NA ASHA BANI-DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Kangi Lugola, jana aligeuka mbogo na kuwakemea hadharani watendaji wa Manispaa ya Kinondoni kwa kushindwa kusimamia usafi katika manispaa hiyo.
Alionyesha hali hiyo Dar es Salaam jana alipokuwa akikagua usafi katika eneo la Tandale kwa Mtogole.
Waziri aliwataka viongozi wa halmashauri zote nchini wakiwamo wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia usafi vinginevyo watachukuliwa hatua.
Akiwa katika eneo hilo, Lugola, alianza kwa kusikiliza kero za wananchi kuhusu usafi wa mazingira.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mhalitani, Sudi Makamba, alisema wanakabiliwa na changamoto ya uzoaji taka, licha ya wananchi kuchangia huduma hiyo lakini manispaa haipeki magari ya kuzoa taka.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli alisema si jukumu lao ila utaratibu wao ni kuzoa taka za umma hasa katika maeneo ya sokoni na siyo katika nyumba za watu.
“Tatizo lipo kwa viongozi wa serikali za mitaa wakiwamo watendaji na wenyeviti kwa kushindwa kusimamia wakandarasi,” alisema Kagurumjuli
Baada ya utetezi huo mkurugenzi, Lugola alisema ameamua kufanya operesheni hiyo kutokana na nchi kukumbwa na athari ya mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hali ya hewa.
Alisema kwa sasa katika Bahari ya Hindi, hasa katika mikoa ya Tanga, Pwani Lindi na Mtwara, maji yameongezeka na kuathiri kingo za bahari hali inayosababishwa na mmomonyoko wa udongo.
Alisema hali hiyo inachangiwa na shughuli za binadamu ikiwamo uchafuzi wa mazingira na uzalishaji wa taka ngumu kama vile mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.