WAFUASI wenye msimamo mkali wa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, wamelalamikia uamuzi wake wa kuachana na ahadi yake ya kumkamata Hillary Clinton.
Maofisa wake walitangaza kuwa Trump atafutilia mbali ahadi yake ya kuteua mwendesha mashtaka maalumu, kuhakikisha mpinzani wake huyo wakati wa kinyang’anyiro cha urais wa Marekani anafungwa jela.
Lakini Trump baadaye alifafanua na kusema kuwa hatua kama hiyo inaweza kuzua migawanyiko zaidi.
Shirika la Upelelezi Marekani (FBI), lilimsafisha Hillary kuhusu kashfa ya kuhatarisha usalama wa taifa kwa kutumia barua pepe binafsi kwa masuala nyeti, lakini wafuasi wa Trump walikuwa wakiimba ‘mfunge jela’ kwenye mikutano yake ya kampeni.
Wafuasi wahafidhina sasa wanasema hatua hiyo ya Trump ni ‘usaliti’ na kwamba amevunja ahadi yake.
Tovuti ya Redstate.com imesema hatua ya Trump kutomteua mwendesha mashtaka maalumu wa kufuatilia tuhuma hizo dhidi ya Hillary, kama alivyokuwa ameahidi, itamfanya ahesabiwe kuwa aliropoka tu katika kampeni bila kuwa na nia ya dhati.
Tovuti ya mrengo wa kulia ya Breitbart News Network, moja ya zile zilizomuunga mkono Trump, pia ilishutumu hatua hiyo na kusema ni ‘ahadi iliyovunjwa’.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Ann Coulter, ambaye ni mhafidhina, naye alisema Trump alipaswa kuwaacha FBI na waendesha mashtaka kufanya kazi kwa uhuru na kwamba kazi yake ni kuwateua na si kufanya kazi zao.
Wakati wa kampeni, Trump alisema mpinzani wake alikuwa mtu mwovu na fisadi zaidi kuwahi kuwania urais wa Marekani, akaapa angehakikisha kesi zinafunguliwa dhidi yake.
Alimweleza kama mgombea mfisadi zaidi kuwahi kuwania urais nchini Marekani.
Lakini tangu uchaguzi kumalizika, alionekana kuanza kulegeza msimamo na wiki moja iliyopita, alisema familia ya Hillary ni ya ‘watu wema’.