NA TENGO KILUMANGA,
MABADILIKO ya kimaisha ni kitu cha kawaida. Mabadiliko hayo yakiwa ni yale ambayo yanaleta maendelo kwa bindamu na jamii basi ni mabadiliko chanya.
Kama haya mabadiliko ni yale ambayo yanairudisha nyuma jamii ya dunia basi hayo si maendeleo ni kurudi nyuma na kuandaa misingI ya ghasia na vurugu. Si lazima iwe ghasia na machafuko ambapo yanaleta maasi ya kijamii lakini fikra hasi na urasimu mbaya ndio mwanzo wa kukwamisha maendeleo na kutekeleza umoja.
Ukitaka kufanikiwa ni lazima jamii yote ipate elimu ya kile unachotaka kukifanya. Mkiwa wote kwenye ukurasa mmoja na wanajamii wengi, kama si wote, wanaelewa na kukubaliana na fikra na mawazo ambayo yanapendekezwa basi hata kama mawazo yanakwenda na kinyume na tamaduni za kawaida basi mtasonga mbele. Njia ni moja, malengo ni wote wanaelewa basi kutekeleza ni rahisi. Kama ni kichwa tu kinataka kubadilika bila ya kuwasilisha kwa mwili na mwili ukakubali basi itabaki kuwa ni ndoto miaka nenda miaka rudi.
Marekani ni nchi ya kibepari na fikra na falsafa ya kibepari ni kwamba soko ndio linatawala. Ukitaja ujamaa, hata kama ni ule usiokuwa na nguvu yoyote na uliokuwa umechanganyika na ubepari na mdogo vipi, Wamarekani wanaweza kupata kwikwi.
Ujamaa na utaasishaji kwa kulipa asilimia kidogo kama kodi ambayo inakwenda kwenye kutengeneza mazingira na maendeleo ya jamii, kutoka kwenye faida yoyote ambayo mtu, kampuni au shirika ambayo imepatikana umebeba ujumbe ulio kinyume na mtazamo wao.
Mafanikio hapa ni ya kibinafsi jamii haipati kitu ila kwa huruma za matajiri na watoa huduma za kusaidia jamii kama makanisa. Na kama wewe upo chini na bahati yako imekwisha kabisa kwa muda huo, na wapita njia wanakukanyaga kama njia ya kijijini na kuacha makovu kwenye nafsi yako, wewe hivyo basi unajikuta kwenye huruma na furaha ya wakubwa na wale wanaotoa misaada. Mfumo huu haujali jamii.
Wanadiaspora hawataki kuona kwamba nchi na jamii zao zinakutwa na hali hiyo na ndio maana nguvu nyingi sana wanaweka kwenye kuwasaidia ndugu na jamaa. Nguvu hiyo haitoshi, kwa mtu mmoja kuchukua jukumu la kutaka kusaidia jamii yake utakuta analazimika achague nani amsaidie na nani amuache. Jamii kwa ujumla haifaidiki. Utawezaje kula na kushiba wakati pembeni yako watu wengine wanakufa na njaa? Nafsi yako itakusuta. Kuepukana na hilo basi ni bora nguvu iwekwe kwenye kunyanyua jamii yote, uwepo mfumo ambao unasaidia kuweka misingi ya ya maendeleo kwa wote. Ukiwapo msingi mzuri basi wengi watafaidika.
Katika jumuiya yetu ya Watanzania Sweden tuna timu yetu ya mpira ambayo inafanya maajabu huku ulaya kaskazini. Ni timu ambayo imeweza kupambana na mazingira magumu sana na kuweza kufika hapo walipo. Timu isingeweza kufika hapo walipo bila ya msaada na jitihada za kijamii. Hasa watu kama Jacob Pius Msekwa ambaye ni mnazi mkubwa wa hiyo timu ya Watanzania, na pia Balozi Dorah Msechu.
Bila ya watu kama hawa ambao wanaona umuhimu wa kusaidia kimawazo, kiuongozi na hata kutoa fedha zao mfukoni jumuiya hii isingekuwa na cha kujivunia na kiunganishi kikubwa katika jamii yetu. Hii pia inatufundisha umoja ni kitu gani. Bila ya kushikana na kunyanyuana tutaua ule utu tuliotoka nao kutoka nyumbani.
Huu si mwenendo wa Watanzania ambao wapo Ulaya Kaskazini, ni jumuia nyingi sana za Watanzania dunia nzima. Kila jumiya inaleta kitu fulani kwenye familia za Watanzania nje, hata kama ni kidogo. Sasa nguvu zote hizi zikiwekwa pamoja bila ya ubinafsi na kwa kushirikiana na Serikali na jamii mbali mbali Tanzania, nchi itasonga mbele kimaendeleo. Mshikamano wa manufaa kwa wote ni muhimu sana hasa muda huu wakati nchi njingi Ulaya na Marekani zinapeleka mbele siasa za kibaguzi.
Ubinadamu si tu mali au hali ya maisha ulipo kijamii, ubinadamu ni jinsi tunavyowaona wenzetu na jinsi tunayopokeana. Jinsi tunavyolea watoto wetu na jinsi tunavyowaelimisha na kuhifadhi historia zetu binafsi na historia ya jamii yetu. Mali, utajiri na nafasi fulani katika jamii ni fikra za kisasa lakini huruma, au tabia ukarimu au mwelekeo wa kutaka kuangaliana na kusaidiana ni sehemu ya ubinadamu wetu.
Tukisema mtu si binadamu tunamaanisha hana utu na anafanya mambo kinyume cha ubinadamu au utu wetu ambao tunajali viumbe vingine na hata kuheshimu mazingira yetu. Ni ubinadamu kumsikiliza au kuwasikiliza hoja za wenzako, Je wanasemaje na kwanini watu hawa wanalilia haki zao kama binadamu? Hawaji tu na madai lakini wanakuja na suluhisho ya hayo madai na kuonyesha jinsi wataweza kushirikiana na binadamu wenzao kuleta maendeleo.
Mwamko huu wa kutaka tutengeneze chombo hicho ni baada ya kuona kwamba fikra zetu na mategemeo yetu ni tofauti kuliko tulivyokuwa tukiambiwa na kuamini. Masikitiko ni kwamba hisia tunazopata ni kwamba mamlaka hayakuwa wazi, ingawa makosa yapo pande zote. Si kwa sababu hatuangalii na kufuatilia sheria inasemaje na mamlaka ya kutokuwa na busara ya kutufafanulia sheria inasemaje. Sidhani kama yote haya yalikuwa kwa ubaya sidhani kama kuna mtu alihisi kwamba tunaweza kupata hali ya namna hii.
Katika ubinadamu wetu na jinsi tunavyokuwa na hisia zinatufanya tuanzishe imani na njia za kuwaleta wanajamii pamoja katika fikra moja na pia kuwa na kila sura ambayo wengi wataweza kuingia na kuwasiliana na wengine kwenye mawazo ya pamoja. Katika hali hiyo kutafuta ukweli wa hali ya mazingira na haja ya kuboresha hali yetu. Diaspora si tofauti na wengine katika kuunda umoja wetu ambao unaleta Watanzania wengi wanaoishi nje na wenye fikra na matakwa yanayofanana na hamu, nia ya kutaka kuchangia kwenye maendeleo ya nchi yetu.
Kama mzalendo mwingine yeyote yule Diaspora ni wale ambao wanapenda sana nchi yao. Wasingeipenda wasingejiita Diaspora na wala kujitambulisha kwamba ni watu wanaotoka eneo hilo. Na hii ni moja ya mapenzi ya nchi yetu ambayo tunjaribu sana kuwapa watoto wetu.
Katika kila makala nitaandika jinsi Watanzania wanavyopandisha bendera yetu huko tulipo. Hapa ni baadhi ya mambo ambayo Watanzania wanafanya nje ya Tanzania na kushirikiana na balozi zetu:
Jumuiya ya Watanzania Dallas walianzisha majadiliano kwa ndege ya moja kwa moja kutoka DFW (Dallas) mpakaTanzania. Watendaji Jumuiya ulioitishwa kutoka uwanja wa ndege DFW na American Airlines na Balozi wa Tanzania kujadili mpango huu. Matokeo yakiwa mazuri yatapunguza gharama ya kusafiri kwa Tanzania na hivyo kuongeza biashara, biashara na utalii
Jumuiya pia iliwezesha mkutano wa ngazi kati ya Southern Methodist University (SMU) na H. E Balozi Masilingi. Lengo la msingi ni kutafuta ufadhili wa masomo kwa Watanzania na pia kuruhusu kwa kushirikiana baina ya taasisi na vyuo vikuu Tanzania
ukisha fahamu haya yote basi ,iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga.