23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Trump atua Uingereza, akimshambulia meya wa London

LONDON, UINGEREZA

RAIS wa Marekani, Donald Trump jana aliwasili nchini Uingereza katika ziara yake ya kiserikali iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu, huku hatua yake ya kwanza ikiwa  ni kurusha kombora kupitia akaunti yake ya Twitter  dhidi ya Meya wa London, Sadiq Khan akisema ni ‘Jiwe potevu la baridi’.  

Ujumbe huo wa Rais Trump kwa Khan ambao ulisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii muda mfupi baada ya ndege yake ya Air Force One kutua katika uwanja wa ndege  jana asubuhi, ulieleza kuwa Khan; “amefanya kazi mbaya na ya kijinga  kama Meya wa London na kwamba anatakiwa kujielekeza kupambana na uhalifu na si  kumshambulia Trump”. 

Trump ambaye ametumia ziara yake  hiyo ya Uingereza kutoa dukuduku lake dhidi ya kauli ya Khan aliyemwelezea rais huyo wa Marekani kama ni fashisti wa karne ya 21,  pia alimdhihaki kwa kuwa ‘mfupi’.

“Khan ananikumbusha sana kuhusu meya wetu asiye na uwezo wa Jiji la New York, De Blasio (Billy de Blasio),  ambaye naye amefanya kazi mbaya –nusu tu ya urefu wake. Kwa namna yeyote natarajia kuwa rafiki mzuri wa Uingereza, natua sasa,” aliandika Trump wakati anawasili Uingereza.  

Awali Khan alisema Uingereza haipaswi kukunjua kapeti jekundu kwa ajili ya Trump.

Kauli ya jana ya Trump dhidi ya Khan ilijibiwa na msemaji wa Meya huyo wa London aliyesema “matusi ya kitoto ” yanapaswa kuwekwa kando na Rais wa Marekani, akiongeza; 

“Khan anawakilisha maadili ya maendeleo ya  London na nchi yetu.” 

Alionya akisema Trump ni mfano mzuri wa kuongezeka kwa vitisho dhidi ya haki duniani.

Jana mchana baada ya kuwasili Trump na mkewe Melania, walikutana na Malkia ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake hiyo ya kiserikali ya siku tatu nchini Uingereza.

Wawili hao waliandaliwa hafla ya kuwakaribisha na kisha kupata chakula faragha katika kasri ya Malkia.

Mara baada ya kuwasili, Trump na mkewe walipelekwa nyumbani kwa balozi wa Marekani.

Ziara yake hiyo imesababisha kuwapo kwa mipango ya maandamano katika majiji mengi ya Uingereza ikiwamo London, Manchester, Belfast, na Birmingham.

Mazungumzo kati ya Trump na Waziri Mkuu anayeondoka madarakani, Theresa May yanatarajia kufanyika leo na zaidi wakijikita katika masuala ya mabadiliko ya tabia ya nchi. 

Inaelezwa May ataibua suala la mabadiliko ya tabia ya nchi, huku msemaji wa Serikali jana kwa mara nyingine akisisitiza kuwa Uingereza “haikuwa imeridhishwa na uamuzi wa Marekani  kujiondoa katika makubaliano ya Paris  ya mwaka 2017”.

Mbali na hilo la tabia ya nchi, pia Trump na Waziri Mkuu huyo wanatarajia kujadili mgogoro wa Marekani na kampuni ya teknolojia ya China ya Huawei, hasa ikizingatiwa kuwa wakati Marekani wakiiorodhesha kwenye kitabu cheusi kampuni hiyo kwa sababu za kiusalama, Uingereza inaweza kuruhusu kusambaza vifaa vyake vya kwa ajili ya 5G.

Kumekuwa na vuta nikuvute kati ya Huawei na Marekani baada ya kumkamata binti wa mwanzilishi wa kampuni hiyo, Meng Wanzhou, Desemba mwaka jana, ambaye ndiye mhasibu mkuu wake.

Marekani inamtuhumu Meng na Huawei kwa tuhuma za kutakatisha fedha, ubadhirifu wa kibenki na kuiba siri za kibiashara mambo ambayo yanakanushwa na Huawei.

WAENDA PIA KUTALII 

Jana baada ya chakula cha mchana alichoshiriki pia Prince Harry, Rais Trump na mkewe  Melania pia waliandaliwa ziara katika eneo la kitalii la Westminster Abbey na pia kukutana na Prince Charles na mkewe Camilla kwa ajili ya kupata chai.

Tayari Rais Trump hajapoteza muda kuelezea mtazamo wake kuhusu uamuzi wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya akisema inapaswa kuchukua uamuzi huo na kukataa kulipa euro bilioni 45 za kujitoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles