WASHINGTON, MAREKANI
RAIS wa Marekani Donald Trump juzi aliyataka mataifa ya Ulaya yachukue mamia ya wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) nchini Syria, akitishia kuwa bila hivyo Marekani italazimika kuwaachia huru.
“Marekani inazitaka Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na mataifa mengine washirika wa Ulaya kuwachukua zaidi ya wapiganaji 800 ambao wamekamatwa Syria na kuwafikisha mahakamani,” rais huyo aliandika katika mfululizo wa maandishi yake kwenye akaunti yake ya Twitter.
“Eneo la Ukhalifa linakaribia kuanguka. Mbadala wake si mzuri kwa sababu tutalazimika kuwaachia huru. Marekani haitaki kuwa walinzi wa wapiganaji hawa wa ISIS kutoka Ulaya, ambako ndiko wanatarajiwa kwenda.
“Tunafanya mengi na tunatumia fedha nyingi, sasa wakati umefika wengine kuchukua jukumu hilo na kufanya kazi, ambayo wanaweza kuifanya.”
“Tunaondoa majeshi yetu baada ya ushindi wa asilimia 100 dhidi ya IS!”
Trump alisababisha wasi wasi mkubwa Desemba mwaka jana wakati alipotangaza ghafla kuwa Marekani itaondoa askari wake kutoka Syria na kwamba IS tayari limeshindwa.
Wakosoaji walionya kundi hilo halijashindwa wala kutokomezwa na kujiondoa kwa Marekani kunaweza kulifufua kwa vile washirika wa Marekani waliopo eneo hilo hawana uwezo wa kupambana na kitisho hicho peke yao.