JOPO la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo watatoa uamuzi wa mvutano mkali kuhusu kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.
Mwenyekiti wa jopo hilo, Sekieti Kihiyo, alisema hayo jana akiwa pamoja na majaji wenzake, Aloycius Mujuluzi na Lugano Mwandambo.
“Jana (juzi) tuliwaambia leo tutatoa maelekezo muhimu, kesho(leo) saa nne tutatoa uamuzi,”alisema Jaji
Kihiyo.
Majaji hao walifikia hatua ya kutoa uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na pande mbili zinazovutana kuhusu kukaa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura.
Upande wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kuwasilisha utetezi, unawakilishwa na mawakili wanane
akiwamo Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Tulia Ackson.
Wengine ni Wakili wa Serikali Mkuu, Obadia Kimeya, Sarah Mwaipopo, Alesia Mbuya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Richard Kilaga, Aida Kisumo, Emmanuel Avishe kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Hamidu Mwanga kutoka Tume ya Uchaguzi.
Upande wa mleta maombi unawakilishwa na Wakili Peter Kibatala na Omary Msemo.
SERIKALI
Dk. Tulia anadai kwamba vifungu alivyotumia mleta maombi kuwasilisha maombi yake mahakamani hakuna mahali ambako vimevunjwa kwa mujibu wa sheria.
Alidai kwamba kifungu cha Sheria ya Uchaguzi namba 104(1) kinakataza mikutano ya aina zote bila kujali umbali.
Alidai kifungu namba 72 cha Sheria ya Uchaguzi kinaelekeza watu wanaotakiwa kuwapo mahali zinapohesabiwa kura kuwa ni mawakala, wagombea, waangalizi wa uchaguzi na wengine wanaoruhusiwa.
Ambao hakutajwa katika kifungu hicho hatakiwi kuwapo, alidai.
Alidai kilichozungumza na NEC kuhusu kukaa umbali wa mita 200 yalikuwa ni maelekezo, yaliyozungumzwa
na IGP ikiwa ni amri, na alichozungumza Rais Kikwete kilikuwa msisitizo.
Dk. Tulia alidai maelekezo yaliyotolewa na NEC yalifuata utaratibu na aliyosisitiza Rais Kikwete yalifuata maelekezo
yaliyotolewa na NEC ili kuwapo uchaguzi wa amani, huru na wa haki.
Alidai sheria inakataza kufanyika mikutano mahali popote siku ya uchaguzi na kwamba umbali wa mita 200 unahusiana na mtu kuonyesha alama, picha, bendera za chama zinazoshabikia chama au mgombea kutoka katika kituo cha kupigia kura.
MLETA MAOMBI
Wakili Peter Kibatala katika kuwasilisha hoja anaiomba mahakama itoe tamko kuhusu maana halisi na kusudio
la sheria la kifungu namba 104(1) cha Sheria ya Uchaguzi sura namba 343.
Pia anaomba mahakama iangalie maana ya kifungu hicho katika haki za wapiga kura au watu wengine wenye
shauku ya kukaa kwa utulivu umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura. Kibatala alidai msingi wa shauri hilo ni matamko yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kwamba mpiga kura au mtu mwingine mwenye shauku asikae mahali popote katika kituo cha kupigia mkura, hata kama utakuwa umbali wa mita 200 kutoka katika kituo ambacho upigaji kura unaendelea.
Maelekezo hayo yalitolewa tena na Rais Jakaya Kikwete katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Oktoba 14 ambako si tu alisisitiza katazo bali alikwenda mbali zaidi na kuonyesha kwamba asiyetii atachukuliwa hatua za sheria.