28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Trump kuwa mgombea urais ni kasoro ya kidemokrasia Marekani (1)

Donald TrumpNA IBRAHIM LIPUMBA

WAPIGA kura wa chama cha Republican wamemchagua Donald Trump kuwa mgombea wa urais wa Marekani. Kauli za Trump na uchambuzi wa wataalamu na waaandishi wa habari magwiji umeonyesha kuwa ni mbaguzi, mropokaji, hana subra na hafai kuwa kiongozi wa taifa kubwa la Marekani atakayekabidhiwa funguo za mabomu ya nyuklia yanayoweza kuteketeza dunia yote.

Imekuwaje wapiga kura wa chama cha Republican, chama cha kiongozi maarufu Rais Abraham Lincoln, aliyetangaza uhuru wa watumwa wote wa Marekani mwaka 1861 na kulazimika kuingia kwenye vita kupinga utumwa katika majimbo ya Kusini ya Marekani yaliyotaka kujitenga, kimchague Trump, mbaguzi dhahiri asiyekuwa na busara kuwa mgombea wa urais?

Mke wake wa kwanza alieleza kuwa kabla ya kulala alikuwa akisoma vitabu vya Adolf Hitler, fashisti mkuu wa Ujerumani aliyesababisha mauaji ya watu wengi wakiwamo Wayahudi milioni 6 wakati wa vita vya pili.

Trump alieleza siku za nyuma kuwa Wamarekani weusi ni wavivu, hataki wafanye kazi za kihasibu katika kampuni zake. Amewaita wananchi wa Mexico kuwa ni wabakaji. Ameahidi kujenga ukuta katika mpaka kati ya Marekani na Mexico kuzuia wahamiaji haramu na atailazimisha Mexico ilipie gharama za ukuta huo.

Amewashutumu Waislamu wote kuwa ni magaidi na kuahidi kuwazuia wasiingie Marekani mpaka itakapoeleweka wana matatizo gani.

Marekani ina vituko vingi. Lakini katika historia ya kampeni za Marekani, Trump ni mgombea pekee wa chama kikubwa Republican au Demokratic aliyejisifia hadharani kwenye mdahalo kuwa yeye ana kifaa kikubwa.

Trump ana dharau dhidi ya wanawake. Mwaka 1992 alilieleza gazeti la New York Magazine kuwa wanawake wanapaswa kutendewa kama uchafu “You have to treat ’em like shit.”  Alimshambulia mwana habari wa Televisheni ya Fox ambaye alikuwa anamuuliza maswali katika mdahalo wa wagombea urais wa Chama cha Republican na kumweleza kuwa damu ilikuwa ikimvuja wakati akimuuliza maswali.

Chama cha Republican kinaungwa mkono na Wakristo walokole. Mke wa sasa wa Trump ambaye asili yake ni Mslovenia ni wa tatu. Trump hana maadili. Ana lugha chafu.

Trump si msomaji wa vitabu na nyaraka. Maarifa na taarifa anazopata ni kupitia kutazama televisheni. Hana uelewa wa sera na matatizo ya uchumi, usalama, ulinzi na uhusiano wa kimataifa yanayoikabili Marekani.

Siku chache kabla ya kura ya Uingereza kuhusu kujitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya, alikuwa hajui maana ya neno ‘Brexit’. Ni bingwa wa majibu mepesi katika masuala magumu yanayoikabili Marekani.

Michael Bloomberg, Meya wa zamani wa New York na Bilionea mkubwa anaamini kuwa Trump ni tapeli na hana akili timamu.

Trump anajisifia kuwa ni mfanyabiashara mahiri. Katika shughuli zake za biashara za ujenzi wa nyumba na casino ana sifa ya kutangaza kuwa amefilisika na kutowalipa makandarasi na kampuni nyingine zilizomuuzia huduma na bidhaa. Kwenye kila shughuli anayofanya ina mlolongo wa kesi nyingi.

Alianzisha Chuo Kikuu cha Trump kilichoahidi kufundisha utaalamu wa kumwezesha mwanafunzi wa chuo hicho kuwa mahiri katika biashara hasa katika sekta ya nyumba na kuweza kuwa tajiri. Ada ya chuo ilikuwa dola 35,000 sawa na zaidi ya Sh milioni 70.

Chuo cha Trump hakikutoa mafunzo ya maana na Serikali ya Jimbo la New York ilikifunga kwa kubaini kuwa ni chuo cha kitapeli. Wanafunzi wengi wa chuo hicho wanamshtaki Trump kudai warudishiwe ada zao walizotapeliwa.

Trump amemshutumu Jaji anayesikiliza kesi hii kwenye jimbo la California, mwenye asili ya Mexico lakini mzaliwa wa Marekani kuwa hawezi kumtendea haki kwa sababu ni Mmeksikani.

Kashfa za Trump ni nyingi lakini amejijengea umaarufu kwa kushiriki katika kipindi cha televisheni – Reality TV. Alijijengea umaarufu wa kisiasa miongoni mwa Wamarekani wabaguzi na wahafidhina kwa kufanya kampeni ya kudai kuwa Rais Barak Obama hakuzaliwa Marekani. Ilimlazimu Rais Obama kuonyesha cheti chake cha kuzaliwa kilichotolewa katika visiwa vya Hawaii ili kuizimisha kampeni hii.

Mwaka 1987, Trump alisaidiwa na Tony Schwartz, aliyekuwa mwandishi wa habari, kuandika kitabu cha ‘The Art the Deal’ ambacho kilieleza namna anavyofanya biashara na kuongeza utajiri wake. Kitabu hicho kilipendwa na kununuliwa kwa wingi.

Zaidi ya nakala milioni moja ziliuzwa na Trump na Schwartz walilipwa mamilioni ya dola. Alipokuwa anatangaza nia yake ya kugombea urais alieleza kuwa sifa yake kubwa ni mfanyabiashara mahiri na ameandika kitabu cha ‘The Art of the Deal.’

Itaendelea wiki ijayo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles