NAIROBI, Kenya
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema watu wote 50 waliotoroka kutoka kwenye kituo cha karantini cha watu wanaoshukiwa kuwa na virusi vya corona mjini Nairobi watakamatwa tena na kurejeshwa tena kwenye vituo hivyo ili waendelee kujitenga kiufuatia mlipuko wa Corona.
Akizungumza na kituo kimoja cha redio nchini Kenya, Kenyatta amesema: ”Tutawatafuta watu wote 50 waliotoroka kituo cha karantini na kuhakikisha wanajitenga kutokana na mlipuko wa Covid -19 wa virusi vya corona”.
Kauli hiyo ya Rais Kenyatta, inakuja baada video ya watu wasiojulika kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii nchini humo, ikionyesha watu wakitoroka kituo cha karantini katika Chuo cha Mafunzo ya Tiba cha Kenya (KMTC).
”Msako wa kuwakamata watu 50 waliotoroka karantini unaendelea,Wakenya waheshimu hatua za kukabiliana na Covid-19.”, alisema rais Kenyatta.
Watu hao walioonekana wakikwea ukuta wa jengo la chuo hicho na kudondoka kwenye barabara ya Mbagadhi,kisha kuondoka kwa mwendo wa kasi na kuchangamana na wapiti njia wengine na baadae kutoweka.
Kituo cha karantini katika kilikua na watu 200 waliotengwa, baada ya kubainika walikutana na watu waliokuwa na virusi vya corona pamoja na wale waliokiuka amri za kutotoka nje na kutosogeleana.
Inaaminika baadhi walitoroka Jumatatu usiku, wakati mvua ilipokua inanyesha na waliosalia walitoroka wakati wa kifungua kinywa wakati ambao maofisa wa usalama wanakua na shughuli nyingi.
Baadhi ya Wakenya wanaunga mkono hatua ya watu kutoroka kwenye kituo cha karantini. Mmoja wao ni Royn Kean ambaye kupitia mtandao wa Twitter anasema ”Ninawaunga mkono, unawezaje kunilazimisha kulipia karantini”
Baadhi ya watu waliokaa maeneo ya karantini, wamekuwa wakilalamika kupitia vyombo vya habari juu ya maisha katika vituo hivyo ambayo wanasema ni ghali kutokana na wamelazimishwa kujilipia gharama za malazi na chakula.
Wengine wanahofia kuwa kuwekwa katika vituo hivyo bila maambukizi ya corona kunawaweka katika hatari ya kuambukizwa na wenye virusi hivyo ambao wanalazimika kuishi nao katika karantini.
Baadhi wanasema kuwa wasi wasi wa kusubiri kwa muda mrefu kupimwa ili kujua matokeo yao ikiwa wana virusi au la ni jambo linalowaathiri kisaikolojia.
Hata hivyo, picha za kituo cha karantini kilichotorokwa na watu 50 zinaonekana kama bweni la kawaida la shule ya sekondari , huku vitanda vyake vikiwa na vyandarua vilivyoning’inizwa vitandani.
Serikali ya Kenya, imekua ikikosolewa na makundi mbali mbali kwa kuwaweka washukiwa wa maambukizi ya corona katika maeneo yanayofanana na mahabusu.
Baadhi ya vituo hivyo vya karantini vimetajwa kuwa na hali asipostahili mtu kuishi na kwamba vinawaweka watu waliomo katika hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.
Ukatili unaodaiwa kufanywa na maafisa wa usalama.
Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Human Rights Watch) linasema watu takriban sita wamefariki kutokana na ghasia za polisi katika kipindi cha siku 10 tangu serikali ilipotangaza sharia ya kutotoka nje kuanzia saa moja jioni nchini Kenya tarehe Machi 27, mwaka huu ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.
Kulingana na Shirika hilo, polisi bila sababu wamekua wakiwapiga risasi na kuwapiga watu masokoni au wanapokua wakirejea nyumbani kutoka kazini, hata kabla ya kuanza kwa kipindi cha marufuku hiyo.
Human Rights Watch linasema polisi wamekua wakiingia kwa nguvu katika nyumba na maduka ya watu.
Virusi vya Corona: Jinsi marufuku ya misongamano inavyokumbana na vikwazo Afrika
Kufuatia ukosoaji kutoka makundi mbalimbali juu ya ukatili uliofanywa na polisi katika nguvu katika Kaunti ya Momba, likiwemo shirika la Human Rights Watch, Rais Uhuru Kenyatta aliomba msamaha wa jumla juu ya matumizi ya nguvu yaliyofanywa na polisi, lakini hakuwaagiza polisi kuacha unyanyasaji , linasema shirika hilo katika ripoti yake.
“Inatisha watu wanapoteza maisha yao kwa kile kinachosemekana kuwa wanalindwa na maambukizi ,” amesema Otsieno Namwaya, mtafiti wa ngazi ya juu wa Human rights Watch barani Afrika “Ukatili wa polisi sio tu unakiuka sharia ;bali pia hausaidii katika vita dhidi ya kuenea kwa virusi .”
Hatua za dharura zilizochukuliwa ni pamoja na kufungwa kwa baa zote na wenye hoteli kuruhusiwa tu kuuza chakula cha kwenda kula nyumbani.
Ibada za Kanisa na sala za pamoja misikitini, zimesitishwa huku mazishi ya kiruhusiwa kuhudhuriwa na familia ya marehemu pekee.