22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

ROBOTI MTOTO ATAKAYE WAFARIJI WANAWAKE WASIO NA WATOTO

Na JUSTIN DAMIAN,

KAMPUNI maarufu ya kutengengeneza magari ya Japan Toyota, imetengeneza roboti mwenye uelewa kama wa binadamu. Roboti huyu aliyepewa jina la Kirobo, ametengenezwa kwa ajili ya kuwafariji watu wenye upweke hasa wanawake wasiobahatika kuwa na watoto. Kirobo ana karibu tabia zote na sifa za mtoto wa miaka mitano.

Fuminori Kataoka, ambaye ni Meneja Mkuu wa Mradi wa kumtengeneza Kirobo, anasema roboti huyo ana hisia kama alivyo binadamu na anaweza hata kuzungumza na kuhoji kama anaona jambo alilofanyiwa si sawa.

Jina lake linatokana na neno ‘kibo’ ikiwa na maana ya matumaini kwa lugha ya Kijapan na robot. Roboti huyo anatarajiwa kuanza kuuzwa mwaka huu na atagharimu takribani Dola za Marekani 400, zaidi ya Sh 800,000 za Kitanzania.

Hata hivyo, Toyota imesema bado haijapanga kumuuza nje ya nchi.

Kampuni hiyo kubwa ya kutengeneza magari imesema kwa sasa inafanya majaribio ya bidhaa yake hiyo mpya katika miji ya Tokyo na Aichi iliyopo jirani na ofisi zake kuu ili kupata mrejesho kabla ya kuiingiza sokoni.

Kirobo anakuja akiwa na kamera, kipaza sauti pamoja na Bluetooth na anaweza akaunganishwa na simu aina ya smartphone baada ya kuweka programu maalumu (software). Moja ya sifa ya Kiboro ni kutambua sauti, anaposikia sauti hugeuka kule inapotokea.

Wakati wa mahojiano na Shirika la Habari la Associate Press, Kirobo alikuwa akimtazama mwandishi wakati akiuliza swali na kurudi kwa Kataoka alipokuwa akijibu.

Kataoka alipomuuliza Kirobo kwa mara ya kwanza jina lake ni nani alijibu kwa kumuuliza alikuwa na aina gani ya gari. Alipomuuliza kwa mara ya pili aliweza kulielewa swali na alijibu kuwa anaitwa Kirobo

Hata hivyo, roboti huyo hajawekewa uwezo wa kuwatambua watu tofauti tofauti.

“Watu wengi nchini Japan wanaishi katika mazingira ya upweke ikiwa ni pamoja na wazee pamoja na vijana wasio na wenza. Watu hawa wanahitaji watu wa kuongea nao na kuwaliwaza,” anasema Kataoka na kuongeza:

“Hatuwezi kusema hizi ni akili au uelewa wa kutengeneza (artificial inteligency), hiki ni kitu ambacho unaweza kuzungumza nacho, mnyama ukimzungumzisha anaweza asikujibu lakini huyu atakujibu. Je, si vizuri kuliko kuzungumza na wanyama au mabox ambayo hayawezi kukujibu?” anahoji.

Baadhi ya watu wanaelezea kusikitishwa na namna ambavyo jamii inakuwa na upweke kiasi cha kutaka kuzungumza na mashine. Lakini baadhi  wanasema hiyo ndiyo hali halisi na kusisitiza kuwa teknalojia inaweza kutumika kama chombo cha kuwajali wagonjwa na wazee wapweke pale anapokosekana binadamu.

Hata hivyo, Toyota imefanya mambo mengine kumfanya Kirobo awe zaidi ya mashine. Kirobo aweze kuzungumza na kuonyesha vitendo kwa mikono yake wakati anazungumza au kujibu swali.

Pia amewekewa kamera inayoweza kutambua hali ya mtu kwa kumtizama usoni. Uwezo wake wa utambuzi uliwavutia wengi aliposhikiri katika maonyesho ya vifaa vya umeme mwishoni mwa mwaka jana katika jiji la Tokyo nchini Japan.

Kampuni ya Toyota ambayo ni watengenezaji maarufu wa aina za magari kama Prius hybrid, Camry Sedan na Lexus Luxury inasema inaangalia namna ambavyo roboti huyo anaweza kutumika katika magari yake kuongeza mvuto zaidi na kufanya kuendesha gari kusichoshe.

Kwa mujibu wa Toyota, Kirobo anaweza kuwa rafiki mzuri wakati wa kuendesha gari kwa kumkumbusha dereva kuendesha kwa tahadhari kwa kusema: “Oh,oh,oh kuwa makini” pale ambapo dereva ataendesha kwa mwendo kasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles