23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Twaweza wazua mjadala

mtz1NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na Taasisi ya Twaweza umepokewa kwa hisia tofauti na watu wa kada mbalimbali.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliotangazwa jana, kama uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ungefanyika leo, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, angeibuka na ushindi wa asilimia 65, huku mgombea wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, akipata asilimia 25.

 

Akitangaza matokeo ya Twaweza Dar es Salaam  jana, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze, alisema utafiti huo umefanyika kati ya  Agosti na Septemba, mwaka huu.

Alisema utafiti huo ulihusisha watu 1,848 waliohojiwa katika mikoa tofauti ya Tanzania Bara kuhusu siasa na wagombea wa mwaka huu.

“Watu waliulizwa katika utafiti huo, endapo uchaguzi mkuu ungefanyika leo (sasa), wangemchagua nani? Asilimia 65 walisema wangemchagua Dk. Magufuli, asilimia 25 walisema wangemchagua Lowassa, wakati asilimia 3 wangemchagua mgombea mwingine na asilimia 7 hawakuwa na chaguo.

“Matokeo ya utafiti huu yamefanywa Tanzania Bara pekee, utafiti huu haumaanishi utakuwa utabiri wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, kwa sababu watu huwa na tabia ya kubadilika,” alisema Eyakuze.

Alisema katika utafiti huo, walibaini mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, anapendwa zaidi maeneo ya vijijini na watu wazima ambako amepata asilimia 66 na Lowassa anapendwa zaidi mjini ambako amepata asilimia 61.

Alisema utafiti huo, umebainisha zaidi ya asilimia 60 ya watu walio na elimu ya msingi waliohojiwa, walionyesha kumpenda Dk. Magufuli ambapo Lowassa alionekana kupendwa zaidi na vijana, ambapo wanaume wanaoishi mijini walimpa asilimia 28.

“Utafiti huu, umebaini wagombea wote wa CCM na Ukawa walionekana kupata nusu kwa nusu kwa upande wa wasomi,” alisema.

Alisema asilimia 26 ya waliomuunga mkono Dk. Magufuli, walisema kwa sababu ni mchapakazi, huku asilimilia 12 wanaomuunga mkono Lowassa, walisema anaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini.

 

UDIWANI

Akizungumzia nafasi ya udiwani, Eyakuze alisema CCM wana asilimia 60, Chadema (24), CUF (2), ACT-Wazalendo (1) na Ukawa (3).
UBUNGE

Kuhusu nafasi ya ubunge, alisema CCM wana asilimia 60, Chadema (26), CUF (3), ACT-Wazalendo (1), NCCR-Mageuzi (1) na Ukawa (3).

Kwa upande wa vyama, nafasi ya urais inaonyesha endapo uchaguzi ungefanyika sasa, CCM ingepata asilimia 66, Chadema (22) na Ukawa (3).

 

MARIA SARUNGI

Mwanaharakati Maria Sarungi akizungumza baada ya utafiti huo, alisema unaonyesha CCM inaongoza kutokana na kujitangaza zaidi.

“CCM wana uwezo wa kuweka mabango karibu nchi nzima tofauti na Ukawa au vyama vingine vya upinzani, inakuwa rahisi jina la mgombea wao kujulikana zaidi ya wengine”

 

UTAFITI WA CCM

Utafiti huo wa Twaweza, umekuja wiki moja baada ya mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM, January Makamba, kutangaza matokeo ya utafiti wa chama hicho na kusema kama uchaguzi ungefanyika sasa kingeshinda kwa asilimia 69.3.

Makamba alisema takwimu hizo, zimetokana na utafiti wa ndani uliofanywa katika majimbo 246 kati ya 269.

“Utafiti huu ulishirikisha taasisi nyingine binafsi, unaonyesha Dk. Magufuli atapata ushindi wa asilimia 69.3. Tunatarajia ushindi huu utaongezeka kadiri Watanzania wengi wanavyozidi kumsikiliza mgombea, ilani na sera zake,” alisema Makamba.

Alisema takwimu hizo, zinajumuisha mkutano uliofanyika mkoani Tabora na kukamilisha mikoa 12 na majimbo 94, ambapo alisikilizwa na wapigakura asilimia 70.

 

MITANDAO YA KIJAMII

Baada ya taarifa ya utafiti wa Twaweza kutangazwa, viongozi na watu wa kada mbalimbali wametoa maoni mbalimbali.

 

MBOWE

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kupitia ukurasa wake wa twitter alisema:  “Wahadhiri wetu mko wapi? Okoeni taaluma yenu mbona inavamiwa na wahuni wanaojifungia Lumumba wakitoka na makaratasi wanayaita utafiti.

“Nyakati za mwisho tutasikia mengi, ikiwa ni pamoja na tafiti za kikanjanja zisizokidhi vigezo vya kuitwa tafiti ili kuvutia upande uliokufa.”

 

LOWASSA

Muda mfupi baada ya Twaweza kutoa matokeo ya utafiti yaliyoonyesha mgombea urais wa CCM, Dk. Mafufuli anaongoza, mgombea wa Chadema, Lowassa, amewataka wananchi kujibu utafiti huo kwa kura.

Mgombea huyo, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema yeye anasubiri mafuriko ya kura Oktoba 25.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Viwanja vya Madeko, Jimbo la Ndanda wilayani Masasi mkoani Mtwara, Lowassa alisema: “Leo asubuhi (jana) kuna watu waliotoa matokeo ya kura ya maoni wakasema eti Magufuli amepata kama asilimia 65 mimi 25.”

Baada ya kutoa kauli hiyo, wananchi waliokuwa katika mkutano huo walidakia na kupaza sauti zao wakisema: “Waongo”.

Lowassa aliendelea kusema: “Sisi tujipange tuwajibu kwenye kura. Nangoja kwa hamu mafuriko ya kura kutoka kwa wana Ndanda na Watanzania wote. Tarehe 25 mnipe kura, mtashindwa kuona hizi mvi?”

 

SUMAYE

Naye Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, akizungumzia utafiti wa Twaweza katika mkutano huo wa kampeni mjini Masasi, alisema umepikwa ili kuwahadaa wananchi wajue Dk. Magufuli ndiye anayependwa zaidi na wananchi.

“Leo (jana) wametoa utafiti feki, hewa, uliotengenezwa. Wanasema ati leo kura ikipigwa Magufuli atapata asilimia 65 na Lowassa asilimia 25,” alisema Sumaye huku baadhi ya wananchi wakijibu: “Waongo”.

Sumaye, alisema: “Tumepita mikoa kibao, watu kwa maelfu wanakuja na kutaka mabadiliko, wao wakija hapa watu hawafiki hata robo ya ninyi, Dk. Magufuli mpaka azoe watu na malori.”

Alisema hakuna jema lolote hadi sasa ambalo CCM imefanya. “Leo wanataka kucheza na akili za watu ili wajue Magufuli ndiye anayependwa.”

 

MAKAMBA

Kwa upande wake, Makamba naye aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter: “Sishangazwi na utafiti wa Twaweza uliompa Magufuli asilimia 65 dhidi ya Lowassa asilimia 25. Imethibitishwa na utafiti wetu wa ndani.

“Utafiti hujibiwa kwa utafiti, si kwa kumtukana mtafiti au matokeo. Kabla hujamtukana mtafiti lete utafiti wako sahihi.”

 

MBILINYI

Aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Profesa Simon Mbilinyi, aliumwagia sifa utafiti huo na kusema umefuata vigezo vya kimataifa.

“Katika hatua za awali za utafiti huu, naweza kusema umefuata vigezo vyote vya utafiti… naamini pindi nitakaposoma taarifa yao kwa undani, naweza kutoa maoni zaidi,” alisema Profesa Mbilinyi.

 

  1. BISIMBA

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo-Bisimba, alisema huo ni utafiti ambao unatakiwa kujibiwa kwa kufanya utafiti ili kujua endapo matokeo hayo ni sahihi.

“Tuupokee kama utafiti, ni kawaida lakini, huwezi kuupinga kama hujafanya utafiti na kujua walitumia njia gani, walihoji watu gani na wangapi,” alisema Dk. Kijo Bisimba.

 

  1. KITINE

Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Dk. Hassy Kitine, alisema utafiti huo umeonyesha CCM imepata asilimia nyingi vijijini kwa kuwa imejiimarisha zaidi.

“Vyama hivi vimetofautiana namna vilivyojiwekea mizizi, hivyo utafiti unawakumbusha wanatakiwa wajiimarishe sehemu zote za nchi,” alisema Dk. Kitine.

 

PROFESA KAJUNA

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki, Profesa Sylvester Kajuna, alisema ni kawaida kufanya utafiti kwani hata mataifa mengine, yakiwamo Uingereza na Marekani hufanya.

Alisema Watanzania wanapaswa kukubaliana na utafiti huo, ingawa si hitimisho la matokeo ya uchaguzi.

 

  1. BANA

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Watanzania hawapaswi kuupuza utafiti huo, bali waufanyie kazi kwani muda wa kurekebisha changamoto upo.

“Huu utafiti wasiupuuze, bado tuna siku 30 hadi kufikia siku ya kupiga kura. kama vyama vitatoa  elimu kwa wapigakura wao wanaweza kubadili matokeo,” alisema.

 

MGOMBEA UDIWANI

Naye mgombea udiwani Kata ya Kyanyari, Wilaya ya Butiama mkoani Mara, Mgingi Mhochi, amepinga utafiti huo na kusisitiza kuwa hauwezi kuwazuia Watanzania kufanya mabadiliko.

“Napenda kuwaambia akina mama, vijana na wazee kuwa mabadiliko ni sasa, tusisubiri wakati mwingine, kwani hatujui hao watakaokuja muda huo watakuja na mawazo gani,” alisema.

 

IMEANDALIWA NA GRACE SHITUNDU, ESTHER MNYIKA, SHABANI MATUTU (DAR ES SALAAM

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles