27.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

Mloganzila yaanza huduma kutoa vivimbe kwenye matiti

Aveline Kitomary – Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili –Mloganzila imeanza kufanya upasuaji wa kutoa uvimbe kwa wanawake wenye saratani ya matiti, huku daktari bingwa wa upasuaji wa hospitali hiyo akisema kwa sasa waathirika wa ugonjwa huo ni kuanzia wasichana wenye miaka 25.

 Daktari Bingwa wa Upasuaji, Casper Haule, alisema hatua hiyo ni kutokana na ugonjwa huo wa saratani ya matiti kushika nafasi ya pili kwa kushambulia wanawake ukiwa na asilimia 16 baada ya sarani ya mlango wa kizazi ambayo ni asilimia 47.

Kwa mujibu wa takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili, wanaogunduliwa na saratani ya matiti ni wanawake wenye miaka 40 hadi 80.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Dk. Haule alisema wanafanya upasuaji huo kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka hospitali za Bugando, KCMC, Mbeya, Benjamin Mkapa na Zanzibar.

“Tunafanya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo madaktari wa hospitali za Serikali. Kwa mwaka jana tulifanya kwa wagonjwa tisa na wanne ni wa kutoa uvimbe. Na mwaka huu tunafanya upasuaji huu kwa kushirikiana na  madaktari hao, lengo ni kujenga uwezo hawa madaktari.

“Tutafanya upasuaji kwa wagonjwa nane ndani ya siku tatu, na leo (jana), kati ya wagonjwa hao nane, wawili watatolewa titi lote na sita watatolewa vivimbe,” alisema Dk. Haule. 

Alisema kwa mwaka jana kati ya wanawake 162 waliofanyiwa utafiti, 152 walifanyiwa upasuaji.

“Tatizo la kansa ya ziwa sasa hivi linaongezaka. Kwa mfano sisi kwa Muhimbili mwaka jana tumeweza kufanya operesheni 152, kati ya hizo wagonjwa 20 walifanyiwa upasuaji wa kutoa uvimbe tu bila kutoa titi lote na hao  wagonjwa wamepata matibabu Ocean Road.  

“Wapo wagonjwa wengi wanakimbilia kutoa uvimbe. Utakuta hata kuna wengine hawapimi, matibabu kidogo inakuwa changamoto kwa sababu akitolewa huko unakuwa hujui ule uvimbe wa kwanza ulikuwa wapi na una ukubwa gani, kama hao unakuja kutoa titi lote,” alisema Dk. Haule.

Hata hivyo aliwataka madaktari wafanye uchunguzi kwa wagonjwa wenye vivimbe ili kubaini kama ni saratani au laa. 

Dk. Haule alitoa wito kwa kina mama kujitokeza kupima saratani ya matiti ili kubaini na mgonjwa kupata matibabu haraka.

“Uelewa kuhusu ugonjwa huu unaongezeka na wagonjwa wengi wanakuja na dalili za mwanzo za saratani, kwa hiyo hao ndio ambao wanatolewa vivimbe, wito hasa kwa kina mama sasa ugonjwa huu unawapata hadi wasichana wa miaka 25, wajitokeze kupima mapema. 

“Kwa sababu ukimtoa titi binti wa miaka 35 unajaribu kuangalia namna gani anaweza kuathirika kisaikolojia, unamjengea kutokujiamini na kujichanganya kwa wenzake. Wajitahidi kuja mapema na sisi madaktari tutajitahidi kutoa matibabu ya kisasa zaidi,” alishauri Dk. Haule.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,530FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles