Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL-Corporation) limeingia makubaliano ya kibiashara na Taasisi ya Serikali ya Nchini Burundi inayosimamia Mawasiliano ya Mkongo wa Taifa wa nchi hiyo, Burundi Backbone System (BBS) ili TTCL kuwezesha mawasiliano katika taifa hilo.
Makubaliano hayo yamefikiwa jana jijini Dar es Salaam na yatadumu kwa takribani miaka 10 huku yakihusisha, TTCL Corporation kutoa huduma za data na intaneti zijulikanazo kwa kitaalamukama IP TRANSIT, BACKHAULING pamoja na huduma ya IPLC.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Waziri Kindamba alisema hatua hiyo ni ya mafanikio kwani TTCL litakuwa ni Shirika pekee linalotoa huduma ya mawasiliano ya mkongo nchini Burundi kupitia vituo vyake vya mpakani katika miji ya Kabanga na Manyovu, na kuiunganisha nchi ya Burundi na Dunia kupitia mikongo mikubwa ya baharini Seancom na Easy.
Kindamba, alisema kuwa makubaliano hayo ya kibiashara yenye thamani ya shilingi Bilioni 13.8 yatahusisha TTCL Corporation kutoa huduma za utunzaji wa kumbukumbu mbadala kupitia kituo cha kimataifa cha kutunzia kumbukumbu ‘National Internet Data center’ cha jijini Dar es Salasam, pamoja na kubadilishana wataalamu kwa kujengeana uwezo kitaalamu nyanja mbalimbali za mawasiliano.
“Mabadilishano ya wateja hasa kwa wateja wakubwa wenye matawi ya biashara au ofisi katika nchi zote mbili (Burundi na Tanzania) kwa mfano Benki ya CRDB, pia kupeana ushauri wa kitaalamu kuhusu watoa huduma na watengenezaji wakubwa wa vifaa vya Mawasiliano vinavyotumika kuhudumia mawasiliano ya mkongo,” alisema
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfumo wa Mawasiliano ya Taifa la Burundi, Elie Ntihagowumwe aliishukuru Tanzania kupitia TTCL kwa kuendelea kushirikiana kibiashara na masuala mengine mengi ambayo Tanzania imekuwa ikiisaidia nchi ya Burundi.
Alisema mbali na makubaliano hayo ya kibiashara Burundi itanufaika kwa mengi haswa kujifunza kutokana na hatua ambazo taifa la Tanzania limepiga kwa sasa ukilinganisha na taifa la Burundi.
“Tunashukuru kwa uhusiano huu wa kibiashara tulioingia leo. Hata hivyo taifa letu lina mengi ya kujifunza na kunufaika kutoka Tanzania hasa kwa hatua Tanzania imepiga kwa sasa,” alisema Ntihagowumwe.
Mwisho