26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tupo salama kwa kiwango cha kimataifa – Dk. Kimei

Dk. Kimei
Dk. Kimei

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KUKUA kwa teknolojia kumerahisisha ufanisi wa utunzaji fedha kutokana na kuwapo kwa benki na hivyo kuchangia kuongezeka kwa mwamko wa watu kutumia huduma za kibenki.

Hapa nchini kuna benki 54 na kila moja imekuwa ikipambana kuhakikisha inaliteka soko la fedha.
Hata hivyo pamoja na wingi huo wa mabenki swali kubwa ambalo limekuwa likiwaumiza vichwa watu wengi ni juu ya suala la usalama wa fedha zao.

Wengi wana matarajio kuwa benki ni sehemu salama ya kuweza kuhifadhi fedha zao lakini suala la usalama huweza kuthibitishwa kupitia tafiti mbalimbali za kuangalia uwezo wa taasisi husika katika huduma zinazotolewa.

Hivi ndivyo ilivyofanya Benki ya CRDB ambayo iliamua kuomba kufanyiwa tathmini na Kampuni ya Kimataifa ya Moody’s inayojihusisha kutathmini uwezo wa taasisi za kifedha.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Marekani, inaongoza kwa tafiti, uchambuzi wa kifedha, takwimu na viwango duniani, iliitunuku benki hiyo darala la uwezo wa kuhimili madeni na athari nyingine za kifedha.

Lengo la tathmini hiyo lilikuwa kuugundua uwezo wa benki hiyo wa kuhimili misukosuko ya kiuchumi kadhalika kuwatia imani zaidi wawekezaji.

Viwango vinavyotolewa na kampuni hiyo mbali ya kuonyesha ubora wa huduma, pia vinalenga katika kuwasaidia wawekezaji kufanya maamuzi ya kuwekeza katika masoko ya mitaji na dhamana.

Matokeo ya utafiti huo yanaifanya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki chache katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zilizofanikiwa kutunukiwa daraja la juu kimataifa katika sekta ya fedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, anasema darala walilotunukiwa ni B1 ambalo limetokana na matokeo mazuri ya benki hiyo katika huduma za mikopo, amana za kigeni na amana za ndani.

“Matokeo ya daraja hili ni kielelezo cha matokeo mazuri na ubora wa benki ambao umekuwa ukipanda na hivyo kuvutia wateja wa kawaida na mashirika mengi ndani na nje ya nchi kuichagua kuwa mtoa huduma wao.

“Daraja hili litasaidia kuvutia wawekezaji wa nje pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa kufanya biashara na benki yetu na hivyo kutanua wigo wa kibiashara. Wateja waelewe kwamba tuko salama kwa kiwango cha kimataifa,” anasema Dk. Kimei.

Nchi zingine zenye daraja kama hilo ni Kenya na Nigeria. Anazitaka taasisi mbalimbali kufanya tathmini na kuweka wazi uwezo wao wa kifedha ili kunufaika na fursa za uwekezaji katika soko la kimataifa.

Pia anasema uwezekano wa bei za hisa zao kupanda utaongezeka maradufu na kwamba wataweza kukopa kwa gharama nafuu na hivyo uwezo wa kutengeneza faida utaongezeka.

“Tumekuwa tukitafuta mikopo ya riba nafuu kutoka mashirika ya kimataifa kama IFC, licha ya kupata lakini masharti na gharama za mikopo inakuwa migumu,” anasema Dk. Kimei.

Hisa za benki hiyo pia zinaendelea kufanya vizuri katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
Naye Meneja Masoko wa benki hiyo, Tully Mwambapa, anasema benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 1996 imeendelea kukua hadi kufikia benki inayoaminika na kuongoza kwa ubunifu katika soko.

“Benki yetu imekuwa ikirekodi ongezeko la faida kila mwaka tangu ilipoanzishwa na imekuwa ikilipa gawio kila mwaka kwa wanahisa wake. Benki ilipiga hatua muhimu hivi karibuni baada ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kuanzisha kampuni tanzu ya CRDB Burundi,” anasema Mwambapa.

Anasema utafiti wa Moody’s umeongeza imani kwa wateja wa benki hiyo kwamba fedha zao ziko mahali salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles