25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: Absalom Kibanda amuasa JPM kuukataa unyonge wa historia

Na Absalom Kibanda

NILITAMANI kukamilisha mfululizo wa makala zangu za ushauri kwa Rais Dk. John Magufuli al maarufu JPM ambao kwa makusudi na kwa sababu mahususi niliuunganisha kwa muhtasari tu na rejea ya safari ya miaka 10 ya urais wa Benjamina Mkapa (1995 -2005).

Ni jambo la bahati mbaya kwamba, matamanio yao ya kukomesha mjadala huu leo umegonga mwamba na hivyo kunifanya nilazimike kusogea mbele hatua moja au mbili zaidi kukamilisha kile ambacho nilikikusudia.

Sina sababu ya kueleza kwa mara nyingine tena ni kwa nini basi niliamua kumtumia Rais mstaafu Mkapa kama rejea ya kumuasa, Rais John Magufuli ambaye sasa hivi ndiye jemedari mkuu na raia nambari wani wa Tanzania.

Kwa ufupi, itoshe tu kueleza katika makala yangu leo kwamba, baba wa siasa wa Rais Magufuli ni Mkapa ambaye mwaka 1995 alipoingia Ikulu kwa mara ya kwanza ndiye aliyemuibua kutoka miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na akamteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Ni wazi kwamba, JPM anazidi kutambua kidogo kidogo uzito wa majukumu ya kuwa mkuu wa nchi tajiri kirasilimali ambayo kwa bahati mbaya idadi kubwa ya wananchi wake wanaokadiriwa kufikia milioni 55 sasa bado wanaishi katika maisha ya ufukara na shida.

Mara kadhaa, kwa maneno yake ya kujirudia rudia ambayo kwa maoni yangu yanabeba ukakasi na wakati mwingine taswira hasi, JPM amekuwa akijitanabahisha kwa namna ile ile ambayo wamekuwa wakifanya watangulizi wake kwamba yeye ni ‘Rais wa wanyonge’.

Ninasema ni maneno yenye ukakasi kwa sababu, neno ‘unyonge’ ni moja ya misamiati kongwe zaidi katika taifa hili ambayo ilianza kutumiwa kama njia ya kuukataa ukoloni zaidi ya miaka 55 iliyopita.

Japo ni kweli bado Tanzania kwa viwango halisi vya maisha ya walio wengi ni taifa la watu maskini, kuendelea kukiri umaskini au unyonge ni mwendelezo ule ule wa woga ambao JPM kwa kujua au pasipo kujua anaweza akawa ameurithi kimazoea kwa Mkapa na pengine kwa marais wengine waliotangulia

Alikuwa ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Tanzania ambaye katika maandishi yake ya mwanzoni ambayo baadaye yaliingizwa hadi katika maandiko ya kisera alisema:

“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha na ni unyonge wetu ndiyo unafanya tuonewe. Sasa ni lazima tufanye mapinduzi, mapinduzi ya kuondoa UNYONGE wetu ili tusionewe tena na tusinyonywe tena,” mwisho wa kunukuu

Maneno hayo si tu kwamba yaliishia kusemwa na Baba wa Taifa, bali yaliingizwa na yakawa ndiyo mwongozo halisi wa mwelekeo wa taifa na miaka sita tu baada ya uhuru lilipozaliwa Azimio la Arusha mwaka 1967, safari rasmi ya kuukataa unyonge ikatangazwa.

Miaka 10 baadaye, yaani mwaka 1977, taifa likatangaziwa rasmi kuingia katika hatua kamili ya kimapinduzi dhidi ya unyonge tuliotangaza kuushinda mwaka 1961 kwa Tanganyika na mwaka 1964 kwa Zanzibar kabla ya kuja na azimio dhidi ya unyonge mwaka 1967 na baadaye mapinduzi ya kifikra ya mwaka 1977 yaliyozaa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ni jambo la bahati mbaya kwamba miaka takriban 57 baadaye, taifa ambalo lilitangaza vita dhidi ya unyonge na kujigamba kuchukua hatua za kimapinduzi kuukabili unyonge huo, kiongozi wake mkuu bado anajitambulisha kwamba yeye ni ‘Rais wa wanyonge’.

Katika hili, kila Mtanzania na si rais peke yake anapaswa kujiuliza ni wapi tulipokwama hata tukasababisha laana ya unyonge badala ya kumalizwa na kutokomea imegeuka kuwa ajenda ya ‘kumpatanisha’ au ‘kumuunganisha Rais na mamilioni ya wananchi anaowaongoza.

Katika hili, kosa si la Rais JPM anayejitambulisha na kujipatanisha na kundi la wanyonge walio wengi bali taifa ambalo kwa miaka nenda, miaka rejea limekuwa likiona fahari kuishi katika ufukara usiostahili.

Miaka minne iliyopita, mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wakati nikiwa katika pitapita zangu za kudadisi juu ya mustakabali wa taifa baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza muda wake, nilikutana na watu waliokuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM na serikali yake.

Niliwasikia watu hao ambao miongoni mwao walikuwapo washauri na wasaidizi wa karibu wa Rais Kikwete wakitafakari namna ambavyo taifa lilikuwa likihitaji kumpata rais mkali ambaye pia atakuwa na uwezo thabiti wa kuchukua maamuzi magumu, kuyasimamia na kuyatekeleza.

mara moja mbili au tatu kwamba, kwa hali ambayo taifa lilikuwa limefikia, alikuwa anahitajika rais ambaye atakuwa tayari kubeba lawama za kuchukua maamuzi pasipo kuangalia mtu usoni.

Makada hao wa CCM walifikia hatua ya kusema, Rais wa Awamu ya Tano alipaswa kuwa mtu ambaye japokuwa kiitikadi ni mwanachama wa chama hicho tawala, basi atapaswa kuwa mtu atakayekuja kuifumua kabisa CCM na kuiunda upya.

Watu wenye maono hayo, japo walikuwa ni sehemu ya viongozi wa karibu wa Kikwete, walikuwa ni wapinzani wakubwa wa lile kundi maarufu la mtandao lililomsaidia rais huyo kwa njia halali na haramu kuingia madarakani mwaka 2005.

Ilipofika Januari mwaka 2015, kundi hilo ambaye kinara wake alikuwa ni mmoja wa viongozi wakuu wanne wa CCM Taifa walikuwa tayari wameshakubaliana kwamba mwanasiasa ambaye alikuwa na sifa stahiki kwa wasifu waliokuwa wakiuhitaji hakuwa mwingine bali JPM.

Sisi tuliokuwa ndani ya vyumba vya habari na hususan katika viunga vya gazeti hili la Mtanzania, tulipozinasa taarifa hizo tulikaa chini na kujiridhisha pasi na shaka juu ya habari hizo kabla ya kuridhia uamuzi wa Mhariri wa gazeti Mtanzania Jumapili, Ratifa Baranyikwa kuzichapa chini ya kichwa kisemacho; “Wakubwa wamtaka Magufuli urais 2015”

Habari hiyo ambayo kwa wengi ilionekana kuwa ni taarifa ya kufikirika ilichapishwa mwezi Februari mwaka 2015, miezi takriban mitano kabla ya mchakato wa uteuzi wa CCM haujamtangaza rasmi JPM kuwa mgombea wake wa urais.

Kilichoandikwa na gazeti la Mtanzania kama rejea ya matamanio ya kundi moja ndani ya CCM, kiligusa moja kwa moja moyo na fikra za kada mwingine wa chama hicho, Anthony Mtaka ambaye sasa hivi ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambaye wakati fulani nilipokutana naye Morogoro wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero mwaka 2014 alikisema na kutamani kitokee.

Mtaka kwa maneno yale yale ya kutamani mapinduzi ya fikra alianza kutamani mapema kuona Magufuli akibeba bendera ya CCM katika urais, msimamo ambao aliurejea tena kwangu, wakati tulipokutana naye Arusha mwaka mmoja baadaye wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro wiki kadhaa kabla ya chama hicho tawala kutoa fomu za urais.

Siku ambayo Mtaka alirejea tena kauli yake huko Arusha akinitaka nianze kumfikiria Magufuli kuwa mwana CCM aliyekuwa akistahili zaidi kumrithi JK ni ile ambayo Edward Lowassa alikuwa akitangaza rasmi nia yake ya kuchukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho tawala.

Nikimwacha RC Mtaka ambaye mara kadhaa nimemsoma na kumsikia akimuelezea vyema JPM na hasa kwa nafasi yake, sina hakika iwapo wale wote ambao walitamani kuona JPM akirithi mikoba ya JK Ikulu bado wanaendelea kuamini iwapo chaguo lao limekidhi ndoto za matamanio yao.

Ninasema hivi kwa sababu ninazo kumbukumbu thabiti kwamba, hadi wakati JK alipokuwa akimaliza muhula wake wa kwanza wa urais mwaka 2010 zaidi ya nusu ya wana mtandao waliokuwa wakiunda kundi lililomuingiza Ikulu miaka mitano kabla walikuwa wamepoteza au kubakiza matumaini kidogo kwa chaguo lao.

JPM anao wajibu wa kugeuka nyuma leo na kuangalia vyema iwapo kweli anao uwezo wa kuvaa viatu alivyovaa Mkapa mwaka 2000 na hata mwaka 2005 wakati akimaliza mara zote kifua mbele hata kama ni kwa woga kipindi chake cha kwanza na cha pili cha urais.

Anapaswa kuanza kututhibitishia kwamba, ndoto zake za Tanzania ya viwanda na Tanzania ya uchumi wa kati itatimizwa akiwa na mawaziri wake hawa hawa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akina Charles Mwijage, Dk Philip Mpango na wengine wanaounda serikali yake.

Sitaki kujifananisha na Thomaso yule mwanafunzi wa Yesu mwenye imani haba hata nikaanza kutilia shaka kwamba huu msamiati usiokoma kwa miongo mitano wa ‘Rais wa wanyonge’, utakuwa umekoma katika kinywa cha JPM ifikapo mwaka 2020 na kama atapenya katika tundu la sindano mwaka 2025.

Ili aweze kufika 2020 na kuvuka salama, atapaswa kukirejea kile ambacho Mkapa alikisema kwa ufasaha mkubwa kule Dodoma Agosti 25 mwaka 2004 mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM katika hotuba ambayo nimekuwa nikiirejea mara kadhaa ambayo yeye mwenyewe Ben aliipa kichwa cha habari kisemacho ‘Ushupavu wa Uongozi” na akaitafsiri mwenyewe “The Courage of Leadership”

Mkapa alitoa hotuba hiyo ambayo japo ilionyesha woga wake dhidi ya vyombo vya habari na vyama vya upinzani ilijenga msingi imara kifikra kwa wana CCM waliokuwa wakijiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ambao ndiyo ambao ulimwingiza madarakani Rais Kikwete. Mungu akipenda tutaendelea wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles