Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Tropiki (TPRI), zimeingia makubaliano ya maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki.
Mfumo huo uliopewa jina la ‘T–Hakiki’ ni huduma ya simu ya mkononi ambayo itamwezesha mkulima kupata taarifa ya kiuatilifu kilichosajiliwa na kwa matumizi sahihi ili kuleta tija katika kilimo
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Kezia Katamboi alisema baada ya makubaliano hayo, utoaji wa huduma hiyo unatarajiwa kuanza mwezi ujao ikiwa ni baada ya kukamilisha baadhi ya taratibu zinazotakiwa.
Katamboi alisema makubaliano hayo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo, ufugaji na viwanda.
Alisema hii ni hatua kubwa katika kulinda bidhaa za kilimo na ufugaji kwani itahakikisha wakulima na wafugaji wanapata mavuno yanayostahili.
“Kwa kupitia mfumo huu ambao utatumia mawasiliano ya TTCL Corporation, utakuwa suluhisho ya kuondoa viuatilifu feki sokoni na kuongeza kasi ya matumizi ya viuatilifu sahihi vya kilimo na ufugaji kwa kuwa mtandao wa TTCL Corporation umeenea nchi nzima hivyo wakulima wote nchi nzima watanufaika na mradi huu.
“Zaidi ya yote, huduma hii itapatikana bure kwa wakulima na wafugaji wote nchini. Kupata huduma hii, mkulima au mfugaji kupitia kwenye simu yake ya mkononi atabofya *148*52# kisha atafuata maelekezo,” alisema Katamboi.
Aidha, Mkurugenzi wa Biashara wa Quincewood ambayo inasimamia mfumo huo wa kuhakiki viuatilifu kwa kutumia teknolojia ya kielektroniki, Fatma Fernandes alisema sekta ya kilimo ni muhimili wa maendeleo ya uchumi.
“Sekta hii inachangia kiasi cha nusu ya pato la taifa, robo tatu ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi na chanzo cha chakula pamoja na utoaji wa fursa za ajira zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania.
“Kilimo kina uhusiano na sekta zisizo kuwa za kilimo kupitia uhusiano wa usafirishaji kwenda kwenye usindikaji wa mazao ya kilimo, matumizi ya ndani, uuzaji nje ya nchi na uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu,” alisema Fatma.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropikia, Dk. Margaret Mollel alisema kuwa huduma ya T-Hakiki itamwezesha mkulima kupata taarifa kuhusu viuatilifu vilivyosajiliwa na vyenye ubora unaotakiwa kwa kutumia hapo alipo kwenye sehemu yake ya kilimo.