24.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tuhuma za rushwa zazidi kuwagombanisha DC, mfanyabiashara

>>Mfanyabiashara atoa ushahidi wa CCTV akihojiwa Takukuru kwa saa tano, ni siku moja baada kumtuhumu DC Sabaya katika kikao cha TRA kutaka rushwa kwa nguvu, mwenyewe adai hawezi kujibu upuuzi

Upendo Mosha na Safina Sarwatt-Moshi

SAKATA la Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya kudaiwa kulazimisha mfanyabiashara wa utalii, Cathberty Swai, kumpa rushwa kwa nguvu, limechukua sura mpya.

Mfanyabiashara huyo amehojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa zaidi ya saa tano  na kuwapa ushahidi wake.

Pia ameonesha video ya CCTV, ikionesha Sabaya akivamia hoteli yake ya kitalii ya Weruweru River Lodge saa 10 afajiri akiwa na walinzi wake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za kampuni yake ya Ahsante Tours zilizopo mjini Moshi, Swai alisema baada ya kuweka tuhuma za rushwa za Sabaya, aliitwa na kuhojiwa Takukuru kwa zaidi ya saa tano.

“Baada ya kusambaa kwa taarifa zangu za kumtuhumu  Mheshimiwa Sabaya kwa unyanyasaji na kutaka fedha kwa nguvu kutoka kwangu zaidi ya Sh milioni 10, jana (juzi) nilishinda Takukuru kwa mahojiano na baada ya hapo nilitoa ushahidi juu za mambo niliyomtuhumu,” alisema.

Kutokana na kukabidhi ushahidi huo, alisema hatoweza kuuweka wazi kwenye vyombo vya habari kwa kuwa tayari unafanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, Swai alionesha waandishi wa habari video ya CCTV ikimwonyesha Sabaya akiingia katika hoteli yake majira ya saa 10 alfajiri.

Katika video hiyo ya dakika 45, Sabaya aliyekuwa ameambatana na watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni walinzi wake, alionekana kulumbana na mtu wa mapokezi katika hoteli hiyo na Swai alidai kuwa alikuwa akilazimisha kuamshwa mmoja wa wageni waliolala hapo.

Sabaya ambaye juzi alikanusha tuhuma hizo, alionekana tena kurudi hotelini hapo saa tano asubuhi, lakini bado hakufanikiwa kuonana na mtu aliyemtaka.

Swai akizungumzia usalama wake baada ya tuhuma zake kwa Sabaya, alidai tangu aziwasilishe amekuwa akiishi kwa wasiwasi na kushindwa kufika katika hoteli yake.

“Toka habari hizi zisambae nina wasiwasi juu ya usalama wangu, imefika hatua hata kwangu ninapoishi ninapaogopa,” alisema.

Alisema kutokana na kuhofia usalama wake, aliomba ulinzi kwa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro na alipatiwa.

Swai alidai pia Sabaya alimlazimisha kuandika barua ya kuomba msamaha, kwamba anaendesha shughuli za michezo ya nyoka kinyume cha taratibu jambo ambalo alilifanya licha ya kuwa ana vibali vyote.

Kuhusu shamba ambalo juzi Sabaya alisema analimiliki kinyume na sheria baada ya kulipora kwa wananchi, Swai alisema eneo hilo analimiliki kihalali na tuhuma za kuwapora wananchi 15 si za kweli.

“Shamba hili nilinunua kihalali bila kificho na kumbukumbu zipo katika ofisi za kijiji, ninalimiliki kwa zaidi ya miaka nane na ninachojua kijiji walinipa kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na kuanzishwa zoo (bustani ya wanyama),” alisema.

Alisema yupo tayari kuongozana na maofisa ardhi hadi eneo hilo na kutoa uthibitisho wa uhalali wa umiliki wake, na kwamba baadhi ya wananchi wanaolalamika ni waliopo ndani ya mita 30 katika bonde la Mto Kikavu.

“Jana (juzi) DC akiongozana na wananchi na Kamati ya Ulinzi na Usalama walifika katika eneo hilo na kufanya uharibifu mkubwa wa kuvunja banda na kuchukua baadhi mali zangu,” alidai.

Alidai chimbuko la madai hayo ya Mkuu wa Wilaya ni kutokana na jazba na hasira kufuatia tuhuma alizotoa juu yake.

MTANZANIA ilipomtafuta Sabaya kujibu tuhuma zinazomkabili, ikiwemo kuvamia hoteli ya mfanyabiashara huyo, alisema hawezi kuzungumza masuala ya kipuuzi na ameshafunga mjadala huo.

“Mwandishi nipo msibani na siwezi kuzungumza mambo ya kipuuzi yanayoendelea kwenye mitandao, nimeshafunga mjadala, sitaki kuzungumza tena,” alisema.

Hata hivyo, alipotafutwa Kamanda wa Polisi kuzungumza suala la kupeleka ulinzi katika hoteli hiyo, hakupatikana kutokana na kutokuwepo ofisini na simu zake alivyopigiwa ziliita bila kupokewa.

Akitoa tuhuma kwenye mkutano wa TRA, Swai alidai licha ya kulipa kodi serikalini ambayo kwa mwaka huwa analipa Sh milioni 148, lakini amekuwa akipokea vitisho na manyanyaso kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya na kumlazimisha kumpa fedha.

“Amekuwa akija usiku hotelini na ile ni hoteli ya kitalii na alipomkuta meneja na akimuuliza maswali akashindwa kumjibu maana siyo kazi yake, alimchukua na kumuweka ndani na kumtoa asubuhi, nilipomfuata kufahamu shida nini, alisema anataka Sh milioni tano, ametumwa na anafanya kazi ya Serikali,” alidai.

Swai alidai kuwa Sabaya alimweleza kwamba anaweza kuitafsiri kauli hiyo kama ni sawa na ya mkuu mmoja wa mkoa nchini ama rushwa.

ÔÇťAlisema anahitaji hiyo fedha na anaripoti moja kwa moja juu. Nilimpa milioni mbili, lakini bado alininyanyasa, na nilimfuata mfanyabiashara mwenzangu kuomba ushauri, alinishauri nimpe tu hizo fedha na kuniambia nikicheza na mjinga atanipasua jicho,” alidai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles