VERONICA ROMWALD Na CECILIA NGONYANI (Tudarco)
–DAR ES SALAAM
WAKATI Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ukiendelea kubomoa nyumba za wakazi wa Kibamba waishio kandokando mwa barabara, wakazi hao wamedai ubabe umetumika na sheria kupindishwa.
Walieleza hayo jana walipozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti katika eneo la Kimara-Stop over, ambako bomoa bomoa ilikuwa ikiendelea.
Mmoja wa wakazi hao, Suleiman Kivatwa (70), alisema amesikitishwa na hatua hiyo wakati kesi ya msingi bado ipo mahakamani na Jaji anayeisimamia hajatoa uamuzi.
“Ninavyofahamu, kulikuwa na kesi tatu ya maeneo haya, kulikuwa na kesi ya wenzetu wa Kibamba, Mbezi na sisi wa Stop Over, nakumbuka wenzetu wa Kibamba walipata ‘stop order’.
“Sisi wa Stop over wakili wetu alifungua kesi Mei 3, mwaka huu tayari imetajwa mara sita tangu wakati huo hadi sasa, ilipotajwa mara ya kwanza hadi ya tatu wakili wa Serikali aliweka pingamizi,” alisema.
Alisema baada ya wakili huyo kuwasilisha pingamizi lake, mahakama ilipanga tarehe ambayo mwanasheria wa Serikali naye angewasilisha hoja zake.
“Baada ya Mwanasheria wa Serikali kuwasilisha hoja zake, Agosti 16, mwaka huu Mwanasheria wetu naye aliwasilisha hoja zake ambapo alipinga zile za Mwanasheria wa Serikali na jaji anayesikiliza kesi hiyo alipanga kuitolea maamuzi Agosti 30, mwaka huu,” alisema.
Aliongeza: “Lakini jambo la kushangaza, kabla ya maamuzi kutolewa, Agosti 17, mwaka huu Tanroads wamekuja na kuanza kubomoa nyumba zetu, tuliomba angalau watupatie wiki moja tusubiri uamuzi wa mahakama lakini wamegoma, huu ni ubabe.
Kivatwa alisema wamekusudia kwenda mahakamani kudai haki yao hapo baadaye.
“Binafsi nimepata hasara ya zaidi ya milioni mbili tangu Julai 28, mwaka huu, leo (jana) nahangaika kuhamisha mali zangu ili kuziokoa, tutakwenda mahakamani kudai haki yetu.
“Kwenye eneo hili nimejenga nyumba yangu tangu mwaka 1981 na hakukuwa na alama yoyote ya ‘road reserve. Mwaka 1997 kulikuwa na ukarabati wa barabara kuu, waliokuwa mbele yangu walibomolewa na walipewa viwanja huko Mbweni, sisi hatukuguswa kwa sababu hatupo ndani ya hifadhi ya barabara,” alisema.
Alisema pamoja na hayo wanaiomba Serikali kuingilia kati suala hilo na kwamba iwafikirie na kuwalipa fidia wanayostahili.
“Tunaiomba Serikali iwe na moyo wa huruma kwa raia wake, heri mimi nina eneo ambalo nitaenda kuanza maisha mapya, lakini ni gharama kubwa kuanza upya, tunaamini katika utawala wa sheria na tunaipenda Serikali yetu katika hili tunaomba watufikirie,” alisema.
Naye Mariam John alisema hadi sasa hajui wapi atakapokwenda kuishi, kwani yeye ni mjane na kwamba alikuwa akiendesha maisha yake kwa kodi alizokuwa akipokea.
“Mimi ni mjane ninalea watoto wanne, tulibahatika kujenga nyumba yetu hii ambayo leo nashuhudia ikibomolewa, inaniuma lakini sina jinsi, sijui hata naenda kuishi wapi hivi sasa,” alisema.
Wakati ubomoaji huo ukiendelea, MTANZANIA lilishuhudia wakazi wa eneo hilo wakihangaika kutoa mali zao zilizokuwa ndani ya nyumba ili kuziokoa.
Vijana waliokuwa na vibanda vya biashara nao kila mmoja alikuwa akihangaika kuokoa bidhaa zake zilizokuwa ndani ya vibanda hivyo.