28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAYOPASWA KUYAFAHAMU KUHUSU SHULE ZA MSINGI ZA BWENI – 2

Na Christian Bwaya,

JUMA lililopita tuliona shule za msingi za bweni zinavyochukua nafasi yake kwenye malezi. Ingawa idadi kamili ya watoto wanaosoma katika shule za msingi kwa mfumo wa bweni haifahamiki, ni dhahiri hitaji la shule za bweni ni kubwa kwa sasa.

Tuliangalia sababu mbalimbali zinazowafanya wazazi wengi kuwapeleka watoto wadogo kusoma mbali na nyumbani. Kwanza, imani kuwa shule hizi zinawasaidia watoto kujifunza vizuri kuliko wanapokuwa nyumbani. Lakini pia, changamoto za kifamilia ikiwamo migogoro baina ya wazazi na ndugu, mazingira magumu ya kazi kwa wazazi; wazazi kutokuwa na uhakika wa malezi wanayoyapata watoto wakiwa nyumbani ni baadhi ya sababu.

Mwaka 2015 mwandishi wa makala haya alifanya utafiti katika shule hizi za msingi za bweni. Lengo la utafiti huo uliokuwa sehemu ya tunuku ya kitaaluma lilikuwa kulinganisha mazingira ya kimalezi katika shule hizo na yale ya nyumbani wanakoishi watoto.

Watoto waliokuwa wakisoma kwenye shule moja kwa mfumo wa kutwa na bweni wenye umri wa miaka sita kwa darasa la kwanza na miaka saba kwa darasa la pili walilinganishwa kwenye maeneo makuu manne kama ifuatavyo; umahiri wao kiakili na kitaaluma kama vile uwezo wa lugha, kuhesabu, kuandika; tabia mahususi za watoto mfano namna wanavyojiamini, uhusiano wao na wengine; aina ya malezi wanayoyapata watoto na namna mazingira hayo yanavyowasaidia watoto kujenga uwezo wa kujitegemea.

Itakumbukwa kuwa katika siku za nyuma hapakuwa na utamaduni huu wa kuwapeleka watoto wadogo kusoma mbali na familia zao. Tulizoea kuona watoto angalau wenye miaka kuanzia 13 na kuendelea wakipelekwa kwenye shule za sekondari za bweni. Mambo yamebadilika.

Kama tulivyokwisha kubainisha, pamekuwa na ongezeko la mahitaji ya shule hizi kwa ngazi ya chekechea na madarasa ya awali. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa kiutafiti unaoweza kuwasaidia wazazi kufanya uamuzi sahihi pindi wanapofikiria kuwapeleka watoto wao  kwenye shule hizi. Utafiti uliotajwa ulilenga kuchunguza kwa kiasi gani mazingira ya bweni kwa watoto wadogo wa miaka sita na saba yanaweza kufanana au kutofautiana na mazingira ya nyumbani ambayo wengi tunayafahamu.

Katika sehemu hii, tunaangalia mchango chanya wa shule hizi za bweni kwa kutumia matokeo ya utafiti huo uliofanywa katika mazingira ya nchi yetu.

Mazingira sisimushi kitaaluma

Shule za bweni zilizohusishwa katika utafiti huo zilionekana kuwa na mazingira bora zaidi kitaaluma ukilinganisha na mazingira ya nyumbani wanakoishi watoto. Upimaji wa umahiri wa watoto kiakili na kitaaluma ulionesha wazi kuwa, kwa ujumla, watoto wa bweni walikuwa na uwezo mzuri wa kitaaluma.

Kwa watoto wa miaka sita, ilionekana kuna tofauti kubwa kati ya watoto wa bweni na wenzao wanaosoma kwa mfumo wa kutwa. Hata hivyo, tofauti hiyo ilikuwa ndogo kwa watoto wa darasa la pili mwenye miaka saba.

Katika kuchunguza sababu za tofauti hiyo, mambo kadhaa yalijitokeza. Kwanza, kuwapo ratiba isiyobadilika kwa watoto wa bweni. Mtoto anayelala shule, kwa mfano, alikuwa na uwezo wa kujua wakati upi anapaswa kufanya nini kuanzia anapoamka mpaka anapokwenda kulala. Mtoto anayejua utaratibu anaopaswa kuufuata kwa siku anakuwa na utulivu wa kiakili kuliko mwenzake asiyejua kitu gani kitafanyika wakati gani.

Itaendelea…

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles