24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAIPONGEZA MUHIMBILI KWA KUANZA KUPANDIKIZA FIGO

WIKI iliyopita Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya India, iliweka historia kwa mara ya kwanza kwa kufanikiwa kupandikiza figo kwa mgonjwa aliyesumbuliwa na maradhi ya figo.

Taarifa ya MNH ilisema upandikizaji huo uliofanywa Novemba 21, mwaka huu chini ya jopo la wataalamu kutoka katika hospitali zote mbili ulifanyika kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 30 baada ya kupewa figo na ndugu yake mwenye umri wa miaka 27.

Kwa mujibu wa Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa MNH, Dk. Onesmo Kissanga, wagonjwa wengine 56 wenye matatizo ya figo nao wako katika foleni ya kusubiria huduma ya upandikizaji figo.

Pia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema upasuaji huo mkubwa ni juhudi zinazofanywa na Serikali katika kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji kupata huduma hiyo nje ya nchi.

Ummy alisema takribani wagonjwa 400 wa figo wanafanyiwa utakatishaji wa damu (renal dialysis) katika vituo mbalimbali vya tiba hapa nchini na asilimia 60 wanaweza kuhitaji huduma ya kupandikiza figo.

Pamoja na mambo mengine, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunaipongeza MNH kwa kuanza kutoa huduma hiyo kwa sababu italeta nafuu kwa wagonjwa kupata matibabu na itaokoa maisha ya wengi.

Kwa sababu kwa mujibu wa Ummy, matibabu nje ya nchi yaliigharimu Serikali Sh milioni 80 hadi 100 kwa mgonjwa mmoja na ilipeleka wagonjwa 35 kwa mwaka, kwa hiyo kuna kiasi kikubwa cha fedha kinaokolewa pindi upasuaji huo ukifanyika hapa nchini.

Mbali na hayo, tunamwomba Ummy aharakishe mchakato wa utungwaji wa sheria ya kuruhusu upandikizaji wa viungo katika mwili wa binadamu ambayo pamoja na mambo mengine itamwezesha mtu kubeba mimba kwa niaba ya mwingine.

Tunaomba mchakato huo uharakishwe kwa sababu hatua ya awali, ilitengenezwa kanuni namba 232 na zilizochapishwa katika gazeti la Serikali na kuwezesha kufanyika kwa upasuaji huo.

Pia tunamwomba Ummy aisimamie vyema kamati ya watu tisa aliyoiteua ili nayo ihakikishe kuwa hakuna biashara ya viungo itakayofanywa katika upandikizaji huo.

Pia tunamwomba Ummy apokee maoni yaliyotolewa na Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru, yanayomshauri kuweka kipengele kinachomruhusu mtu anayetarajiwa kufariki dunia kutoa viungo vyake kwa ajili ya matibabu ya wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles