28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

KITUO CHA NYUKLIA KUGHARIMU SH BILIONI 11

Na ELIYA MBONEA

-ARUSHA

KUKAMILIKA kwa ujenzi wa mradi wa  maabara ya Teknolojia ya Nyuklia ya Tume ya Nguvu za Atomiki  (TAEC), kutaifanya Tanzania kuwa kituo mahiri cha kanda katika masuala ya uhamasishaji na udhibiti wa matumizi salama ya nguvu za atomiki.

Majengo ya maabara hiyo ya kisasa yatarajiwa kukamilika Februari  mwaka 2018, huku ujenzi huo ukigharimu Sh bilioni 2.3, kisha kufungwa vifaa vya  Sh bilioni 11 ambapo tayari vifaa vya Sh bilioni 2.6 vimewasili.

Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi uliofanywa jana mjini hapa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki (TAEC), Brigedia Jenerali Fulgence Msafiri, alisema mradi huo unaihusisha Serikali na Umoja wa Ulaya (EU).

Brigedia Jenerali Msafiri, alisema maabara hiyo itaiwezesha Tanzania kujenga uwezo katika kusimamia uchimbaji, uchakataji na usafirishaji wa madini ya Urani kwa kuzingatia usalama na viwango vya kimataifa, tija na faida, ikiwamo kujengea uwezo maabara za tume hiyo.

“Manufaa yatakayotokana na maabara ya teknolojia ya nyuklia, ni  kuongeza ufanisi wa tafiti mbalimbali katika fani ya Nyuklia hususani kutoa msaada wa utafiti kwa wanafunzi wa vyuo vikuu katika ngazi za Shahada ya Uzamili na Uzamivu,” alisema Brigedia Jenerali Msafiri.

Alizitaja taasisi zinazohusika na mradi huo, kuwa ni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ambayo itahusika kuimarisha uwezo wa kudhibiti mionzi kupitia TAEC, kwa upatikanaji wa vifaa na mafunzoili kuweza kudhibiti shughuli za matumizi vya vyanzo vya mionzi ikiwamo uchimbaji urani.

Alisema kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini, itakuwa ni kujenga uwezo wa matumizi ya nguvu za nyuklia, hususani uzalishaji wa umeme endapo Serikali itaweka na kusimamia utekelezaji wa sera ya matumizi ya nguvu hizo. Kwani kilogramu moja ya urani asili huzalisha joto sawa na linalopatikana kutokana na tani 20 za makaa ya m awe.

“Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, itakuwa na jukumu la usafirishaji wa urani na pia kubainisha uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo ya daraja la Saba ikiwamo madini ya urani ikiwamo Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kuhakikisha mradi husika unakuwa rafiki kwa watu na mazingira.

“Kwa upande wa EU, mradi unahusisha Kampuni ya LOKMIS kutoka Lithunia inayohusika na uboreshaji wa maabara  za tume kwa usafirishaji na usimikaji wa vifaa na kampuni ya ENCO: STK ya Finland na SCK.CEN kutoka Belgium inayohusika na mafunzo,” alisema Brigedia Jenerali Msafiri.

Kwa upande wake Profesa Ndalichako akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi, alisema ujenzi wa maabara hiyo unafanywa kwa fedha za serikali ambapo awamu ya kwanza tayari Sh bilioni moja zimetolewa, huku bilioni 1.3 zikitarajiwa kutolewa katika awamu ya pili.

Katika hafla hiyo, Profesa Ndalichako aliitaka TAEC kuhakikisha Maabara hiyo pindi itakapoanza utekelezaji wake ianze kuchangia Mfuko wa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi kutokana na kuanza kuingiza fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles