Na MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM
MATUKIO ya watoto kubakwa na kulawitiwa yamezidi kuongezeka kwa kasi hadi kufikia watoto 2,571 mwaka huu kutoka 1,585 mwaka jana.
Takwimu zilizotolewa juzi katika maadhimisho ya miaka 21 ya Kituo cha -Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zinaonyesha kuwa kuanzia Januari ilikuwa watoto 180 hadi kufikia Machi mwaka huu watoto 1,765 walifanyiwa vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Helen Kijo Bisimba alisema idadi ya watoto wa kiume kulawitiwa inaongezeka kwa kasi ya ajabu.
“Matukio ya watoto wa kiume kulawitiwa yameendelea kuonezeka kwa kasi ya ajabu huku wahusika na ukatili huo wakirandaranda bila kuchukuliwa hatua za msingi kwa hoja ya uhusiano wa karibu kati ya mtoto na aliyemlawiti,”alisema Bisimba.
“Ripoti inaonyesha kuwa asilimia 49 ya vitendo hivyo hufanyika nyumbani,asilimia 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda au kurudi shuleni na asilimia 15 hufanyika shuleni,”alisema
Katika maadhimisho hayo LHRC walitoa msaada wa mahitaji ya watoto wanaoishi katika kituo hicho.
Akishukuru msaada huo, Ofisa Mfawidhi wa watoto katika kituo hicho, Betres Laurence alisema kuwa serikali, jamii ma wadau kwa pamoja wanawajibu wa kushirikiana ili kutatua changamoto za watoto.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Afisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Tabu Shaibu alisema kati ya hao, watoto wa kike sawa na asilimia 43 walikuwa wamebakwa na 24 wa kiume sawa na asilimia 7.9 walikuwa wamelawitiwa.
“Kwa sasa Mazingira mengi yanayowazunguka watoto hayapo salama kutokana na watoto kushindwa kuhimili changamoto hiyo wazi wachukue tahadhari dhidi ya Mazingira wanayokuwepo watoto baada ya muda wa masomo..
“Vitendo hivyo huanzia majumbani na ndiko kunakoongoza kwasababu kwa wakati huo walimu hawapo katika nafasi ya kujua nini wafanyacho watoto nje ya shule,’’alisema Tabu.
Aidha aliwataka wazazi na walezi kuchukua tahadhari dhidi ya mazingira yanayowazunguka watoto hususan kuchangamana na watu walio wazidi umri.
“Wazazi na walezi mjenge mazingira ya ukaribu,upendo huduma ya msaada wa kisaikolojia unaogusa na kujenga mawazo yao katika mihemko na tabia za watoto ikiwa ni pamoja na masuala ya kijamii yanayogusa elimu, mazingira, mila,desturi pamoja na mahusiano yao na wenzao”alisema.
Kulingana na sheria ya mwaka 2009 ni jukumu la kila mmoja kutoa taarifa za ukiukwaji wa haki za mtoto, ukatili na udhalilishaji ili hatua za kisheria ili ziweze kuchukuliwa dhidi yao.