23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

Tusisubiri Walimu watende makosa ili tuwaadhibu- Nkwama

Na Adili Mhina, Dodoma

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama amewataka watendaji wa Tume hiyo kujikita zaidi katika kutoa elimu kwa walimu ili wazingatie maadili ya kazi yao badala ya kukaa na kusubiri watende makosa ili wawachukulie hatua za kinidhamu.

Agizo hilo amelitoa hivi karibuni alipofanya ziara katika ofisi za TSC Wilaya ya Dodoma na Chamwino kwa lengo la kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku pamoja na kuona namna ofisi hizo zinavyotoa huduma kwa wateja katika wiki ya Utumishi wa Umma.

Nkwama alisema kuwa TSC ina wajibu wa kuwasaidia walimu katika masuala ya maadili na maendeleo ya utumishi wao ili wawe na ustawi mzuri na kufanya watoe elimu bora kwa wanafunzi.

“Tumepewa dhamana ya kuwahudumia walimu katika masuala ya ajira, maadili na maendeleo yao. Sasa ni lazima tujikite katika kuzuia walimu wasijiingize katika vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kuwa wakiwa na maadili mema ndipo tunaweza kujivunia kuwa tunafanya kazi,” alisema.

Aliwataka watendaji wa ofisi hizo kuhakikisha wanatumia muda wao kuwafikia walimu na kuwapa elimu kuhusu haki, wajibu na maadili ya utumishi ili kuwaepusha na makosa ya kinidhamu.

Aliongeza kuwa mamlaka za nidhamu ambazo ni wakuu wa shule na TSC ngazi ya wilaya hawajatekeleza wajibu wao ipasavyo katika kuwasaidia walimu kuelewa umuhimu wa kuzingatia miiko na maadili ya kazi yao katika utendaji wa kazi.

Alifafanua kuwa mamlaka hizo zinapaswa kubaini mienendo ya walimu isiyofaa na kuwarekebisha mapema kabla ya kufikia hatua ya kuanzisha shauri la nidhamu ambao linaweza kusababisha mwalimu apoteze ajira yake.

“Haiwezekani mkuu wa shule anaona mwalimu siku ya kwanza hayupo shuleni, siku ya pili hayupo halafu badala ya kufanya jitihada za kumtafuta ili ajue tatizo na kuona namna ya kumsaidia, anasubiri siku tano ziishe apeleke taarifa kwa mkurugenzi ili hatua za kinidhamu zichukuliwe, hii siyo sawa,” alisema.

Aliongeza kuwa pale inapotokea mwalimu anafukuzwa kazi ni lazima mamlaka za nidhamu zijitafakari kama zinatekeleza wajibu wao wa kuwaelimisha walimu inavyotakiwa.

“Hatuwezi kujivunia kuwa tumefanya kazi nzuri endapo tunaona bado walimu wanafukuzwa kazi kwa makosa ya kinidhamu. Pale inapotokea tumemfukuza kazi mwalimu lazima tujiulize kuwa tumetekeleza wajibu wetu wa kutoa elimu na kumrekebisha mwalimu kama ianvyotakiwa,” alisisitiza.

Pamoja na kusisitiza hayo, Katibu huyo alisema pale ambapo mwalimu amerekebishwa lakini hataki kubadilika ni lazima mamlaka za nidhamu zimchukulie hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu husika.

Katika kuadhimisha wiki ya utumishi wa Umma, Katibu huyo alipata fursa ya kuona namna ofisi hizo zinavyopokea wateja na kuwahudumia, pia alipokea malalamiko na changamoto za watumishi wa ofisi hizo na kuahidi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili waendelee kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi ya kuwahudumia walimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles