28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

TUSOME KITABU: UTUMWA WA JAMII ZA KIAFRIKA

Na Markus Mpangala,

LEO tunaendelea na uchambuzi wa kitabu cha ‘Shetani Msalabani’ ambacho ni moja kati ya riwaya zilizoandikwa na ngwiji wa fasihi simulizi, Ngugi wa Thiong’o raia wa Kenya.

Kitabu hiki ni tafsiri ya kile kilichochapishwa kwa lugha ya Kiingereza, ‘The Devil on the Cross.’ Kimechapishwa  East Africa Educational Publishers ya nchini Kenya na kupewa nambari ya usajili ISBN 978-9966-46-167-4. Kinapatikana katika duka la vitabu la TPH Bookshop jijini Dar es Salaam.

Kama tulivyoanza wiki iliyopita juu ya utangulizi, mandhari na dhamira ya riwaya hii. Tulikomea wakati Wariinga akiahidiwa mambo kemkem ili akubali kuwa kimada wa Kihara. Katika ahadi za Kihara kwa Wariinga ndipo tunapata dhamira nyingine ya mwandishi juu ya ukosefu wa uzalendo wa wananchi wa Kenya ambao wamechorwa kama mfano wa nchi za Afrika.

Mwandishi anaandika; “nyumba hiyo niipambe pembe hadi pembe kwa kila kitu vitanda,  meza, viti, magodoro, mapazia, mazulia, vitambaa-chochote unachotaka. Nitaviagiza vitu vyote kutoka Paris, London, Berlin, Rome, New York, Tokyo, Stockholm na hata Hong Kong,”(uk.21).

Mwandishi anaonyesha tatizo kubwa la kushindwa kuthamini bidhaa za kwetu na badala yake tunakimbilia kununua za nje.

Tatizo hilo limekuwa likizungumzwa kwa miaka mingi hapa nchini Tanzania, ambapo wajasiriamali wamekuwa wakilalamikia kasumba ya kupuuzwa bidhaa za Kitanzania.

Badala yake tunaambiwa Watanzania hupendelea zaidi bidhaa za kigeni hali ambayo inawanyima wajasiriamali kupiga hatua kutokana na ubunifu wao.

Aidha, Ngugi anaelezea namna wananchi wa Bara la Afrika walivyohangaika kuupata uhuru lakini wakakosea fursa ya kufaidi matunda baadaye.

“Tulipopigana vita vya uhuru, hatukubaguana na kusema; huyu ni maskini au amevaa matambara na arudishwe nyuma, huyo mwenye matambara hata aghalabu ndiye aliyekuwa katika mstari wa mbele vitani. Na mwenye tai na suti alikuwa akikimbilia kofia ya beberu iteguliwapo kwa risasi za mashujaa wetu wazalendo.” (uk.47).

Dhima kuu tunayopata hapo ni namna matabaka yalivyopanuka. Mwandishi anaonya juu ya hatua hiyo kama mojawapo ya sababu zinazochangia kukosekana kwa utulivu ndani ya jamii.

Kwamba watu wanapofika mahali wananyimwa heshima au kutopatiwa mambo muhimu katika maisha yao binafsi, basi kinachofuata ni mtikisiko wa jamii.

Jamii inajengwa katika misingi ya haki sawa, amani na upendo. Ubaguzi wowote huchangia ghasia kubwa mno na kusababisha maelewano hafifu.

Mwandishi wa riwaya hii ameonyesha upande mbaya wa itikadi ya ubeberu na ukoloni, pamoja na baada ya ukoloni. Tunasimuliwa juu ya sherehe kubwa ya wanyang’anyi iliyoandaliwa pangoni.

Katika sherehe hiyo walikutana watu wazito au tuseme vibaraka wa wakoloni ambao walikuwa wakihadithiana umahiri wa kupora rasilimali za Kenya (Afrika). Wangari, Muturi na Mwaura ni miongoni mwa watazamaji wa sherehe hizo. Walishangazwa na ujasiri wa Wakenya wenzao kujisifu namna walivyoliibia taifa lao.

Katika muktadha huo, mwandishi anajaribu kuonyesha kuwa licha ya wakoloni kuondoka na kukabidhi madaraka kwa wenyeji bado kulikuwa na wizi na unyang’anyi mkubwa uliokuwa ukiendelea.

Unyang’anyi huo ulikuwa na malengo ya kutojali hatima ya Kenya na wananchi, wala ubora wa huduma zenyewe.

Mwandishi anamtumia mhusika  Kihahu wa Gatheeca ambaye anajiita jina la kigeni la Lord Gabriel Bloodwell Stuart Jones, akisema; “nilitazama kwa makini kuangalia upepo uvumako. Nikifahamu kuwa Mwafrika tajiri akinunua shamba kubwa hawezi kumwajiri Mwafrika mwenzake kuwa mkurugenzi; hawezi kumwajiri awe mhasibu wake; humwajiri Mzungu au Mhindi. Waafrika wawili wanapozungumzia mambo, hawawezi kuzungumza kwa lugha za kikwao, bali hutumia za wageni….(uk149).

Hiyo ni mifano ambayo ilitolewa mwaka 1978 katika kipindi ambacho nchi za Afrika hazikuwa na uzoefu wa kiundeshaji. Hata hivyo, dhamira hiyo iko sahihi hadi sasa kutokana na mambo yanayoendelea katika jamii zetu.

Mwandishi anatuonyesha utamaduni wa kutojali hatima za wengine kwa kutoa huduma mbovu pale anaoponyesha Gatheeca akimiliki shule ya watoto na kumwajiri Mzungu kikongwe ambaye hakuwa na uwezo wa kuhimili shughuli.

Hatuna sababu ya kupinga kuajiriwa Wazungu lakini kiini cha kuwapa majukumu wasiyoyaweza pamoja na kutoaminiana baina ya Waafrika ndicho kitu anachokionyesha  Ngugi wa Thiong’o.

Kwa hakika simulizi za Shetani Msalabani haitoshi kukumalizia hapa. Ni muhimu ukikapata kitabu chenyewe kisha ukaburudishwa na vituko, vitimbi na timbwili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles