28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Pinda apongeza utekelezaji mpango wa maendeleo

Na MWANDISHI WETU

-PWANI

WAZIRI Mkuu mstaafu Mizengo Pinda amesifu Serikali kwa kuendelea kutekeleza mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016 /21 kwa kukuza uchumi wa viwanda hali ambayo itafanya wananchi kuondokana nan a umasikini kutokana na viwanda hivyo kutumia malighafi zilizopo nchini.

Waziri Mkuu Mstaafu Pinda aliyasema hayo juzi wakati akifunga maonesho ya bidhaa za viwandani vilivyoko Mkoa wa Pwani yaliyokuwa yakifanyika katika viwanja vya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha Mjini.

Alisema moja ya mpango huo ni ujenzi wa reli ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam- Morogoro na makutopora na kwamba kukamilika kwake itakuwa na mchango mkubwa kwa Taifa ambapo Mkoa wa Pwani utakuwa umepata fursa kubwa itakayokuwa inawasaidia wawekezaji wake katika kufanya biashara kutokana na mnyororo wa usafiirishaji.

Pinda alisema uwepo wa Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL) kwa kuwa na ndege mchango wake mkubwa kwa faida ya maendeleo ya Taifa na kuiingizia nchi fedha za kigeni kutokana na wafanyabiashara wengi kuja nchini kwa ajili ya uwekezaji pamoja na fursa za utalii.

“Baadhi ya watu walikuwa wanasema maneno ya hovyo sana,mara vindenge vyenyewe vidogo,havijazi watu na maneno mengine mengi ya kubeza juhudi hizo lakini sasa hivi watu wanaruka moja kwa moja kutoka India kwa ndege hizohizo kwahiyo lazima tukubali matokeo,”alisema Pinda

Mbali na miradi hiyo alisema RaisDk. John Magufuli, anajenga mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere huko Rufiji Mkoani Pwani ambao kukamilika kwake utakuwa na uwezo wa kufua umeme zaidi ya megawati 2000 ambao utasaidia kuboresha mazingira ya uendeshaji kwa wamiliki wa viwanda nchini.

Alisema kuwa, mradi huo wa umeme ulibuniwa miaka mingi ya nyuma tangu enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini Rais Magufuli amefanikiwa na sasa anajenga kwa fedha nyingi kwahiyo lazima watu wakubali matokeo hayo ya maendeleo na ikiwezekana waunge mkono juhudi za Serikali.

Kutokana na hali hiyo alizipongeza taasisi wezeshi kwa namna zilivyojipanga kuendeleza shughuli za uwekezaji wa viwanda hapa nchini kwakuwa jambo hilo litasaidia kuimarisha uchumi wa nchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Evarist Ndikilo, alisema chimbuko la maonesho hayo limetokana na wamiliki wa viwanda kuonyesha changamoto za ukosefu wa masoko kupitia bidhaa wanazozalisha na hata kutofahamika kwa Wananchi.

Ndikilo, alisema malengo mahususi ni kutangaza bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya mkoa wa Pwani pamoja na kusaidia kutafuta masoko kwa bidhaa hizo na kwamba mpaka maonesho hayo yanakamilika zaidi ya watu 10,000 wametembelea.

Alisema kuwa kupitia maonesho hayo wawekezaji wamepata masoko mbalimbali na hata baadhi ya wananchi wamenufaika kwa kutambua bidhaa mbalimbali zinazopatikana mkoa wa Pwani huku akisema kupitia kauli mbiu ya ujenzi wa viwanda mkoa umetenga zaidi ya ekari 53,000 kwa ajili ya wawekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles