23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

BADO NAMKUMBUKA MSHKAJI WANGU KANUMBA!

Na JOSEPH SHALUWA

MIAKA mitano imekatika sasa tangu mkali wa sinema za Kibongo, Steven Kanumba afariki dunia. Marehemu Kanumba alifariki Aprili 7 na kuzikwa Aprili 10, 2012 katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Tasnia ya filamu za Kibongo bila shaka bado inamkumbuka shujaa huyu ambaye alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupaisha filamu zetu katika medali za kimataifa.

Nimeshaandika mengi kuhusu Kanumba. Niliandika habari za kumhusu akiwa mzima na hata alipoondoka katika ulimwengu huu.

Lakini kila ninapotazama namna soko la filamu zetu linavyozidi kudidimia siku hadi siku, nashindwa kumsahau shujaa huyu. Katika mwezi huu ambao alifariki dunia miaka mitano iliyopita, nimemkumbuka zaidi.

Namkumbuka Kanumba kama staa wa ukweli, asiye na majivuno, ambaye alikuwa na kiu ya kupaa kimataifa. Kanumba ambaye alikuwa na uthubutu wa kufanya chochote ili azidi kuwa juu yeye mwenyewe, tasnia na hata nchi yake.

 

FROM ZERO TO HERO

Najivunia kumfahamu Kanumba wakati akianza kupata umaarufu wa kazi zake, lakini akiwa hana mafanikio makubwa. Akiwa anapanda daladala. Akitembea kwa miguu, hadi alipokuwa katika mafanikio makubwa.

Nilikutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 2005, nikiwa kinda katika uandishi wa habari za burudani. Wakati huo nilikuwa mwandishi wa burudani, gazeti la Bingwa.

Mhariri wa Habari wa Bingwa, wakati huo Petter Mwendapole ndiye aliyeniagiza kufuatilia makala ya Kanumba. Nilipata namba yake kutoka kwa mwigizaji mwenzake, Simon Simalenga ‘Dimera’ ambaye kwa sasa ni Afisa Uhusiano wa Clouds Media.

Nilikutana naye baada ya kikao chao (Kaole Sanaa Group), kilichofanyika Travertine Hotel, Magomeni. Hiyo ilikuwa ni baada ya vuguvugu la kusimamishwa kuonyesha michezo yao katika Runinga ya ITV.

Baada ya kikao chao, tulikaa kando, tukafanya mahojiano ambayo baadaye yalitoka kwenye Jarida la Jungu Kuu, ndani ya Gazeti la Bingwa, lililotoka siku ya Jumamosi.

Ni Kanumba ndiye aliyenikutanisha na msanii Vincent Kigosi ‘Ray’ na kunitambulisha kwake. Huo ukawa mwanzo wa kuwafahamu wasanii hao wawili, waliopata kuwa marafiki wakubwa.

Kutoka kutoka kwa makala yake ambayo ilikuwa na maswali na majibu iliyochukua kurasa zote nne za jarida hilo, tukatokea kuwa marafiki wakubwa kihabari. Akawa chanzo changu, lakini tukiwa na uswahiba.

 

USWAHIBA, UADUI

Sikukaa sana Bingwa, maana sikuwa nimeajiriwa wakati huo. Nilikuwa nikifanya kazi mwandishi wa kujitegemea. Nilipopata nafasi ya ajira gazeti la Mseto, nikaenda. Lilikuwa gazeti la michezo na burudani, nikiwa na mhariri Dennis Fussi.

Nilimjulisha Kanumba, Ray na wasanii wengine marafiki kuhusu kuhamia kwangu pale. Kanumba akaendelea kunipa ushirikiano mkubwa. Ukweli alitokea kuniamini. Akitaka jambo lake liripotiwe, basi alinitafuta mimi.

Miezi kadhaa mbele, Novemba, 2006 nikahamia katika Kampuni ya Global Publishers, akaendelea kuwa mtu wangu wa karibu kihabari.

Kwa bahati mbaya, Kanumba hakupenda sana kuandikwa magazetini, na kama ikitokea akiandikwa, alipenda kuandikwa kwa mazuri zaidi. Ndivyo tabia ya binadamu wote ilivyo.

Lakini alikuwa mjanja sana, hakuwa mzalisha habari mbaya. Alijua namna ya kuishi kwenye jamii ili asiharibu jina lake. Lakini kuna wakati nililazimika kama mwandishi kuweka uswahiba pembeni na kuandika habari zisizofurahisha.

Jambo muhimu nililofanya ilikuwa ni kumpa haki ya kuzungumza. Nilifanya hivyo pale ambapo kulikuwa na habari ambayo aliizalisha na haikwepeki. Nilikuwa napenda kumtania: “… kaka hata kama tusipoandika sisi, itaandikwa na wengine, funguka tu.”

Alikuwa akinishirikisha baadhi ya mambo yake, huku akinieleza wazi kuwa siyo habari (off-record) na niiache palepale. Nilitii.

Siku ya siku, niliandika makala moja kwenye moja ya safu zangu nikieleza matatizo ya Bongo Muvi, nikataja mapungufu niliyoyaona kwa mtazamo wangu, huku nikieleza matatizo yake kitaaluma kwa maoni yangu. Ukawa mtafaruku mkubwa.

Mimi niliyekuwa rafiki yake, ambaye aliweza kunieleza chochote, ambaye angeweza kuongea na mimi tu kuhusu habari fulani, tukawa hatuongei tena. Hapokei simu, hajibu meseji wala hanipi mialiko ya kihabari.

Bahati nzuri, miezi kadhaa mbele tulikutana ofisini kwake (Kanumba The Great Film Company), Sinza – Meeda. Tuliongea mpaka usiku, tukacheka pamoja na kuagana.

Nakumbuka nilimtania,”Kaka una kila kitu, umeshafanikiwa sasa. Hutembei kwa miguu kama zamani, unayo kampuni yako, unasubiri nini kuoa?”

Alicheka sana, kisha akanijibu: “Mimi bado bado bwana, lakini kwanini wewe unayetuandikia makala za uhusiano hutaki kuoa hadi sasa?” Tukacheka wote. Tukaagana.

 

  

KWENU BONGO MUVI

Namkumbuka Kanumba, msanii aliyekuwa busy muda mwingi. Ni muda gani wa Kanumba haukuwa na kazi? Alipanga ratiba yake sawasawa.

Nakumbuka kati ya matukio mengi yaliyodhihirisha kuwa yeye alikuwa busy, nilimtembea ofisini kwake Upanga (wakati huo akiwa Game 1st Quality), nilimkuta akiwa anafanya mambo matatu kwa wakati mmoja.

Mezani alikuwa na script, mkononi sahani ya chakula na wakati huohuo anatazama sinema moja ya Kinigeria. Ni siku hiyo, Kanumba alinionyesha gari lake la kwanza kumiliki aina ya Toyota Starlet.

Nawasihi wasanii na wadau wa filamu za Kibongo, tuachane na maneno. Tuacheni visingizio, tufanye kazi. Tuangalie tupojipojikwaa ili tujisahihishe.

Msemo ulionea mitaani hivi sasa kuwa Kanumba ameondoka na Bongo Muvi yake, siuungi mkono. Ni vile tu, hakuna aliyesimama na kuamua kuiga angalau hata nusu ya yale ya Kanumba katika juhudi za kupeleka mbele filamu zetu.

Wapo wachache wanaojaribu, lakini bado. Uzuri tatizo linajulikana. Limeshasemwa na wadau wengi, hata mimi nimelisema mara kadhaa, lakini mnafumbia macho.

Tatizo kuu ni hadithi, mengine yanarekebishika. Hii ndiyo sababu namkumbuka sana mshikaji wangu Steven Kanumba. Atabaki kuwa msanii shujaa kwa taifa hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles