KINSHASA, DRCÂ Â Â Â Â Â Â |Â Â Â Â Â Â Â Â
MAKAMU wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mbabe wa kivita, Jean-Pierre Bemba, ameshindwa kupata vigezo ambavyo vingemwezesha kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba 23, mwaka huu.
Kwa mujibu wa majina ya awali yaliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC, CENI, Bemba ni miongoni mwa wagombea sita wa urais waliokuwa wamewasilisha majina yao, lakini wameshindwa kujieleza kinagaubaga katika mahojiano ya saa kadhaa na tume hiyo.
Juni mwaka huu, kiongozi huyo wa zamani wa waasi aliachiliwa huru baada ya mahakama kubatilisha hukumu dhidi yake ya uhalifu wa kivita.
Tume ya Uchaguzi imesema Bemba amezuiwa kuwania kwa sababu alipatikana na hatia ya kuwahonga mashahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Mwanasiasa huyo aliyerejea DR Congo mwanzoni mwa Agosti baada ya kukaa miaka 11 uhamishoni na gerezani, lakini alishinda rufaa yake ya kupinga hukumu aliyowasilisha katika ICC.
Uchaguzi wa mwaka huu utafanikisha kuchaguliwa kwa mrithi wa Rais Joseph Kabila, ambaye muhula wake wa pili na wa mwisho wa kuongoza ulimalizika miaka miwili iliyopita.
Muungano wa chama tawala nchini humo ulimteua waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea wake.
Kulikuwa na jumla ya watu 25 waliotaka kuwania nafasi ya urais, wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Antoine Gizenga na Adolphe Muzito. Wawili hao pia wamekataliwa kuwania.
Vyama vya upinzani vimelalamikia hatua hiyo ya Tume ya Uchaguzi hata kabla ya uamuzi huo kutangazwa rasmi, wakiituhumu serikali ya sasa kwa kujaribu kudhibiti na kuelekeza mchakato wa uchaguzi.
Wagombea waliozuiwa kuwania, akiwamo Bemba, anayetazamwa na wengi kama mgombea atakayetoa ushindani mkali zaidi kwa muungano wa chama tawala, wanaweza kukata rufaa uamuzi huo wa kuondolewa majina yao.
Orodha kamili na ya mwisho ya wagombea inatarajiwa kuchapishwa Septemba, mwaka huu.
CENI imesema wagombea waliokidhi vigezo vya kuwania urais nchini humo ni kama ifuatavyo: Emmanuel Ramazani Shadary, Kikuni Masudi Seth, Mukona Kumbe Kumbe Pierre, Ngoy Ilunga Isidore, Makuta Joseph, Kabamba Noel, Mabaya Kinkiey Mulumba, Freddy Matungulu, Felix Tshisekedi, Allain Shekomba, Radjabu Sombolabo, Kamerhe Vital, Fayulu Martin Bomba, Gabriel Mokia, Basheke Sylvain, Charles Gamena na Mbemba Francis.
Kiongozi mwingine wa upinzani, Moise Katumbi, anayemiliki klabu ya TP Mazembe, alizuiwa kurejea nchini DRC siku ya mwisho ya kuwasilisha nyaraka za kuomba kuwa mgombea wa urais.