26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

BODI: KABILA AMBALO WANAUME HUSHINDANA UNENE ETHIOPIA

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI,

KIONACHO pichani ni wanaume wa kabila lililopo katika bonde moja eneo la porini nchini Ethiopia.

Wanaume hawa hushindana kumpata mshindi atakeyekuwa mnene kuliko wote ndani ya kipindi cha miezi sita.

Kwa nusu hiyo ya mwaka, watu hao wachuanao wa kabila la Bodi huwa hawanywi kitu chochote zaidi ya maziwa freshi na damu ya ng’ombe ili kuongeza unene.

Wakati wa kipindi hicho cha ‘ligi’ huwa hawaruhusiwi kufanya tendo la ndoa wala kuondoka katika vibanda vyao.

Mshindi wa mchuano huo wa kila mwaka hupata sifa na heshima kemkem kutoka kabila lao hilo kutokana na kutumia miezi sita kuongeza uzito kwa kunywa maziwa na damu ya ng’ombe.

Katika tukio hilo, wanawake na wasichana huwa na kazi ya kuleta maziwa na damu kila asubuhi, ambazo huhifadhiwa katika vyungu au chombo kilichotokana na mianzi.

Ijapokuwa hakuna zawadi kwa mshindi, kuna sifa, hadhi na heshima kedekede na zaidi ya yote ukubwa wa umbo, yaani kuwa na kiuno kipana kunahesabiwa kama sumaku inayovuta wanawake wa kabila hilo.

Mchuano huo ni sehemu ya ibada ya Ka'el, inayofanyika kuadhimisha mwaka mpya. Kila familia huruhusiwa kumtoa mwanamume ambaye bado hajaoa kwa ajili ya kushiriki. Anaposhiriki tu hupumzika katika kibanda chake, haruhusiwi kuhama au kufanya tendo la ndoa wakati wa kipindi chote hicho.

Mpiga picha Eric Lafforgue, ambaye alichukua picha hizo, anasema: “Ng’ombe pia husujudiwa mno na kabila la Bodi na hivyo huwa hawauawi. Damu huchukuliwa kwa kutengeneza shimo katika mshipa wa damu wa ng’ombe kwa kutumia mkuki au shoka na huliziba kwa kutumia udongo wa mfinyazi.

Katika siku ya sherehe, wanaume hao hupaka miili yao udongo wa mfinyazi na majivu kabla ya kutoka katika vibanda vyao.

Anaendelea: “Wanaume wanane hunywa maziwa na damu siku nzima. Bakuli la kwanza la damu linanyewa wakati wa mapambazuko. Mahali hapo huvamiwa na inzi.”

Anasema mwanaume hutakiwa kunywa haraka kabla damu haijaganda lakini wengine hawawezi kunywa kila kitu na hivyo huitapika.

Bahati mbaya sana, ibada ya Ka'el na utamaduni wa Bodi unatishiwa na Serikali ya Ethiopia, ambayo inapanga kuwahamisha na kuwatawanya kote nchini humo watu 300,000 wa kabila hilo kutoka ardhi zao.

Kwa sasa, kabila hilo linaendelea na utamaduni wake ikiwamo kusherehekea utamaduni wa Ka'el kila ifikapo Juni.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles