21.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 16, 2021

KUKATAZA SIASA NI KURUDISHA NYUMA MAENDELEO

Baadhi ya wanachama wa chama cha UKAWA wakiwa katika moja ya mikutano yao

 

 

Na Balinagwe Mwambungu,

VYAMA vya siasa vimekatazwa kufanya ‘siasa’ Tanzania. Ni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu. Lakini hapana shaka, mamlaka ililitafakari jambo hili na kutambua kwamba siasa ni sehemu ya mpangilio wa maisha ya Watanzania na ikafafanuliwa kwamba kilichokatwa ni mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Ikaelezwa kwamba viongozi wa kuchaguliwa, wabunge, madiwani, wanaruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao.

Ukweli ni kwamba hakuna anayeweza kukataza kufanya siasa. Siasa ndio chachu ya maendeleo. Ni kwenye siasa tu ambako watu hugonganisha fikra na mawazo na siasa inaleta changamoto nyingi; kwa maana siasa haifanywi na wanasisa tu, bali ni makubaliano ya jamii ambayo hayajaandikwa popote.

Siasa ni ya watu kuanzia ngazi ya familia hadi jumuiya nzima ya watu waishio na kufanya kazi pamoja. Mtu anayeishi peke yake kisiwani ambako hakuna watu, hawezi kufanya siasa au akawa mwanasiasa. Atafanya sehemu moja tu ya siasa ambayo ni kujilinda.

Kuna dhana nyingi kuhusu maana ya siasa na wasomi nguli duniani wametoa maana tofauti ya neno siasa. Lakini nakubaliana na wale wanaosema kuwa siasa ni mpangilio wa maisha ya watu (si mtu) na utawala wao. Kwa hiyo jamii mbalimbali zimeifanya siasa kuwa sehemu ya tamaduni zao za namna ya kuendesha utawala wao, mambo ya kijamii ikiwa ni pamoja na mahusiano ndani ya jamii na masuala ya kiuchumi, ulinzi na usalama.

Ni kwa mantiki hiyo kwamba hakuna mtu anayeweza kupiga marufuku siasa na wala haiwezekani siasa isifanyike katika jamii. Kinachoweza kufanyika ni kiongozi kuingilia mpangilio huo wa maisha kwa punguza baadhi ya mambo ambayo jamii ilijipangia na kuzoeleka kuwa ni sehemu ya mpangilio wa kidemokrasia ambamo kila mtu ni mshiriki.

Lakini mambo kama haya ya makatazo, huwa yanatendeka kote duniani na hasa katika nchi zinazoendelea.

Kwa mfano, mtu anatafuta madaraka ya kutaka kuendesha mambo ya utawala. Inabidi atumie ushawishi mkubwa kwa jamii, ili akubalike kwamba mambo anayokusudia kuyafanya ni kwa faida ya jamii nzima. Lakini imetokea katika historia, mtu huyo akishachaguliwa, anageuka na kuacha njia za kidemokrasia na kuanza kuendesha nchi bila kufuata misingi ya utawala, yaani kuongoza kwa kutumia katiba, sheria, kanuni na taratibu zilizozoeleka katika jamii husika.

Madikteta hawaibuki hivi hivi. Wanapewa madaraka (dola) kutokana na ushawishi wao mkubwa katika jamii, tena wanachaguliwa kwa kura nyingi, watu wakiamini kwamba akipewa dola atafanya kama alivyoahidi. Kama waliingia madarakani kwa kuuza sera za vyama vyao, huziweka pembeni. Wakishashika dola huanza polepole kuminya uhuru wa watu ambao anaona wanaweza kumwondoa madarakani. Sehemu nyingine watu kama hao (wapinzani), huuliwa au hupotezwa, hufunguliwa mashtaka ya uhaini na kufungwa. Wengine hupewa vitisho na kunyimwa haki ya kupata kipato, tunao mfano wa nchi moja jirani ambako kiongozi wa chama pinzani amekamatwa zaidi ya mara 30 na kufunguliwa mashtaka. Anatumia muda wake mwingi mahakamani.

Wafalme au masultani hawawekwi katika fungu la madikteta kwa kuwa ni watawala wa jadi. Malkia wa Uingereza kwa mfano, huwezi kumlinganisha mtawala wa kuchaguliwa ambaye anatawala kwa muda fulani tu. Kwanza Uingereza huendeshwa kwa mila, desturi na taratibu za Waingreza; hawana katiba.

Wafalme na masultani wanapata nafasi ya kutawala si kwa njia ya kuchaguliwa. Ufalme na usultani ni uongozi wa kuzaliwa, wanarithi kutoka kwa koo zao, kwa hiyo uongozi wao hauna ukomo. Mtu anapewa uongozi mradi tu ni damu ya kifalme, hata kama hana sifa za kuwa kiongozi. Hii ilikuwa sababu mojawapo ya Mwalimu Julius Nyerere, kuufuta uchifu mara baada ya Uhuru wa Tanganyika (1961), kwa sababu chifu alikuwa mwenye madaraka makubwa sana, chochote anachoamua lazima kitekelezwe. Alikuwa hachaguliwi na alikuwa hawajibiki wala kuhojiwa na yeyote; kauli yake ilikuwa ni amri.

Lakini watu wanaochaguliwa kwa njia ya kura, huwa wanaficha mambo yao fulani ambayo wanawaaminisha wananchi kwamba yakitekelezwa, yataleta faida kwao (binafsi) na kwa wananchi. Hivyo husimama majukwaani na kunadi sera zao ili wapewe nguvu ya dola wawezeshe kutimiza malengo yao.

Katika nchi za kidemokrasia, watu wote wanapaswa kuchangia maamuzi; nani awe kiongozi wao na akishachaguliwa akatekeleze yale aliyoyaahidi, zingine zinakuwa ahadi hewa.

Wasomi wanasema hapa ndipo unapofanyika udanganyifu wa kisiasa. Mtu huyo  akishashika dola, huwageuka wananchi na kufanya anayotaka yeye. Hataki kuulizwa kwanini anafanya hayo, hataki kupingwa, anajivisha madaraka yasiyo na ukomo, anaweza hata akasigina au akaamuru Katiba ya nchi ibadilishwe ili aendelee kushika dola na kufanya anavyotaka, kwa vile amewajengea hofu wananchi waliompa madaraka, anaminya haki, uhuru wa kusema au kushiriki katika kufanya maamuzi.

Lakini pia wanaolilia kwenda Ikulu, ni wepesi wa kukosoa na kupinga mambo ambayo hawakubaliani nayo. Kwa kawaida huwa hawasemi kwamba wanataka washike hatamu, ili waweze kugawa rasilimali za nchi kwa uwiano. Mwalimu Nyerere alisema Ikulu hakuna biashara, kwa sababu yeye hakuamini katika dhana ya kuendesha nchi kwa kauli ya mtu mmoja, ingawaje wafuasi walitaka kumwaminisha kwamba ndiye pekee aliyekuwa anajua wananchi wanataka nini; ndio msingi wa ‘zidumu fikra za Mwenyekiti.’

Mwalimu alitaka kuendesha utawala wa umma, alijenga misingi ya kujiongoza kwa kufuata malengo ya namna ya kujiletea maendeleo ya pamoja (hakuamini kwamba mtu anaweza kuwaletea maendeleo) kwa kufuata misingi ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kama ilivyokuwa imeanishwa kwenye Azimio la Arusha.

Lakini baada ya Azimio la Arusha kufutwa, Ikulu ambayo Mwalimu alisema ni mahali patakatifu, ikageuka kuwa mahali pa biashara kubwa na ndogo. Ikulu ndio inayogawa nani apewe nini, kwanini, kwa namna gani na kwa wakati gani.

Kinachofanyika bungeni hivi sasa (kipindi cha Bajeti), ni utekelezaji wa dhana hiyo; kugawa rasilimali za nchi. Kuna sekta zinazopendelewa na sekta zinazopewa fedha kiduchu. Mawaziri ni wawakilishi tu wa Ikulu ambako ndiko kuna mamlaka ya kusema nani apewe nini, kwa nini, kwa wakati gani na apeweje.

Wabunge wakidharauliwa au kunyamazishwa, dhana ya demokrasia shirikishi aliyopigania Mwalim itapotea. Ndio maana wananchi wanalilia Bunge ‘live’ (ni sehemu ya demokrasia shirikishi) ili waone na kusikia mambo yanayosemwa na wawakilishi wao.

Uwamuzi wa kuendesha Bunge bubu ni kinyume cha misingi wa demokrasia shirikishi, demokrasia ambayo imekuwa kichocheo cha wananchi kuamua mambo ya kufanya kwa pamoja kwa maendeleo yao, maana watakuwa wamefuatilia mijadala na kuridhika kwamba hawatapata mgao wa nani kapewa nini kwa kuwa huenda mgao hautakidhi mahitaji yao. Kwa hiyo wanaamua kujipanga kutumia kile walichopewa na kama ni kiduchu watahamasishana nini cha kufanya.

Bunge ‘live’ liliwawezesha wananchi kusikia moja kwa moja majibu ya mawaziri na kuyafanyia kazi. Lakini Bunge la sasa limepooza, halina mvuto. Mtu mmoja anasema Bunge la sasa ni kama mvulana aliyesimama gizani kisha  kumkonyeza msichana.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
161,801FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles