Na Christian Bwaya
PAMOJA na changamoto za malezi ya shule za bweni tulizoziona, bado mzazi anaweza kulazimika kumpeleka mwanawe kwenye shule hizi. Kwanza, kuna suala la kazi. Wazazi wanaofanya kazi mbali na familia zao wanaweza kuamua kuwapeleka watoto kwenye shule ya bweni ili wasiwe na wasiwasi na uangalizi wao.
Pili, hutokea familia zikawa na misuguano ya uhusiano. Wazazi wanaofarakana wanaweza kuamua kumlinda mtoto kwa kumpeleka shule ya bweni. Lakini pia kuna suala la watoto wanaoachwa na wazazi (yatima), au watoto wanaozaliwa kwenye mazingira yanayowanyima uhusiano wa kifamilia.
Sambamba na hilo, kuna imani imejengeka kwa wazazi –wenye uwezo wa kiuchumi– kuwa mazingira ya shule ya bweni yanamwezesha mtoto kujifunza vizuri zaidi kuliko anapokuwa nyumbani.
Ndio kusema yapo mazingira yanayoweza kufanya shule ya bweni isikwepeke. Makala haya yanajaribu kuangazia mambo ya msingi kuzingatiwa mzazi anapoamua kumpeleka mwanawe kwenye shule za bweni.
Malezi yenye ubora
Kama tulivyokwisha kuona, suala la ubora wa malezi kwenye shule hizi linaonekana kuwa na changamoto nyingi. Ni kawaida kukuta shule nzima ikitegemea huduma ya mlezi mmoja. Hali hii, kama tulivyoona, huathiri uwezekano wa mtoto kupata msaada unaokidhi mahitaji yake ya pekee.
Jiridhishe kuwa shule unayompelekea mtoto ina walezi wa kutosha. Idadi ya walezi iwiane na idadi ya watoto wanaolelewa na mlezi mmoja. Lengo ni kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika makundi madogo madogo yanayowawezesha kufahamiana na kushirikiana kwa karibu.
Kwa mfano, idadi ya walezi wanaowatazama watoto wadogo wa darasa la kwanza inabidi iwe kubwa kuliko idadi ya walezi wanaowatazama watoto wa darasa la nne au la saba. Mantiki ya utaratibu huu ni ukweli kuwa watoto wadogo wana mahitaji mengi zaidi ya wenzao wenye umri mkubwa zaidi.
Kadhalika, watoto wa umri mdogo hawana uwezo mzuri wa kusema mambo yanayowasibu hivyo wanahitaji mtu wanayeweza kumwamini wamwambie mambo yao. Ni kwa msingi huo, epuka shule inayokuwa na uwiano mdogo wa mlezi na watoto.
Vile vile, kwa kuwa unampeleka mtoto mdogo kiumri mbali na wewe, jiridhishe kuwa shule inatumia walezi wanaoweza kufanya wajibu wa mama. Hapa tunamaanisha kuwa mlezi anayehudumia watoto anapaswa kuwa na utulivu, upendo na uelewa wa mahitaji ya watoto pasipo kujisikia kukerwa na madai mengi ya watoto.
Ubora wa huduma
Katika mipaka ya makala haya, ubora wa huduma ni kupatikana kwa malazi safi, chakula bora, usalama na utaratibu mzuri wa usafi kwa watoto. Kadhalika, ubora unaweza kumaanisha namna mazingira ya shule yanayolinda faragha na hadhi ya mtoto.
Tunapozungumzia faragha tunaaminisha haki ya mtoto kuishi katika mazingira yasiyoruhusu mwingiliano usio na mipaka kati ya mtoto na watu wengine wakiwemo watoto wenzake. Mwingiliano huu ni pamoja na watoto kuchangia vitanda, watoto wengi kulala chumba kimoja, kuchangia mahali pa kuweka vifaa vyao kwa namna ambayo mtoto anapoteza umiliki wa vitu vyake.
Muhimu kujiridhisha kuwa shule inawalaza watoto katika mazingira yanayoheshimu faragha ya mtoto mmoja mmoja. Watoto wadogo wasichanganywe na watoto wakubwa wala kuishi. Mchanganyiko wa watoto usiozingatia umri unaweza kufanya iwe rahisi kwa watoto wakubwa kuwaambukiza wadogo zao tabia walizotoka nazo nyumbani.
Inaendelea