KESHO Jumapili Aprili 16, 2017 Wakristo duniani kote wanasherehekea Sikukuu ya Pasaka. Ni siku yenye maana sana kwa Wakristo kwani hukumbuka siku ambayo Yesu Kristo Masihi alifufuka.
Kwa sisi wazee wa Swaggaz, mambo ni mperampera, kula bata na starehe kwa sana. Wengine ndiyo watapotelea baa kwa siku mbili ndipo waonekane majumbani mwao.
Kwa nafasi hii nimeona siyo vibaya angalau kidogo tujue maana ya sikukuu hii ili hata tunaposherehekea tuwe tunajua tunachokisherehekea.
Kwa mujibu wa Biblia tunaelezwa kuwa Yesu alikuwa amemaliza tu kuadhimisha Pasaka pamoja na mitume wake alipoanzisha mlo wa pekee ambao ungekuwa mfano wa jinsi kifo chake kingepaswa kukumbukwa.
Hiyo ndiyo Sakramenti ya Meza ya Bwana ambayo Yesu mwenyewe alisisitiza: “Fanyeni hivi kila mlapo kwa ukumbusho wangu,” wakati akimega mkate na kisha akasema: “Fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu,” alipotwaa kikombe.
Siku hii inapaswa kuadhimishwa kwa njia ya kutafakari kuhusu mambo ambayo Yesu ametufanyia. Pamoja na kujifunza namna ya kuthamini kifo chake.
Licha ya maandiko kutuelekeza namna ya kuadhimisha Pasaka lakini wengi wetu tumekuwa tukifanya kinyume na maagizo ya vitabu hivyo kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda watu wamekuwa wakisheherekea siku hii kwa namna nyingine au unaweza kusema isivyopendeza machoni.
Utakubaliana nami kuwa wengi wamekuwa wakienenda kinyume na siku hii kwa kuigeuza kama ya kufanya dhambi, ufuska na uchafu wa kila aina licha ya ukweli kuwa siyo makusudi ya kuwepo kwa sikukuu hii.
Achana na mambo yasiyofaa. Ili Pasaka iwe na maana kwako, wakumbuke wahitaji. Wasaidie ndugu zako wasiojiweza ili waweze kufurahia siku hii kama wewe.
Baadhi ya watu wamejihalalishia siku hii na siku nyingine za sikukuu kama sehemu ya kufanya maovu na maasi ikiwamo kujishughulisha na anasa za ulimwengu huu.
Hata kwa upande wa makundi ya vijana ambayo kwao kutoka imekuwa ni nadra kutokana na taratibu ngumu ambazo zimewekwa majumbani mwao na wazazi wao wamekuwa wakitumia mwanya wa sikukuu kujiingiza katika kufanya mambo yasiyopendeza.
Hivyo tutumie siku hii ya kufufuka kwa Yesu Kristo katika kuitafakari Biblia namna inavyotuagiza. Swaggaz linawatakia Wakristo wote Pasaka njema. Hakikisha kila kitu unafanya kwa kiasi.