Na Mwandishi Wetu - Dar es Salaam
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL), imekabidhi bidhaa mbalimbali za vyakula kwa vituo vitatu vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wazee wasiojiweza, ikiwa ni zawadi ya Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akikabidhi msaada huo Dar es Salaam jana kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba, Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemas Mushi, alisema vituo vilivyopokea msaada huo ni pamoja na Green Pastures Orphanage Mapinga Bagamoyo, Bethel Center Mbagala na Kituo cha Bethel cha Mbagala Kuu vyote vya Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kugawa msaada huo, Mushi, alisema ni utaratibu wa kawaida wa TTCL kutoa msaada kwa jamii, hasa kwa makundi ya watu wasiojiweza ili yaweze kujumuika na Watanzania wengine katika kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya kwa makundi hayo.
“Huu ni utaratibu wa kawaida wa kampuni yetu, kila mara hali ya uchumi inaporuhusu huwa tunayakumbuka makundi yenye mahitaji maalumu na kupitia ule utaratibu wetu wa kawaida wa kurejesha sehemu kidogo ya faida yetu kwa jamii, tumechagua makundi haya baada ya kupitia maombi yao na kujiridhisha wana vigezo vya kusaidiwa kutokana na walivyojieleza changamoto walizonazo,” alisema.
Mushi alisema TTCL itaendelea kuyakumbuka makundi hayo maalumu na kuyasaidia kwa chochote kadiri inavyokuwa na uwezo wa kufanya hivyo, huku akishauri taasisi nyingine na watu wanaojiweza kusaidia pale wanapokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
“Natoa wito pia kwa kampuni, taasisi na watu wengine wenye uwezo kuunga mkono juhudi hizi za kusaidia makundi ya wasiojiweza ili yaweze kufarijika kwa namna moja ama nyingine,” alisema.
Alizitaja bidhaa zilizokabidhiwa ni pamoja na mbuzi watatu, kilo 300 za mchele, ndoo tisa za mafuta ya kula, kilo 300 za maharage, kilo 150 za sukari, kilo 300 za unga, juisi, maji, soda na aina mbalimbali ya mafuta ya kujipaka na sabuni vyote vikiwa na thamani ya Sh milioni tano.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la EAG, Dennis Shija, ambaye ni Msimamizi wa Kituo cha Watoto na Wazee wasiojiweza cha Mbagala Kuu, alimshukuru Kindamba kwa msaada huo na kumhakikishia watautumia kama ulivyokusudiwa.
“Sisi tunashukuru kwa msaada tuliopokea leo (jana) kwa maandalizi ya sikukuu za mwisho wa mwaka huu, hii si mara ya kwanza kusaidiwa na TTCL, naomba kuwahakikishia msaada huu utatumika kama ulivyokusudiwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kituo cha Green Pastures Orphanage, Restiel Natai, aliishukuru TTCL kwa kuamua kuwakumbuka watu wasiojiweza ili waweze kusherehekea kwa furaha sikukuu hizi za mwisho wa mwaka.