WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani, Donald Trump ametia saini sheria itakayoruhusu kuagizwa kwa dawa zinazohitajika kwa bei nafuu kutoka nje.
Trump alitia saini maagizo manne yanayonuia kupunguza bei ya dawa kinyume na bunge ambalo linadhibitiwa na chama cha Democratic ambalo hadi sasa halijapitisha miswada kuhusiana na suala hilo.
Akizungumza kutoka ikulu, Trump alisema amechukua hatua hiyo ya ushupavu na kihistoria kupunguza bei ya dawa kwa ajili ya wamarekani wagonjwa na wazee.
Trump atakutana na wakuu wa kampuni za dawa siku ya Jumanne lakini baadhi ya wachambuzi wa masuala ya viwanda wamesema, hatua hiyo huenda isilete tofauti kubwa.
Katika taarifa, shirika la utafiti na utengenezaji dawa nchini Marekani limesema, serikali ya Trump imeamua kufuata sera hatari ya kudhibiti bei kulingana na viwango vinavyolipwa na mataifa ambayo Trump ameyataja kuwa ya kisoshalisti. Amesema sera hizo zitawaathiri wagonjwa kwa sasa na siku za usoni.