25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TULIMPENDA SANA KIKWETE ILA TULIMHITAJI ZAIDI MAGUFULI

NA RAMADHANI MASENGA,

JAKAYA Mrisho Kikwete ni mtu mcheshi sana. Anajali na anawapenda watu. Mnamo Aprili 4, mwaka huu, alipokewa kwa shangwe ndani ya ukumbi wa Bunge wakati alipomsindikiza mkewe, Salma Kikwete, kula kiapo baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge na Rais John Magufuli.

Waliowahi kufanya kazi na Kikwete kwa karibu wanasema ni mtu ambaye hutachoka kukaa naye. Ni mzungumzaji mzuri, pia msikilizaji mzuri na muungwana mno.

Katika miaka kumi ya utawala wake tumeyaona hayo. Alikuwa karibu na kila kundi. Aliwapenda walemavu, watoto, wasanii, wanamichezo, viongozi wa dini na waumini wao, wafanyabiashara na watu kila rika.

Tabia ya Kikwete kama ilivyo kwa mtu yeyote, ilikuwa ina faida upande mmoja na kuumiza upande mwingine kulingana na mamlaka aliyokuwa nayo. Kwa upole wake, wengi walikuwa huru kusema kila kitu. Kwa uungwana wake, alimvumilia kila mtu. Hata wale wasiopaswa kuvumiliwa.

VIONGOZI NA DAWA ZA KULEVYA

Mnamo Juni 5, 2011, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za kumsimika Askofu Mpya wa Pili wa Jimbo Katoliki la Mbinga, mkoani Ruvuma. Ibada ya kuwekwa wakfu Askofu huyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Katika sherehe hizo, Kikwete alisema ana majina ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Alisema wapo wanasiasa, wafanyabiashara maarufu na viongozi wa dini.

Badala ya kuwashughulikia kama ilivyotarajiwa na wengi, kwa upole wake alisema anawaomba waache. Pia aliwataka watu waliokumbwa na kashfa ya EPA kurejesha fedha zote pamoja na kuwapa muda wajirekebishe. Watu wakapigwa na butwaa.

Katika uongozi wake kuna watu wengi walihusishwa na ufisadi. Akiwa rais wa nchi, viongozi kadhaa wakubwa walituhumiwa kuingia mikataba ya kitapeli, huku wengine wakitumiwa kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi. Kwa upole wake, akasema atawashughulikia. Haikuwa hivyo.

HESHIMA YA CCM

Akiwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilisifika kwa kuwafuga mafisadi na wafanyabiashara wenye kila taswira za utata katika jamii. Maelfu ya watu wakapiga kelele mpaka wakakoma. Kikwete hakushtuka.

Baadaye Kikwete alibaini sifa na heshima ya chama chake ikizidi kupotea. Lilikuwa jambo la kawaida kuona mtu akizomewa kwasababu amevaa sare ya CCM.

Upesi akarudisha viongozi makini katika chama kama Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti), Kanali Abdulrahman Kinana (Katibu Mkuu) na Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi) kwa kuwataja wachache. Zoezi la kwanza likawa kuvua gamba, lakini likaishia njiani.

KIKWETE, WASANII NA MICHEZO

Kwa kipindi cha miaka 10 ya Rais Kikwete aliwasaidia sana wasanii. Aliwapenda na kusikiliza vilio vyao, ingawaje baadhi walionekana ‘kumsaliti’ katika kampeni za mwaka 2015 alipokuwa akimnadi John Pombe Magufuli.

Ukweli hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kuwafanya wasanii wajivune kama ilivyo yeye. Wengi tunakumbuka mradi wa kuwasaidia wasanii studio ya kurekodia kazi zao.

Aidha, kwenye michezo pia Kikwete ameacha alama kubwa, mbali na kuamua kuwalipa makocha wa timu za taifa, Marcio Maximo na Itamar Amorim kutoka Brazil.

Ni katika kipindi hiki ndipo timu ya taifa ya soka, ‘Taifa Stars’ ilifuzu kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN). Tulishuhudia ujio wa wachezaji magwiji wa klabu ya Real Madrid wakifanya ziara nchini.

Lengo la kutaka sekta ya michezo isonge mbele lilionekana kwa kila mtu. Alisaidia kila aina ya michezo bila kubagua. Aliajiri kocha wa mpira wa pete (netball), Simone Macknis, kocha wa riadha pamoja na ujenzi wa kituo cha michezo cha Jakaya Kikwete kilichopo Dar es Salaam.

Wasanii na wanamichezo wote walialikwa Ikulu kutiwa moyo na hamasa kila kukicha.

Aliweza kumsaidia mwanamuziki mahiri nchini, Rehema Chalamila “Ray C’ kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Hayo yalimfanya Kikwete apendwe mno. Tabia yake ya kumsikiliza kila mtu, subira na uvumilivu ni vitu ambayo daima vitabaki katika akili za Watanzania na dunia.

KIU YA MABADILIKO

Uungwana wake ulikwenda sambamba na kuwachekea watu waliofaa kuchukiwa, hali iliyozamisha nchi na kujenga matabaka ya haraka. Ndani ya miaka kumi, wajinga wachache walitumia hali hiyo kutajirika kwa haraka.

Ndani ya uongozi wake, miungu watu waliongezeka, heshima ikashuka na rushwa ikatamalaki. Ilifikia hatua mtu akikwambia unanijua mimi, unaanza kutetemeka na kuomba msamaha.

Heshima ya utu ilipotea na umungu wa fedha ukashika usukani. Kwa mambo hayo, wazalendo kadhaa waliona japo wanampenda sana, ila bora arudi kijijini Msoga akacheze na wajukuu.

Baada ya kufaidi upole na uungwana wake watu walitaka mabadiliko. Japo wengi walioimba wimbo wa mabadiliko hawakujua ni mabadiliko ya namna gani waliyokuwa wakiyataka, ila baadhi walijipambanua kwa kujua nini wanataka.

Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, aliwahi kusema nchi hii ilipofikia inahitaji rais mkali. Asiyecheka na wajinga wanaofanya rasilimali za taifa ni zao, wala kucheka na mafisadi pamoja na wahujumu uchumi.

Mnamo Mei 27, 2015, Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, katika mahojiano yake na gazeti moja la kila wiki hapa nchini alisema Tanzania kwa sasa inahitaji rais mwenye uamuzi mgumu.

“We need someone like a dictator person. Anayetafuta majibu kwa haraka. Hii ni kwa sababu, mfumo wa sasa hauleti majibu stahili kwa wakati. Sasa tuombe Mungu labda tutapata viongozi wenye zero tolerances ya ufisadi, rushwa na mambo mengine mengi. Hata kwenye utendaji wa Serikali mambo kwa sasa si mazuri hata kidogo. Mpaka ukiona Rais naye analalamika ujue kwamba system is not delivered (mfumo haujibu),” alibainisha Msuya katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake, Dar es Salaam.

Mtazamo wa waziri huyo ulikuwa na maana  nchi ilipofikia ilihitaji kiongozi ambaye hataki kuyumbishwa wala kubabaishwa na kelele za kisiasa.

Wengi walifikiri watu wa namna hiyo hawapo. Wengi walipima watu kwa umaarufu wao na kusema hawafai kwa sababu kwa namna moja ama nyingine walihusika na ufisadi wa hapa ama pale.

Aidha, wengine waliamini Dk. Slaa anaweza kazi ya kuinyoosha nchi. Wengine walisema John Magufuli anaiweza ila hawakuwa na uhakika kama chama chake kingempa nafasi.

Mbali na Magufuli kuonekana kutokuwa na umaarufu mkubwa katika chama chake, ila pia hakuonekana kuwa na mbwembwe katika harakati zake za kuchukua fomu mpaka kutafuta wadhamini.

Ila miujiza ikatokea. CCM ikamchagua John Magufuli na wananchi wakamkubali. Sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikwete aliishia kusema ana majina ya wauza madawa ya kulevya, lakini utawala wa Serikali ya Magufuli tunaona watu wakishughulikiwa ipasavyo. Kikwete alisema watu inabidi wajitathimini, Magufuli anawachunguza na akiona hawafai anawafukuza.

Baada ya miaka mingi ya vilio vya ufisadi na watu kutokuwa wawajibikaji katika maeneo yao ya kazi, sasa wimbo huu unaelekea kupoteza umaarufu. Zamani ukiangalia ama ukifuatilia habari za bungeni, ungekuta wabunge wa upinzani na wa CCM wakipiga kelele juu ya ufisadi wa mambo fulani. Sasa hali ni tofauti.

Wachache wanaotaka kulazimisha kuonekana kuna ufisadi mkubwa ama uzembe unaolelewa na serikali, wanaishia kuumbuliwa.

Mfano ni suala la ununuzi wa ndege kubwa ya abiria za Bombardier, ambayo Mbunge wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe, alisema serikali inanunua ndege chakavu na kwa bei kubwa.

Sasa ukweli umejulikana kuwa ni ndege mpya na inanunuliwa kwa bei rafiki.

Labda kuna mengi tunammisi Kikwete. Ila pia kuna mengi zaidi tulimhitaji Magufuli aje kuyafanya. Uongozi wa Kikwele kuna mengi ya maana umefanya katika taifa hili.

ZAMA ZA MAGUFULI

Uongozi wa Magufuli una mengi unahitajika kufanya kuweka sawa misingi ya taifa hili ambayo kwa miaka takribani 20 ilikuwa ikichezewa.

Sasa japo kwa mbali tunaweza kuhisi harufu ya utu na heshima. Tunaweza kunusa harufu ya maendeleo ya kweli na si ujanja ujanja. Sasa maendeleo yetu yatakoma kupimwa kwa wingi wa magari barabarani hata kama magari hayo yanamilikiwa na watu kutoka katika familia moja.

Kwa mbali wale mafisadi sasa wanageuka kuwa waaminifu, bila shaka wakihofia kushtakiwa Mahakama ya uhujumu uchumi. Wale miungu watu sasa wanaanza kuwa viumbe wenye kujitambua na kujua kuna Mungu na wao ni viumbe wenye kufaa kuabudu na si kuabudiwa. Binafsi ninammisi sana Kikwete, ila nashukuru ujio wa John Magufuli.

[email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles