IS-HAKA OMAR-ZANZIBAR
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema chama hicho kimejizatiti kutatua kero za wananchi na kusimamia demokrasia kwa kukemea vitendo viovu vinavyohatarisha amani na utulivu wa nchi.
Kauli hiyo aliitoa katika ziara yake ya kukagua uhai na utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
Alisema vipaumbele ni kutekeleza kwa kasi ahadi zilizotolewa na taasisi hiyo kwa wananchi wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita.
Alisema CCM kinaendelea kuaminiwa, kupendwa na kuthaminiwa na mamilioni ya Watanzania kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa sera zake kwa kutatua changamoto za jamii kwa wakati mwafaka.
Dk. Mabodi alisema katika kusimamia dhana ya demokrasia, CCM haitasita kukemea vitendo viovu vinavyoonyesha kuvunja sheria za nchi, hasa vinavyotekelezwa na baadhi ya vyama vya upinzani.
“Tumekubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi tushindane kwa sera na siyo kushindana kwa vituko na vurugu.
“Ni muhimu kila mwanasiasa kujitathimini juu ya mwenendo wake kwa jamii anayoiongoza,” alisema Dk. Mabodi.
Alisema zama hizi CCM mpya imekuwa ni kimbilio la wananchi wanaoamini katika siasa za maendeleo ambao wametelekezwa na vyama vyao na kupokewa vizuri ndani ya chama hicho ili wanufaike na demokrasia iliyotukuka.
Aliwataka viongozi na watendaji wa CCM kutowawekea vikwazo wananchi wanaotaka kujiunga na chama na badala yake wapewe fursa hiyo bila masharti magumu na kuwasomea miongozo na itikadi za taasisi.