29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TUMEUA AZIMIO HALALI, TUNAZAA LA KILAGHAI

Na MARKUS MPANGALA,

MIONGONI mwa mambo yanayozungumzwa sana katika siasa za Tanzania, ni hatua ya kulifuta Azimio la Arusha. Kila mwaka tunapoadhimisha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere tunakumbuka Azimio la Arusha.

Na kwa sasa azimio hilo limekuwa simulizi zisizokwisha na kukosa utekelezwaji. Ingawaje Profesa Issa Shivji anaamini kuwa Azimio la Arusha linarejea, lakini jambo moja la msingi hatuwezi kujiambia kwamba tunarejesha pasipokuwa na madhumuni ya kulirejesha.

Azimio la Arusha ni moja ya uongozi bora barani Afrika, hivyo kilichopaswa kufanywa ni marekebisho ya yale yaliyosababisha kasoro, mfano suala la vijiji vya ujamaa. Tulifanikiwa kutongoa njia za kuboresha na kuinua kilimo, lakini hatukuweka misingi ya kuondokana na changamoto ya nini matokeo ya vijiji hivyo.

Kwa mantiki hiyo, kilichotakiwa kufanywa ni kuweka misingi ya vijiji vya ujamaa vya majaribio au kutenga maeneo maalumu ambayo yangelikuwa yanafanya kazi ya kijiji cha ujamaa, huku maeneo mengine yakiendelea na shughuli za kilimo kwa mtindo tofauti, lakini ukiwa na dhana ile ile ya kuhifadhi na kulinda ujamaa.

Bahati mbaya ziliibuka filimbi za uasi dhidi ya ujamaa, hivyo ukijumlisha na kasoro zake, basi ikawa kwamba ujamaa ulifeli, wakati waliofeli ni watu wenyewe waliobuni.

Sera zilizozungumzwa katika vijiji vya ujamaa zilikuwa na nia moja tu ya kuhifadhi uchumi na kuleta maendeleo kwa manufaa ya jamii nzima.

Kwahiyo, pale ambapo tuliona dosari kwenye Azimio la Arusha tulipaswa kuelewa kuwa lazima kufanyike mabadiliko ya msingi ili kuondoa kabisa ukakasi katika azimio hilo. Sasa baada ya kuondoa azimio ambalo liliweka miiko ya uongozi na kuhimiza uongozi bora, tukaamua kuachana nalo na kukubali azimio la kilaghai kabisa la utawala bora.

Kimsingi mipango iliyobuniwa katika utawala bora haikuwa na makusudio yale yaliyowekwa katika uongozi bora. Azimio la Arusha lilihimiza uongozi bora kwa kuweka maadili ya uongozi, lakini kwenye utawala bora tumekuwa tukiwekewa mwongozo wa kupunguza umasikini, kugawa madaraka kwa kufuata jinsia, yaani uwiano, kuanzisha uongozi kulingana na jinsia na mengineyo.

Sasa kwetu kuwa na Azimio la Arusha ambalo ndilo msingi na kanuni za uongozi katika nchi tukaona ni baya zaidi, hivyo ni vyema kuleta azimio la utawala bora ambalo ni sawa na ulaghai bora. Ndani ya utawala bora tukaanza kujiona mbele ya IMF/WB ni watu dhalili tusioweza kufikiri njia za kuongoza nchi yetu. Tukabakia kuwa bendera fuata upepo kwa madai ya sera za mageuzi ya kiuchumi.  

Rafiki yangu Kudakwashe Afrika wa Malawi aliandika maneno machache tu akisema: “As Africans we have our authentic own ways of addressing our own needs. Being different, does not mean that our ways are not right, neither are they to be despised”.

Tafsiri isiyo rasmi: “Sisi Waafrika tunayo njia yetu ya kutatua matatizo yetu. Kuwa tofauti na wengine haimaanishi njia zetu si nzuri”.

Tulikuwa na dhumuni zuri kudhani utawala bora ni njia ya kuweza kufikisha ujumbe na kuinua hali ya maisha ya watu wetu, lakini kosa tulilofanya ni kupuuza misingi yetu na kuchukua mipango isiyoshabihiana na mazingira yetu.

Tukapuuza kuwa hata wenzetu Afrika Kusini waliamua kwa dhati kabisa kuwawezesha wenyeji wa nchi yao ili kujaribu kuvumbua njia za kuinua uchumi. Sisi mageuzi ya kiuchumi tukayapeleka matumaini yetu yote kwenye makaratasi ya IMF/WB.

Kwa mtindo wa sera hizo, tukaanza kuhubiriwa misingi mipya ya demokrasia ya kiliberali, huku MDG (Millenium Development Goal) ikaibuka kama nyenzo ya mageuzi ya uchumi wakati huko tulijiwekea njia ya kukopeshwa kwa riba ya hali ya juu na malimbikizo ya madeni. Bahati mbaya zaidi tukajiona kwamba hatuna njia nyingine ya kufanikisha kukuza uchumi wetu.

Tukajiona kuwa njia zetu za kukuza uchumi ni mbovu, wakati tulizoletewa tukaziona ni dhahabu. Yalikuwa makosa ambayo yamefanyika na tunaendelea kuumizwa nayo kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi miongoni mwa mataifa makubwa.

Badala ya Azimio la Arusha kulifanya kuwa msingi wa maendeleo yetu, tukaamua kuligeuza na kuimba pambio za utawala bora.

Tukasahau kufuata njia tofauti si kosa na lazima tuchukue hilo kama msingi wa kujenga uchumi ama maendeleo ya nchi zetu. Vilevile MDG yenyewe tunafahamu kuwa ni tunda bovu la sera zilizofeli kwa kutojali mazingira halisi ya nchi zinazotoka IMF/WB.

Ni sera hizo ziliwaangamiza Wamalawi na kukumbana na wimbi la njaa baada ya kushauriwa wasizalishe mbegu za mazao, badala yake wanunue kwenye makampuni makubwa ya uuzaji mbegu.

Kama si mshituko uliompata aliyekuwa Rais wa Malawi, Bakili Muluzi, basi lilikuwa janga maridhawa na Wamalawi waliugulia kwa kipindi kirefu kwenye janga la njaa. Malawi ni mfano bora, sababu ndani ya makabati ya IMF/WB wanajua kilichotokea nchini humo.

Afrika hatujawahi kuhitaji utawala bora. Toka awali tulikuwa tunahitaji uongozi bora. Afrika hatukuwahi kuhitaji kupunguza umaskini, tulidhamiria kuondoa umaskini. Wakasema hapana.

Kuanzia sasa fuateni utawala bora na muachane na uongozi bora. Zaidi sana wakasema acheni kuondoa umaskini, ila punguzeni umaskini!

Maneno haya yanaweza kutufumbua macho na kuelewa zaidi kiini cha mkanganyiko na uchumi dhaifu unaopandwa, licha ya matumizi ya sera za IMF/WB. Ni wakati wa kupima endapo tunahitaji uongozi bora au ulaghai wa utawala bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles