25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Uamuzi mgumu CCM

mangulaNa Khamis Mkotya, Dodoma

NI uamuzi mgumu, ndivyo unavyoweza kusema wakati Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) inapoanza vikao vya juu mjini Dodoma leo.
Vikao hivyo ni mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Kikao cha kamati hiyo kinatarajiwa kuanza saa nne asubuhi, ambapo wajumbe wa kikao hicho watajadili masuala mbalimbali, ikiwamo hatima ya makada sita wa chama hicho waliofungiwa.
Hata hivyo, taarifa ambazo zimelifikia MTANZANIA zinasema Kamati ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, ilikutana jana asubuhi kuanzia saa nne hadi saa kumi jioni.
Wakati vikao hivyo vikianza, baadhi ya wapambe wa wagombea urais, hususan makada sita waliofungiwa waliotua Dodoma kufuatilia vikao, wamekuwa na hofu iwapo wagombea wao watatoka kifungoni au la.
Mjumbe mmoja ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini, alilidokeza MTANZANIA kuhusiana na kikao hicho na kueleza kuwa kilichukua muda mrefu kutokana na uzito wa ajenda.
Mbali ya suala la makada sita, mjumbe huyo alisema baadhi ya makatibu wa chama wa mikoa na wilaya ambao walilalamikiwa katika kamati hiyo na baadhi ya wanaCCM kutokana na kukiuka taratibu za chama kwa kuanza kuwafanyia kampeni wabunge nao walihojiwa.
Mtoa taarifa huyo alisema baada ya kamati kumaliza kikao chake, Kamati ya Sekretarieti nayo ilikutana jana jioni kuendelea na vikao vyake vilivyoanza tangu juzi, kwa ajili ya kumalizia ajenda zitakazowasilishwa katika mkutano wa leo.
Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ambapo pamoja na mambo mengine, kitapitisha ajenda zitakazojadiliwa katika vikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), vitakavyofanyika kesho na keshokutwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliwataka wananchi kupunguza wasiwasi juu ya vikao hivyo na kueleza kuwa chama hicho kitamaliza vikao vyake salama na wajumbe watatoka wamoja na nguvu kubwa.
Nape alitoa taarifa hiyo jana jioni viwanja vya jengo la makao makuu (White House).
Alisema maandalizi kwa ajili ya CC na NEC yamekamilika.
Nape alisema baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu walianza kuwasili tangu jana jioni, huku wajumbe wa NEC wakiendelea kuwasili tayari kwa ajili ya vikao vya chombo hicho.
“Tunatarajia baada ya vikao hivi tutatoka Dodoma tukiwa wamoja na wenye nguvu tofauti na baadhi ya watu wengine wanavyotarajia,” alisema.
Akizungumzia vikao hivyo, Mkuu wa Utawala Ofisi Ndogo na Mjumbe wa NEC Zanzibar, Bakar Hamad Hamis, alisema matumaini yake ni kupata ajenda zitakazowaunganisha wana CCM.
“Tangu juzi kulikuwa na vikao mbalimbali vya maandalizi, ikiwamo sekretarieti, kamati ya masuala ya kanuni na ilani ambavyo viliendelea hadi jana jioni,” alisema.
Katika maeneo ya jengo la makao makuu ya CCM, kumekuwa na pilikapilika za wanachama na wasiokuwa wanachama wa CCM ambao wamekuwa wakijadili mustakabali wa vikao hivyo.
Mbali na hilo, wajasiriamali nao kama kawaida hawakubaki nyuma, kutokana na kupanga biashara zao, hususan sare za CCM, wakitumia vizuri fursa za vikao hivyo.
Wanachama wa CCM wamekuwa wakitega sikio Dodoma, kwani vikao hivyo ndivyo vinavyotarajiwa kutoa dira namna kitakavyowapata wagombea wake kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa katika vikao vya sekretarieti ni pamoja na maboresho ya mfumo wa kura za maoni, utakaotumika katika kuwapata wagombea wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

MAKADA
Itakumbukwa Februari, mwaka jana, CCM ilitoa adhabu ya kifungo kwa makada wake sita waliopatikana na hatia ya kuanza kampeni za urais kabla ya wakati, kinyume cha maadili na kanuni za chama hicho.
Makanda hao ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Lakini hadi jana mchana, Kamati ya Maadili ilikuwa haijakaa na kuandaa ripoti yake.
Kamati ndogo ya kuwachunguza inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, inatarajiwa kuwasilisha taarifa yake.
Chanzo chetu kutoka Dodoma kilisema: “Kaka nakwambia mambo yote sawa, lakini macho na masikio yako kwenye Kamati ya Maadili, hii ndiyo imebeba roho zetu hapa mjini.
“Tunaweza kutoka tunachekelea au tumenuna…si unajua inakuja na hukumu ya makada sita, tuwe wavumilivu mambo yanaanza kesho (leo).
“Kila kona ya mji huu tunahemea juujuu utafikiri bundi asiyekuwa na pumzi…lakini Mungu ni mwema, naamini atutusaidia ili tuvuke jahazi hili salama,” kilisema chanzo chetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles