28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

UAMUZI HUU WA SERIKALI NI WA KUPONGEZWA

MIAKA ya hivi karibuni kumekuwapo na wimbi kubwa la wanasiasa wanaochipukia katika ngazi mbalimbali, jambo ambalo si baya katika uhai wa masuala ya kisiasa duniani kote.

Wanasiasa wachanga anaoibuka, huwa ni hazina inayowezesha kupatikana kwa viongozi wa baadae katika nyanja mbalimbali.

Hivi karibuni tumeona kuna watu wengi wanateuliwa kushika nyadhifa kubwa za kisiasa serikalini, hata bila kupata mafunzo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako viongozi kupitia vyama vyao walipikwa vizuri.

Kutokana na kupikwa vizuri, viongozi hao walikuwa na mchango mkubwa kwa jamii kwani walijitoa kwa nguvu zao zote bila kutegemea kubebwa au kufanya jambo kwa shinikizo.

Lakini si hayo tu, viongozi hawa hawakuwa wepesi wa kuhongwa fedha ili mradi tu wapitishe jambo fulani kwa manufaa ya wachache kutokana na kunolewa vizuri kimaadili.

Leo tumelazimika kusema hayo, baada ya Serikali kuchukua uamuzi sahihi wa kuwapeleka wakuu wa mikoa na maofisa wengine wa Serikali kunolewa katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC), kilichoko Dar es Salaam.

Uamuzi wa kupeleka wakuu wa mikoa 13, makatibu wakuu wanne, naibu makatibu wakuu sita, makatibu tawala wane na viongozi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Magereza, ni jambo ambalo limekuja wakati mwafaka.

Katika orodha ya wakuu wa mikoa ambao wamepelekwa, tumeguswa kuona wengi wao ni vijana ambao ni hazina ya taifa katika uongozi kwa siku zijazo.

Miongoni mwa wakuu wa mikoa hao vijana ni pamoja na John Mongella (Mwanza), Mrisho Gambo (Arusha) na Anthony Mtaka (Simiyu).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Issa Haji Ussu Gavu, wakati akifungua mafunzo hayo juzi, alisema washiriki 45 wanapatiwa mafunzo ya muda mfupi chuoni hapo ambayo yamelenga kuboresha uelewa wao.

Sisi wa Mtanzania, tunaona jambo hilo ni jema kwani tunaamini malengo ya chuo hiki ni kutayarisha viongozi kwa masuala ya ulinzi na usalama.

Hivyo ni wazi kuwa kupitia mafunzo hayo, viongozi hawa – hasa wakuu wa mikoa, watapata ufahamu wa masuala ya ulinzi na usalama ambayo katika utendaji kazi wao wanayasimamia kutokana na kuwa ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama za mikoa yao.

Tunaamini mafunzo haya pamoja na kuwa ya muda mfupi, yatasaidia mno kufungua ukurasa mpya wa utendaji wa wanasiasa na viongozi ambao katika siku za karibuni umeonekana kuwa na tatizo kubwa.

Tumeshuhudia baadhi ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa mikoa wakiamuru wananchi au viongozi wengine kukamatwa ovyo na kuswekwa mahabusu.

Tunapenda kuona kozi hiyo inasawaidia kuwapa washiriki misingi ya uadilifu katika masuala ya uongozi wa umma na utendaji wao wa kila siku.

Wote tunakumbuka jinsi viongozi walivyokuwa wakipikwa katika vyuo vya uongozi kama Kigamboni, ambao walikuwa tofauti na hawa wa sasa katika masuala ya maadili.

Sisi MTANZANIA, tunashauri kozi za aina hii kwa viongozi ziwe endelevu ili kusaidia kutokuwa na viongozi wasiokuwa na ujuzi mkubwa wa kuongoza umma.

Tunafurahi kuona kozi hii imehusisha hadi maofisa kutoka taasisi za kijeshi ambao katika siku za karibuni, wengi wao wamekuwa wakiteuliwa kushika nyadhifa za kisiasa.

Lakini pia makatibu tawala wa mikoa ambao wana jukumu kubwa la kusimamia shughuli za kila siku wamehusishwa.

Ndiyo maana tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huu na kushauri jambo hili liwe endelevu kwani taifa linahitaji viongozi walionolewa vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles