25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TSC yahamasishwa kuhakikisha walimu hawaondoki kazini

Na Veronica Simba – TSC, Mwanza

Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wamehamasishwa kubuni mbinu zitakazowafanya walimu waache kukiuka maadili ya kazi yao, suala ambalo husababisha wengi kupata adhabu mbalimbali ikiwemo kufukuzwa kazi.

Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Mwl. Martin Nkwabi, akifungua mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) zilizoko Kanda ya Ziwa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Aprili 28, 2021 jijini Mwanza. Kulia ni Mwenyekiti wa TSC Prof. Willy Komba.

Wito huo umetolewa Aprili 28 mwaka huu  na Afisa Elimu wa Mkoa wa Mwanza, Mwl. Martin Nkwabi, wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Wilaya za TSC zilizoko Kanda ya Ziwa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo.

“TSC hakipaswi kuwa chombo cha kusubiri mashauri. Lazima muwe na utaratibu wa kuhakikisha walimu hawafanyi makosa yanayosababisha kuondolewa kazini,” alisisitiza.

Kuhusu suala la maadili, Mwl. Nkwabi ameishauri TSC kuzifikia shule zote kwa lengo la kuhakikisha walimu wanazingatia maadili ya kazi yao kwa kuwalea vema wanafunzi ili wawe raia wema.

Alisema kuwa ni wajibu wa walimu kusimamia maadili na makuzi ya wanafunzi hivyo TSC ikiwa ni Mamlaka yao ya Nidhamu, inapaswa kuhakikisha wajibu huo unatekelezwa kikamilifu.

Afisa Elimu huyo alikemea tabia ya baadhi ya walimu kuwachukulia wanafunzi kama wateja wao hivyo hawashughuliki na malezi yao wakiamini kuwa mteja hakemewi kwani ndiye anawawezesha kupata mshahara.

“Siku walimu wote wakiwaangalia wanafunzi kama watoto wao wa kuzaa, tunaweza kuondokana na tatizo hili,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TSC, Prof. Willy Komba, akitoa neno la kumkaribisha Mgeni Rasmi, aliwaasa watendaji wa Tume hiyo kuhakikisha wanatenda haki kwa walimu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, ili nao waweze kuwalea wanafunzi vema.

“Walimu bora ndiyo watazaa elimu bora. Walimu bora lazima wahudumiwe vizuri. Bila kuwahudumia walimu vizuri watakuwa na manung’uniko na kero na hawatafanya kazi vizuri. Ndiyo maana Serikali ikatuamini sisi tuwahudumie,” alisisitiza Prof. Komba.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa Kamati za Wilaya za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) zilizoko Kanda ya Ziwa, wakichangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Mwanza, Aprili 28, 2021.

Akitoa neno la utangulizi, Katibu wa TSC, Mwl. Paulina Nkwama alitoa shukrani kwa Mungu na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kushika wadhifa huo, hivyo aliahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu na weledi ili asimwangushe Rais.

Akizungumzia mafunzo husika, Mwl. Nkwama alieleza kuwa ni zoezi endelevu ambalo litaendelea katika Kanda zote saba zinazohudumiwa na TSC kwa lengo la kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati husika waweze kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

“Ni matarajio yetu kuwa baada ya mafunzo haya, Wajumbe wa Kamati husika wataenda kutatua kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili walimu, ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao ya kuwalea wanafunzi ipasavyo kimwili na kiroho.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameshirikisha Wajumbe kutoka Wilaya zote za Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambazo ni Mara, Geita, Simiyu, Shinyanga na Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles