33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

TTCL yaibuka mshindi wa pili Sekta ya Mawasiliano Sabasaba

*Yajipanga mwakani kushika nafasi ya kwanza

*Faiba mlangoni yawakosa washiriki Sabasaba

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Imeelezwa kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL linabeba taswira ya Kitaifa na hivyo kuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha mawasiliano yanapatikana kwa kila mwananchi na kwa bei nafuu.

Zuhura Muro akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa TTCL wakati alipotembelea banda la shirika hilo.

Hayo yameelezwa juzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, Zuhura Muro alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mwelekeo wa Shirika hilo mara baada ya kushika nafasi ya pili ya Mtoa huduma bora za mawasiliano katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Zuhura amesema TTCL imejipanga vizuri ambapo mwaka huu shirika lilijipanga kuwaonesha Watanzania na washiriki wote wa maonesho hayo kuwa linao uwezo wa kuiunganisha nchi kidigitali kwani mwelekeo uliopo sasa mawasiliano ndiyo nyenzo muhimu ya kunyanyua uchumi, hivyo kuweza kuchangia pato la Taifa na kulikuza kupitia mawasiliano.

“Tumejipanga vizuri kimkakati kuhakikisha tunaufuata mwelekeo huo ambapo mkakati huo unaenda sambamba na kuangalia usalama wa nchi yetu, rasilimali zetu zikiwemo za baharini, nchi kavu na za angani,” amesema Zuhura.

Amesisitiza kuwa katika maonesho yajayo ya 47 wananchi watarajie kuiona TTCL ambayo imeanza kutimiza mkakati ambao utaifungua Tanzania kidigitali na Mataifa mengine, hivyo malengo ya maonesho yajayo ni kuhakikisha inakuwa kinara katika nafasi ya mtoa huduma bora za mawasiliano nchini nakwamba ushindi huo utakuwa endelevu.

Katika hatua nyingine Zuhura amewaasa watumishi wote kwa ngazi zote kufanya kazi kwa bidii ili mikakati inayowekwa na Menejimenti inatimilika na hivyo kuliwezesha shirika kutimiza wajibu wake kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema shirika hilo litaendelea kuweka nguvu kubwa katika bidhaa na huduma na kwamba kwa mwaka huu eneo lililowekewa mkazo ni suala la huduma ya faiba mlangoni ambayo inawahakikishia watumiaji mbalimbali wa huduma za mawasiliano kupata huduma kwa kasi kubwa kabisa majumbani na ofisini.

Amesema maonesho ya mwaka huu yameshuhudia nguvu kubwa iliyowekwa na hivyo kuibuka washindi nafasi ya pili sekta ya mawasiliano na kuwaahidi maonesho yajayo kufanya vizuri zaidi.

Ameongeza kuwa TTCL katika utekelezaji wa majukumu yake haipaswi kujishindanisha na kampuni yoyote bali inapaswa kujishindanisha yenyewe kwa kuhakikisha linakidhi mahitaji ya wateja na serikali kwa ujumla, hivyo wafanyakazi wanapaswa kufanya kazi kwakujituma na kuongeza ubunifu kwa kila mmoja katika nafasi yake.

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara(Sabasaba) yamefungwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango ambapo pamoja na mambo mengine amezishukuru Kampuni za Mawasliano nchini kwakuandaa programza bunifu ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao kidigitali katika nyakati zote za janga la ugonjwa wa Uviko-19 ambapo kwa kiasi kikubwa uliathiri shughuli za kibiashara na kusababisha uchumi kushuka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles