29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

TUSISUBIRI FURSA ZITUFUATE TUNAPASWA KUZITAFUTA

ZIARA ya hivi karibuni ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki hapa nchini aliyetumia saa 48 katika ardhi yetu imetufungua macho katika nyanja nyingi zikiwamo za kisiasa na kiuchumi kupitia uwekezaji, kutokana na kubainisha dhamira ya taifa lake kuwekeza katika sekta muhimu zinazohitaji ukuaji hususani katika kilimo cha kibiashara na miundombinu, ikiwemo reli itakayotuunganisha na nchi jirani zinazotuzunguka hivyo kuboresha zaidi uwezo wetu kiuchumi kupitia biashara na kuimarisha kiwango cha ukuaji wa kujimudu kimaisha kwa Watanzania wengi kutokana na fursa zitakazopatikana.

Kuna mashiko mengi katika ziara ya Rais huyo ukiachilia mbali wito wake wa kusitisha ushirikiano na hasimu wake kisiasa Fethula Gullen kupita taasisi zake, lakini ziara yake yenye mrengo wa kiuchumi zaidi inabainisha jinsi tunavyosubiri fursa zitufuate badala ya kuzitafuta kwa juhudi kubwa ili kuboresha mustakabali wa maisha yetu. Kisiasa, umbali baina ya nchi mbili husika hauzuii ushirikiano wa kimataifa katika nyanja mbalimbali mtambuka kwani ni mojawapo ya umuhimu wa kuwa na uwakilishi wa nje kupitia balozi zetu katika nchi mbalimbali duniani.

Ili kuhakikisha tunaboresha uhusiano wa kidiplomasia lakini pia kutangaza fursa tulizonazo na kuvutia wageni kwenye sekta ya utalii na ukuaji wa kiuchumi, ambao hujiakisi katika mipango na mikakati ya sera zinazoongoza taifa kwa mujibu wa ilani ya chama kinachotawala, kwa kuwa ujirani mwema ni moja ya njia za kufanikisha maisha bora ya watawaliwa si tu kwa yanayotokea ndani ya nchi lakini pia kupata mhimili wa nje kwa ushirikiano na mataifa yanayotuzidi hatua za maendeleo katika wigo wa sekta mbalimbali.

Ukitazama kwa jicho hilo ni sawa na umelenga kiuchumi zaidi lakini kwa mtazamo mwafaka zaidi katika historia ya ushirikiano baina ya mataifa kwa ustawi wetu, si kwa uchumi pekee lakini kisiasa pia ndipo umuhimu wa kujikita katika kutafuta badala ya kutafutwa unapojisadifu kwani kulenga inakopatikana tija ni mojawapo ya majukumu ya Serikali inayoongoza. Mathalani, Rais Erdogan aliyeambatana na msafara mkubwa unaojumuisha wajumbe wa baraza la ushirikiano wa uwekezaji wa kimataifa kutoka nchini mwake anaitazama kwa hamu fursa ya kujenga reli yenye thamani kubwa ya dola za Marekani bilioni 7.6 muda mfupi baada ya tenda hiyo iliyozawadiwa kampuni za China kusimamishwa kutokana na utata wa kimchakato, baada ya Rais JPM kuingia madarakani na kuiachia Uturuki nafasi kubwa zaidi ya kunyakua tenda hiyo.

Lakini pia eneo lingine ambalo Uturuki imelenga ni katika kutusapoti kwenye Bajeti yetu kutokana na mataifa mengi wafadhili kusitisha baadhi ya misaada ama kutokana na ufisadi ambao Serikali ya Rais Magufuli inahangaika kuudhibiti, lakini pia bila shaka ni mwenendo wetu kwenye baadhi ya maeneo kutokana na demokrasia yetu isiyoeleweka kwa baadhi ya matukio yetu ya uchaguzi. Kwa hiyo Serikali inaigeukia Uturuki lakini pia ilishapanga kujielekeza kwenye mataifa ya China na India ili kupata mikopo nafuu ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 939.

Kwa mtazamo wa haraka ni sawa na ‘mgeni njoo mwenyeji apone’ lakini kwa mtazamo wa kina ni sawa na mataifa makubwa na ya kati duniani yanachungulia usingizi wetu kuhusiana na fursa tulizonazo, ambazo kwa uyakinifu hatuzishughulikii ipasavyo katika sekta nyingi tukitibu makovu ya makosa ya kila awamu ya utawala na kurudi kuchota tena kwenye makosa hayo na kujinufaisha licha ya uwekezaji kutunufaisha sisi kwa fursa za ajira.

Ni katika zama za sasa ambazo hatuna fungamano kubwa za kisiasa duniani zilizodhoofika kutokana na mabadiliko ya upepo wa kisiasa, ukiwamo Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande wowote (Non Alligned Movement) huku kukiwa na jumuiya za kimaeneo hususan barani Afrika (SADC, IGAD, COMESA, ECOWAS), ikiakisi hulka ya kila kundi na mashiko yake kisiasa kwa njia ya kidiplomasia ili kuimarisha nguvu zake na kuneemesha maisha ya watu wake.

Si kweli kuwa tunapendwa kupita kiasi ndiyo maana mataifa mengine yanakimbilia kwetu katika kuwekeza na kubadilishana fursa, lakini pia inawezekana kuwa tunabadili mwelekeo na kuwa na rekodi nzuri zinazovutia ingawa pia inawezekana kuwa hatujagundua kwamba tuna almasi mkononi tukidhani ni jiwe hivyo kuwa tayari kubadilishana na wanayoitaka.

Kwa undani zaidi ni kwamba katika muundo wetu wa mfumo wa utawala tuna sekta zenye jukumu hilo la kimsingi, kuhakikisha tunapiga debe kuvuta waje kwetu lakini kwa manufaa yetu si yao ili tuepuke kurudia makosa kama tuliyofanya kwenye sekta ya madini kutokana na mirabaha isiyokidhi kwa tunachowapatia.

Unaweza kutaja wizara mbili tu za Utalii na Mambo ya nje lakini pia majukumu wanayokasimiwa mabalozi wetu tunaowatuma nchi za nje, kama ambavyo siku zote Rais Magufuli anapowaapisha akiwasisitiza kutuwakilisha vyema lakini pia kutunadi na kutimiza wajibu wa kuhakikisha tunaneemeka kupitia nafasi alizowateua. Lakini kuna la kimsingi zaidi la kutekelezwa katika nafasi ya juu ya uongozi hata kwa Rais mwenyewe kwa kuwa baba mwenye nyumba akiinuka kumfuata baba mwenye nyumba mwenzake, kunakuwa na uzito zaidi kuliko akimtuma mtoto kumwakilisha kwenye suala muhimu kwa kuzingatia baadhi ya maeneo muhimu ili kupunguza utegemezi wa asilimia ya Bajeti yetu kufikia asilimia 3 kutoka 6.4 iliyokwishapunguzwa kutoka asilimia 10,ingawa kitakwimu ndivyo inavyosema lakini huenda ikatofautiana na kiuhalisia.

Kwa kutumia sera ya ushirikiano wa kimataifa kuimarisha uwiano wa kimataifa kujikita katika uhusiano baina yetu na nchi moja moja na jumuiya za kimataifa, tutapata fursa za makubaliano ya uwekezaji utakaotukwamua kwa kulenga uchumi wa kisasa wa viwanda vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini.

Lakini pia jinsi tunavyotumia fursa za kutanua wigo wetu mdogo katika nyanja ya kimataifa ili kujiweka katika mzania sawia, si tu kwa fursa zitakazotuongezea pato la kigeni litakalotuwezesha kufukia shimo la utegemezi mkubwa wa Bajeti kwa mujibu wa sera yetu ya uwekezaji wa ndani na nje, kwa kukuza kiwango cha tunachouza nje kwa uwiano wa tunachovuna ili kukuza uwezo. Lakini mwisho kabisa ingawa si kwa umuhimu ni tunavyojiweka katika nyanja za ushirikiano wa kisiasa kimataifa bila kusiganisha pande zinazohasimiana kwa kuwa tumerejesha uhusiano na Israel lakini bado tunaunga mkono uhuru wa Wapalestina.

Tukiwakirimu viongozi wakubwa kimataifa wanaofuatana kuja kutengeneza fursa hapa kwetu akiwamo Erdogan, Rais Truong Tan Sang wa Vietnam na bila kusahau ingawa muda umepita Rais Xi Jinping wa China. Tuna nafasi ya kutumia kukubalika kwa namna yoyote ile kuzitafuta fursa badala ya kubweteka kuzisubiri zitufuate kwani hakuna shaka kuwa, tunakubalika tangu awamu ya kwanza hadi ya tano tulichozubaa ni kutotumia vyema kukubalika kwetu kwa manufaa yetu kwa mujibu wa sera zetu tulizojiwekea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles