BEIJING, CHINA
SERIKALI ya China imeeleza kutoridhishwa na azma ya Rais mteule Donald Trump kutaka kufutilia mbali sera ya Marekani kuhusu China moja, iwapo Beijing haitaridhia masuala mbalimbali yakiwamo ya kibiashara.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Geng Shuang, ameonya kuhusu kubatilisha au kutatiza sera ya ‘China Moja’ inayotoa mwongozo wa uhusiano kati ya Serikali ya Beijing na Taiwan, kisiwa inachokihesabu kuwa sehemu ya mkoa wake.
“Iwapo hilo litatokea, uhusiano kati ya China na Marekani pamoja na ushirikiano wa sekta mbalimbali kati ya mataifa haya mawili utakuwa jambo gumu kutekelezeka,” alionya Shuang.
Serikali ya China inalichukulia eneo la Taiwan kuwa muhimu katika uhuru wake na ulinzi wa mipaka yake, na uzingatiaji wa sera hiyo ya ‘China Moja’ ndicho kigezo cha kisiasa katika uhusiano wake na Marekani.
Shuang aliongeza kuwa matamshi hayo ya Trump wakati wa mahojiano kupitia runinga mwishoni mwa juma, yanatishia kusambaratisha uhusiano kati ya Marekani na China.
Kwa mujibu wa Trump, haoni sababu ya kuzingatia sera hiyo ya iwapo hawatakubaliana na China kuhusu masuala mbalimbali, ikiwamo biashara.
Aliilaumu China kwa kuiumiza Marekani na pia kutetea vikali hatua ya kuwasiliana kwa simu na Rais wa Taiwan, Tsai Ing-Wen.