WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Mteule wa Marekani, Donald Trump amefanya mkutano wa kwanza na wanahabari tangu achaguliwe na kuelezea masuala kadhaa juu ya uhusiano wake na Urusi, udhibiti wa kampuni zake, na ujenzi wa ukuta na Mexico.
Hata hivyo, katika mkutano huo uliochukua saa moja Trump alionekana kujawa na hasira na kuvishambulia baadhi ya vyombo va habari kikiwemo kituo cha utangazaji cha CNN.
Trump alisema CNN ni chombo cha ‘habari za uwongo’ na alikataa kujibu maswali ya waandishi wake.
Trump alibishana na mwandishi Jim Acosta wa CNN na alinukuliwa akisema, ‘hapana sio wewe, sio wewe, shirika lako ni la hovyo! kaa kimya! nyamaza, siwezi kukupa nafasi ya kuuliza swali nyie ni chombo cha habari za uwongo.”
Wakati wa mkutano huo Trump pia alitangaza kuachia udhibiti wa kampuni zake kwa watoto wake wakubwa Donald Trump Jr. na Eric Trump.
Aidha Trump alionekana kukubali kuwa Urusi ilihusika na udukuzi wa uchaguzi mkuu lakini alisema mataifa mengine pia yamewahi kuingilia uchaguzi wa taifa hilo.
Akijibu maswali kadhaa, Trump amesema anaamini ni faida kwa Marekani ikiwa wataelewana na Urusi.
Alisema huo ni ‘mtaji’ wala sio ‘deni’ kwa sababu kumekuwa na mahusiano mabaya baina ya mataifa hayo mawili kwa miaka mingi.
Kuhusu ujenzi wa ukuta wa Mexico kiongozi huyo amesema ahadi yake iko palepale akisema Marekani itafadhili upande wa mbele wakati Mexico ikigharamia ujenzi wake.
Muda mchache baadae Rais Enirique Pena Nieto wa Mexico alimjibu kwa kukataa mpango huo wa Trump.