23 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Clinton, Sanders walivyounusuru mkutano mkuu wa Democratic

BernieSandersHillaryClintonNA JOSEPH HIZA

VYAMA vikuu vya siasa nchini Marekani, Democratic na Republican, vimefanya mikutano yao mikuu iliyopitisha rasmi wagombea wao watakaowania kuongoza taifa hilo katika Uchaguzi Mkuu wa Novemba 8, mwaka huu.

Ikiwa imefanyika kwa nyakati tofauti mwezi uliopita, ilishuhudia tofauti na pia mifanano ya mambo.

Achana na tofauti hizo, miongoni mwa mifanano ni kwamba matukio yote mawili yaliandika historia.

Yote ilijaribu kutibu mipasuko kutokana na uwapo makundi yanayosigana kuhusu wagombea wao hao, hivyo kuweka historia kwa vyama hivyo kutoa wagombea wasiokubalika vyema.

Aidha yote miwili ilitumia ‘hofu’ na ‘mashaka’ kutilia uzito wa kampeni zao kujiandaa kwa uchaguzi huo.

Katika hilo, mgombea urais wa Republican, Donald Trump, aliutumia mkutano huo mjini Cleveland kuchochea hofu; kuwa taifa limeparanganyika na linakabiliwa na tishio la misukosuko na machafuko kutoka pande zote.

Hivyo, alitaka kuuaminisha umma kuwa nchi haipaswi kurudishwa mikononi mwa Democratic.

Lakini mgombea urais wa chama hicho, Hillary Clinton, katika mkutano wao wa Philadelphia, maono yake yalipingana na dhana hiyo; akiuhakikishia umma kuwa taifa hilo li katika hadhi yake ya ukuu bado. Na hofu aliyoizungumzia ni taifa hilo kuangukia katika mikono isiyo salama;-Trump.

Clinton alieleza hatari ya kukabidhi dhamana juu ya majeshi na nyuklia kwa mtu ambaye; alimaanisha yu ‘kichaa’.

Tukirejea katika suala la mpasuko ndani ya vyama hivyo, maandamano na zomea zomea zilitawala.

Wakosoaji hawamkubali Trump kwa kushindwa kudhibiti mdomo wake unaoudhi wengi ndani na nje ya taifa hilo, wakati Clinton anachukuliwa mwongo, mzembe, mbabaishaji na mbinafsi fulani aliye kwa ajili ya matajiri.

Licha ya kuwa mkutano uliompitisha Trump, zomea zomea na maandamano hazikutikisa sana kulinganisha na za mkutano uliompitisha Clinton, mwishowe ni Democratic walioibuka washindi.

Kwanini? Wakati mgawanyiko ndani ya Republican ukisawazishwa kwa staili ya ‘kuzima moto wa kifuu cha nazi kwa mchanga’, ule wa Democratic tofauti zilifanyiwa kazi kwa miezi kadhaa.

Wakijua fika bila kuchukua hatua mkutano huo chama kingepata janga, wasaidizi watano wa Clinton na watatu wa aliyekuwa mpinzani wake katika uteuzi ndani ya Democratic, Bernie Sanders walikutana faragha na kuanza kuzifanyia kazi tofauti zao.

Miongoni mwa wasiwasi uliojadiliwa ni mpango wa wajumbe wanaomuunga mkono Sanders kuuvuruga na hivyo kuhatarisha mkakati wa kuunganisha majeshi dhidi ya Trump.

Njama za kuvuruga ilikuwa ni pamoja na kushinikiza hadi kieleweke Nina Turner, mwanaharakati mwenye msimamo mkali wa Sanders, awe mgombea mwenza badala ya Seneta wa Virginia, Timothy M. Kaine.

Lingine ni watu, ratiba na utaratibu wa kuzungumza wakati wa mkutano huo, ambao kambi ya Sanders ilikuwa na mapendekezo yake yaliyokuwa awali yakikataliwa na ile ya Clinton.

Ushirikiano huo ulianza hata kabla ya mchakato wa kura za uteuzi kumalizika, ikiwamo ziara nyumbani kwa Sanders jimboni Vermont iliyofanywa na Meneja wa Kampeni ya Clinton, Robby Mook.

Majadiliano hayo hayakuzuia Sanders kuzomewa mwanzoni mwa mkutano huo Jumatatu ya wiki iliyopita na wajumbe karibu 1900 wanaomuunga mkono pale alipowataka wamuunge mkono Clinton.

Hilo lilimfanya Mook ampigie simu meneja wa kampeni wa Sanders, Jeff Weaver.

Muda mfupi baadaye Sanders alituma ujumbe mfupi wa maneno kwa wajumbe wake hao, akiwasihi kwa heshima yake wajaribu kumwelewa kwanini wamsaidie Clinton.

Lakini hilo bado lilitua katika masikio mfu, kwani kadiri mkutano ulivyoendelea, jina la Clinton lilipotajwa, zomea zomea iliibuka.

Ukaidi wa wajumbe hao ulichagizwa zaidi na kuibuka kwa kashfa ya barua pepe zilioonesha Sanders hakutendewa haki na vigogo wa chama hicho.

Wakati wa kuelekea mkutano huo, barua pepe 20,000 zilianikwa hadharani na mtandao maarufu wa Wikileaks  zikionesha Sanders alivyohujumiwa kwa kumuonesha yu mtu asiyeamini uwapo wa Mungu.

Hilo lililazimisha pia kujiuzulu kwa mwenyekiti wa chama na mkutano huo, Debbie Wasserman Schultz, baada ya kubainika alisambaza barua pepe zikieleza Sanders kamwe hatokuwa rais.

Akiwa amekasirika Sanders alisema: Mimi si mkana uwapo wa Mungu. Sishtushwi na hilo, lakini nimesikitishwa sana, hili ni tusi.

Alisema hakuna ubishi vigogo wa chama hicho walikwamisha kampeni yake na kumpendelea waziwazi Clinton wakati wa mchakato wa uteuzi.

Licha ya hayo, Sanders ameweka wazi anatarajia kwa nguvu zote kumpigia kampeni Clinton, akisema Trump ni mtu hatari kuiongoza Marekani.

Alisema mtu mwenye kuligawa taifa, si mtu anayehitajika, bali yule mwenye kuwaleta watu pamoja na hivyo chaguo sahihi ni Clinton.

Majadiliano yaliendelea hata baada ya kuibuka kashfa za barua pepe, ijapokuwa zomea zomea iliendelea hadi usiku wa mwisho, lakini mafanikio yalionekana, kwani hali ilikuwa tofauti na mwanzoni.

Wakati wa hotuba, Clinton alitenga mistari kadhaa maalumu kwa wafuasi wa Sanders akisema. “Nimewasikia. Kilio chenu ni chetu sote”. Hadi mkutano unakwisha timu ya Clinton ilitangaza wiki ya mafanikio.

Mojawapo ya mafanikio hayo yaliweza kuonekana usiku wa Alhamisi, wengi wa wafuasi wa Sanders walipopeperusha mabango yenye jina la Hillary.

Mchuano mkali baina ya Clinton na Sanders ulianza mapema mwaka jana kwa wagombea wote wawili kuzungumza kwa nadra.

Kwa kadiri Sanders alivyokuwa akipunguza pengo la kura za uteuzi kinyume na matarajio ya wengi kuwa angekuwa msindikizaji, ndivyo mpasuko baina yao ulivyoongezeka.

Na hata Clinton alipopata kura za kutosha kutwaa tiketi ya kugombea urais Juni mwaka huu, ilimchukua Sanders mwezi mzima kumpitisha.

Lakini Juhudi za kusaka amani za Clinton zilianza mapema, hasa alipopata uhakika wa kushinda wakati alipokuwa akiinua simu kumpigia Sanders akimpongeza aliposhinda.

Mwishowe Sanders naye akawa akifanya hivyo na hilo liliwezesha uaminifu na mshikamano wakati wa mkutano huo mkuu.

Aidha uhusiano wa mameneja wao wa kampeni uliojengeka kwa miezi kadhaa, ulikuwa msingi muhimu zaidi ya upatanisho huo.

Ijapokuwa wote wawili wanatokea Vermont, Mook na Weaver walikuwa hawajakutana kabla ya kuanza mchakato kwa uteuzi.

Lakini Oktoba mwaka jana katika hafla moja ya chakula cha usiku walionesha urafiki hadharani.

Na wakati wa kura za mchujo California Juni 7, mwaka huu zilipokatisha matumaini kwa Sanders kuteuliwa kuwania urais baada ya jimbo hilo kwenda kwa Clinton, Weaver na Mook wakawa wakizungumza kila siku.

Ni wao waliofanikisha mkutano baina ya Sanders na Clinton wiki moja baadaye.

Kilichokuwa wazi, Sanders alitaka kutumia fursa hiyo kushinikiza sera zake kipenzi cha wengi nchini humo kutumiwa na kambi ya Clinton.

Clinton alionesha kukubali hilo hasa katika masuala mawili; ada ya vyuo na upatikanaji wa huduma za afya.

Sanders kwa mfano; kampeni zake zilikuja na ahadi ya elimu bure kwa kila anayehudhuria chuo cha kati na kikuu cha umma.

Ilhali Clinton alikuwa akisema fedha za walipa kodi hazipaswi kuwapeleka watoto wa bilionea Trump shule, akimaanisha bure isiwe kwa kila mtu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles