Na Clara Matimo, Mwanza
SHIRIKISHO la Vyama huru vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Mwanza limempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma nchini.
TUCTA imetoa pongezi hizo kupitia maandamano yaliyofanyika jijini hapa leo Juni, 2 ambayo yaliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, yaliyolenga kumpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan.
Miongoni mwa maslahi ya wafanyakazi yaliyoboreshwa ni nyongeza ya kima cha chini cha mishahara kwa asilimia 23.3, kupandisha vyeo watumishi 92,619 na kuajiri watumishi wapya 12,336 ambao wamepunguza uhaba wa watumishi nchini hasa katika sekta za elimu na afya.
Pongezi hizo zilitolewa na Mratibu wa TUCTA Mkoa wa Mwanza, Zebedayo Athuman, akisoma risala ya Shirikisho hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel, baada ya kupokea maandamano hayo yaliyoanzia Gandhi hall hadi ofisi za mkuu huyo wa mkoa.
“Kwa niaba ya wafanyakazi wa Mkoa wa Mwanza TUCTA tunamshukuru pia Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kuruhusu maboresho katika posho za watumishi watakaosafiri ndani ya nchi kwa viwango vilivyobainishwa.
“Sisi wafanyakazi wa Mkoa wa Mwanza, tukiwa ni miongoni mwa wafanyakazi wa nchi hii tunaahidi kuwa waadilifu, wachapakazi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, wakati wote tutaendelea kukupa ushirikiano wakati ukiendelea kuifungua nchi yetu kiuchumi na kidiplomasia katika kuliletea taifa letu maendeleo,” alisema Athuman wakati akisoma risala hiyo na kuongeza.
“Ni dhahiri kwa kuongeza maslahi ya wafanyakazi mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, ametufuta machozi na kilio chetu cha kuongezewa mishahara na kupandishwa vyeo, tunaamini hata manung’uniko yaliyopo miongoni mwa wafanyakazi wa sekta binafsi na yale yanayohusu kikokotoo kilichopitishwa cha asilimia 33 atayatafutia ufumbuzi,” alisema.
Aidha, Athuman alimuomba Rais Samia Suluhu Hassan jitihada hizo alizozifanya kwa watumishi wa sekta ya umma zifanyike pia kwa uharaka na unyeti wake kwa wafanyakazi wa sekta binafsi ambao nao wanastahili kuongezewa mishahara kwani Mara ya mwisho kubadilishiwa kima cha chini ilikuwa ni mwaka 2013.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel, aliwasihi wafanyakazi hao kufanya kazi kwa bidii, wawe wazalendo, wapendane wawatumikie watanzania kama wanavyomtumikia Mwenyezi Mungu maana serikali inawajali ili wawe na morali ya kazi.
Akizungumza na Mtanzania digital, Mwalimu Viviani Nyambui kutoka jiji la Mwanza, alimpongeza Rais Samia kwa kuwarudisha shuleni wanafunzi wa kike waliopata ujauzito kwani sasa wataweza kutimiza ndoto zao.
Ikumbukwe wakati wa kilele cha Mei Mosi kitaifa mwaka 2021 yaliyofanyika Mkoani Mwanza Rais Samia Suluhu Hassan alitoa ahadi ya kuwaongezea mishahara wafanyakazi wa sekta ya umma.