Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
HATIMAYE Rais Dk. John Magufuli amechukua uamuzi mgumu wa kununua korosho yote katika mikoa ya Lindi na Mtwara, huku akiliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuanza kazi ya kuisomba kupeleka kwenye maghala.
Rais Dk. Magufuli pia ameeleza sababu za kuwatumbua mawaziri, Dk. Charles Tizeba (Kilimo) na Charles Mwijage (Viwanda, Biashara na Uwekezaji).
Alitangaza uamuzi huo Ikulu, Dar es Salaam jana, wakati wa kuwaapisha mawaziri wapya.
Rais alisema Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ndiyo itanunua korosho hiyo kwa bei ya Sh 3,300 kwa kilo.
“Wanaoendelea kuja wala wasihangaike, sasa ni saa 5:15 (asubuhi) nimeshafunga… wasije korosho tunanunua wenyewe.
“Walijaribu kuleta mapendekezo kwako (kwa waziri mkuu) achana nao, watakuja kutuchezea baadaye.
“Walikuwa wapi siku zote kwani walikuwa hawajui tuna korosho na korosho yetu ni first class (daraja la kwanza),” alisema Rais Magufuli.
Awali, Rais alitoa muda wa hadi leo saa 10 jioni kwa makampuni yanayotaka kununua korosho, lakini baada ya kupewa taarifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana, alisema hakuna haja ya kusubiri muda huo.
Rais Magufuli alisema korosho hiyo inaweza kubanguliwa na kuuzwa nchini na kwamba Watanzania milioni 35 kila mmoja akinunua kilo mbili itaisha.
“Korosho iliyobanguliwa inauzwa kati ya Sh 15,000 na Sh 25,000 kwa soko la ndani. Tuna wastani wa tani 210,000 hadi 220,000 ukibangua kilo tatu unatoa kilo moja, tutapata wastani wa tani 70,000.
“Tuko milioni 55, Watanzania milioni 35, kila Mtanzania atakula kilo mbili zinaisha zote. Hata tukikosa masoko ya nje kwa bei ya ndani bado tutauza,” alisema.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hadi sasa korosho iliyoko kwenye maghala ya kuhifadhia korosho kutoka mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ni tani 90,232. Alisema uzalishaji mwaka huu hautazidi tani 220,000.
Pia alimuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo kujipanga tayari kwa kazi hiyo lakini akatahadharisha zisipelekwe korosho za wizi.
“CDF (mkuu wa majeshi) panga kikosi chako vizuri kila ghala lilindwe na jeshi na jeshi limeshawezeshwa hakuna korosho itakayopotea hata moja.
“Wakulima walipwe bila kuchelewa na wakilipwa asitokee mtu yeyote wa kumwambia huyu alikuwa na deni…atamfuata baadaye,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema korosho nyingine zitapelekwa katika Kiwanda cha Buko kilichopo mkoani Lindi ambacho awali kilibinafsishwa.
“Kuanzia leo kiwanda hiki ninawapa JKT hadi uamuzi mwingine utakapofanyika,” alisema.
Awali, kabla ya uamuzi huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alieleza kuwa hadi kufikia jana asubuhi kampuni 13 zilikuwa zimejitokeza kutaka kununua korosho kwa bei elekezi.
Alisema kati ya makampuni hayo, matano yalipeleka barua katika ofisi yake ya Dar es Salaam na manane yalipeleka barua Dodoma.
Alisema Kampuni ya Mega Movers ya India ilionyesha nia ya kutaka kununua tani 200,000, Mkemi Agri(tani 5,000), kampuni tatu (tani 1,500), kampuni nne (tani 1,000 kila moja), kampuni mbili (tani 500 kila moja) na kampuni nyingine mbili zilikuwa chini ye bei elekezi.
SPIKA NDUGAI
Naye Spika wa Bunge, Job Ndugai, alizitaka Wizara za Kilimo na Viwanda zijitathmini kumpungumzia mzigo rais.
“Moja ya kazi ngumu ni kuteua watu na wakati mwingine kuwatoa, si jambo rahisi na halifanywi ghafla.
“Wizara ya Kilimo imekuwa pasua kichwa kwa muda mrefu sasa sijui tatizo ni nini…wajitathmini, wajitazame tumpunguzie mzigo rais,” alisema Ndugai.
BODI ZA MAZAO
Rais Magufuli alisema alilazimika kuvamia kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu na kushirikisha wanunuzi wa korosho lakini alipoanza kusikiliza yaliyokuwamo yalimuumiza.
“Mwakilishi wa Bodi ya Korosho aliulizwa bei elekezi kwa mwaka huu, akasema ni Sh 1,500 niliumia sana. Yaani mkulima anahangaika na kulima, aweke mbolea, apalilie, apewe kilo moja Sh 1,500 na bodi ikawa imepitisha…ukishaona hilo unajua hii bodi si kwa ajili ya wakulima wa korosho.
“Niliwaambia bei elekezi ianzie Sh 3,000 lakini siku ya mnada wengine wakaongeza Sh 1, 2 na aliyeongeza zaidi ni Sh 16, wanafanya hivyo wakati tayari tumeshatoa baadhi ya kodi.
“Niliona huu ni mchezo ambao unaratibiwa, wamefanya makusudi ili mvua inyeshe korosho ianze kuharibika iuzwe kwa bei ya chini. Je, hii ndiyo sekta binafsi tunayotaka kuiendeleza?
“Bei ya korosho imeshuka hasa India na Vietnam, unapoangalia vyombo tulivyonavyo; Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara) jukumu lake ni kutafuta biashara nje na bodi nyingine mbalimbali kama za pamba, korosho, tumbaku lakini hakuna anayeshughulika.
“Tumebaki kusikiliza matapeli wanaotumiwa hawajali shida za wakulima. Na kilichotokea kwenye Bodi ya Korosho, Bodi ya Pamba ijiandae, tutapitia ‘performance’ ya kila bodi.
“Zao la pareto wakulima Kyela wanapata shida na bodi zipo. Ina maana Tantrade kazi yake ni Sabasaba au mkurugenzi wake anafikiria Julai 7 maonesho na kukusanya viingilio… kwa nini hashughuliki kutafuta bei ya mazao ya Watanzania?
“Mahindi wananchi wanauza kwa bei ya chini wakati Malawi wametenga Dola milioni 27.2 lakini wizara, makatibu wakuu na bodi zipo tu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliagiza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe katika ofisi ya waziri mkuu kwa kushindwa kufanya kazi vizuri.
“TIC hai – perform vizuri mahali iliko, inaingiliwa sana na wakurugenzi. Ihamishiwe ofisi ya waziri mkuu na mfanye mabadiliko.
“… na nitakuwa naangalia uwekezaji gani umekuja maana kuna wawekezaji wa ovyo sana wanakuja nchi hii,” alisema.
KILICHOWAPONZA MWIJAGE, DK. TIZEBA
Rais Magufuli alieleza hadharani sababu za kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri ambayo yaliwatupa nje, Dk. Tizeba na Mwijage.
Alisema sekta za kilimo na viwanda ni nyeti na muhimu kwa maendeleo ya Watanzania lakini zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania ambao ni wakulima muda mrefu wamekuwa vibarua wa watu wenye uwezo katika mazao yote.
Baadhi ya sababu hizo ni jinsi mawaziri hao walivyoshindwa kushughulikia suala la bei ya korosho, kahawa, pareto na ufufuaji wa Kiwanda cha Chai Mponde kilichopo Tanga na kile cha Buko mkoani Lindi.
Akizungumzia suala la korosho alisema: “Sikuona statement (taarifa) yoyote ya Waziri wa Viwanda au Kilimo hata kuwakemea sekta binafsi”.
Kuhusu suala la Kiwanda cha Chai Mponde alisema: “Kiwanda kimekaa idle (bila kufanya kazi) miaka minane.
“Nimemtuma Waziri Mkuu akaenda akatatua tatizo, mwishoni nikamwambia nitakufanya uwe Waziri wa Kilimo au Waziri wa Viwanda…unapoona mahali pengine lazima nimtume Waziri Mkuu ninajiuliza maswali mengi.
“Na kiwanda cha Mponde na kile cha Lindi havikurudishwa na Wizara ya Viwanda na hadi vinarudishwa hata mchakato wake hawakuujua,” alisema.
Aligusia pia suala la bei ya kahawa akisema: “Kama bei ya kahawa jirani kule mpaka wapigakura wa mheshimiwa Mwijage wanavuka mpaka kwenda kutafuta bei…ninajiuliza Waziri wa Kilimo hakujua kahawa ni kilimo pia…najaribu kutoa mifano michache”.
Hata hivyo Rais Magufuli aliwapongeza Dk. Tizeba na Mwijage kwa kuhudhuria hafla hiyo na kusema kuwa wameonyesha moyo wa uungwana kwa sababu kazi ni za kupita.
“Baada ya kutangaza tu Dk. Tizeba akanipigia simu, nikajiuliza nipokee…lakini alitaka kushukuru hajaishia gerezani amemaliza salama.
“Nampenda sana Mwijage na Dk. Tizeba lakini kwenye hili hapana, wengine wanasema nina ubaya na majina ya kina Charles…lakini sina nia mbaya nataka tufike mahali tusukume gurudumu la wakulima wetu.
“Niliyoyasema ndiyo sababu…wasitafute sababu nyingine, siyo kwamba siwapendi nawapenda tu sana,” alisema.
MAWAZIRI MIZIGO
Rais Magufuli pia alionyesha kukerwa na utendaji wa baadhi ya wizara na kusema wakati mwingine amekuwa akilazimika kumtuma Waziri Mkuu.
“Mara nyingi nimekuwa nikigombana na Waziri Mkuu na saa nyingine nampigia hata saa 8.00 usiku, namtuma huku na kule. Nilimwambia awakumbushe mawaziri wake kazi za uwaziri ni utumwa lazima tuwe watumwa wa watu maskini.
Hata hivyo alimpongeza Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo, kwa utendaji kazi akisema:
“Kuna wizara zinafanya kazi vizuri ingawaje si vizuri kuzitaja lakini Tamisemi kuna kijana huyu (anamtaja Jafo), kila mahali yupo amejenga vituo vya afya 300 na hospitali zaidi ya 67. Anashughulikia miradi ya barabara…natoa mifano tu si kwamba wengine hawafanyi kazi.
“Najiuliza ile miaka miwili iliyobaki wangapi watakuwa wamebaki, lakini ndiyo kaz,i si lazima wote mfike, hata wewe kiongozi unaweza bado usifike uliko tarajia lakini lengo lazima likamilike,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka mawaziri wapya kwenda kufanya kazi na kuhakikisha wanaendeleza ushirikiano huku akiwatahadharisha wakaridhike.
“Kazi hii ni ngumu na ni utumwa, mimi sitashangaa hata nikibaki na mmoja wala sitajali. Kubadilisha ni ‘very simple’, wabunge wako 300 nafanya ‘rotation’ tu ili kusudi nipate matokeo.
“Mimi si mkorofi ni mpole, lakini ninyi ndiyo wakorofi kwa sababu hamtekelezi wanayotaka wananchi…usipofanya nakutoa kwa ukorofi.
“Tunayoyasikia ni mengi lazima mkaridhike ndiyo kazi ya utumishi…zao la korosho limeingiliwa mno baadhi ya viongozi wa siasa walikuwa wanafanya biashara hiyo na baadaye wanasubiri kupigiwa kura,” alisema Rais Magufuli.
Aligusia pia wabunge wenye ndoto za uwaziri na kusema” “Msifikiri mtapendwa sana na baadhi ya wabunge kwa sababu wako wabunge watano kila siku wanawaza uwaziri, na mimi nimewasahau.
AIPA NENO BOT
Rais Magufuli aliitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iendelee kuzifuatilia benki mbalimbali nchini kutokana na kujihusisha na utakatishaji fedha.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hivi karibuni BoT iliwezaa kubaini kuwapo Sh bilioni 150 zilizoingizwa kwa ujanja ujanja kupitia benki moja.
“BoT fuatilieni kwa sababu kuna michezo inachezwa watu wanataka kuleta fedha za utakatishaji kupitia mabenki yetu, endeleeni kubana hivyo hivyo,” alisema.
Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mwijage alisema suala lililokuwa gumu akiwa waziri ni kuwajenga katika imani Watanzania katika uchumi wa viwanda.
“Nilipoteza muda wangu mwingi, si kazi rahisi na imenipa shida sana,” alisema Mwijage.
Hata hivyo, alisema yeye ni mjasiriamali hivyo ataendeleza shughuli zake hizo kwa sababu ana wateja katika sekta mbalimbali.
“Kwa wanaonijua ninapokuwa kwenye benchi ndipo nafanya kazi vizuri sana, nimetoka kina kirefu bado nipo maji mafupi,” alisema.
MAWAZIRI WAPYA
Akizungumzia uteuzi huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, alisema: “Viwanda vingi vilivyobinafsishwa uwekezaji wake hautufurahishi, hivyo tutachukua hatua na tutaisimaia TIC kuhakikisha wawekezaji wa ndani wanapata mazingira mazuri.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mary Mwanjelwa, alisema vipaumbele vyake ni kukuza ajira, upandishwaji wa madaraja kwa watumishi na kuongeza nidhamu ya utumishi.
“Tusifanye kazi kwa mazoea, kila mtu atapimwa kulingana na utendaji wake wa kazi na tutakuwa tunatoa mrejesho wa utendaji,” alisema Mwanjelwa.
Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa alisema vipaumbele vyake ni kuleta mageuzi ya kilimo kwa kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati na kwa gharama nafuu na kushirikiana na wizara ya viwanda kuhakikisha masoko ya mazao yanapatikana.
Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara, alisema: “Rais ameniamini nitajitahidi kutunza imani hiyo na uaminifu nitauonyesha kupitia kazi inayofanyika.