Gazzini, mchambuzi wa masuala ya Libya katika shirika la kimataifa la kushughulikia migogoro, alisema iwapo kutakuwa na makubaliano ya kweli kati ya Haftar na Siraj basi hatua kubwa itakuwa imepigwa katika juhudi za kuleta amani nchini Libya